1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sarkozy ataweza kweli kutimiza ahadi zake

Josephat Charo7 Mei 2007

Rais mpya wa Ufaransa atakuwa Nicholas Sarkozy. Baada ya kampenzi za kukata na shoka mwanasiasa huyo wa chama cha kikosavativ alimshinda mpinzani wake Segolen Royal katika uchaguzi wa jana.

https://p.dw.com/p/CB4G

Nicolas Sarkozy amefaulu baada ya kampeni kati ya wagombea wa vyama vya mrengo wa shoto na kulia wa uchaguzi wa rais nchini Ufaransa uliowavutia wapigaji kura wengi zaidi ikilinganishwa na chaguzi za awali. Ufaransa sasa inaelekea katika siasa za mrengo wa kulia baada ya Wafaransa kumchagua mgombea anayepigania kuilekeza nchi hiyo katika uchumi huru hata katika nyenzo za kiuchumi wa kitaifa. Sarkozy ni kiongozi anayetaka shughuli za serikali zipunguzwe na sheria dhidi ya wahamiaji zingoezewe makali.

Kwa matamshi ya kuvutia Sarkozy amefaulu kumshinda mwanasiasa wa mrengo wa shoto, Jean - Marie Le Pen. Sarkozy kwa mara nyengine amewarudishia hadhi wanasiasa wa mrengo wa kulia katika nchi ambayo idadi ya watu wasio na ajira imefikia kiwango cha juu zaidi ikilinganishwa na mataifa mengine ya Umoja wa Ulaya.

Mjadala mkali kwenye runinga kati ya ´Sego´ na ´Sarko´ kama Wafaransa wenyewe walivyouita, ulidhihirisha wazi kwamba Sarkozy ni mtaalamu wa siasa mtulivu lakini anayeelewa jinsi ya kupanga mikakati. Ni mtu anayefahamu takwimu na maswala mbalimbali lakini kwa upande mwingine bwana Sarkozy ameonekana kuwa mgeni mwenye hisia zinazobadilika ambaye tayari amewahi kuwa waziri katika serikali ya Ufaransa lakini akashindwa kujieleza kinaga ubaga mapendekezo yake ya kutatua matatizo yanayowakabili Wafaransa.

Je ni matarajio gani Umoja wa Ulaya na Ujerumani inayotazamia kutoka kwa bwana Nicholas Sarkozy? Kwa kweli hatarajiwi kusuluhisha matatizo ya kisiasa barani Ulaya. Umoja wa Ulaya haukujishuhgulisha sana na kampeni ya Sarkozy wala mpinzani wake Segoléne Royal. Kwa hiyo kuhusu swala hili ni Umoja wa Ulaya unaotakiwa kusaidia kuyatatua matatizo ya Ufaransa na wala sio Ufaransa kuusaidia Umoja wa Ulaya.

Kwa Ujerumani Sarkozy anayeonekana kuwa mgumu kukubali kufanya mazungumzo na ambaye kila mara amekuwa akipigania masilahi ya nchi yake, atakuwa mshirika mgumu wa kufanya naye mazungumzo. Wakati wa kampeni Sarkozy alitoa matamshi yasiyokubalika mara kadhaa akiwataja Wajerumani kuwa magaidi wa vita vya pili vya dunia na kusisitiza kwamba Ufaransa haikulazimika kufanya mauaji ya halaiki na baadaye kulazimika kutafuta suluhisho la kuyamaliza.

Tabia ya bwana Sarkozy kutoa matamshi hayo kwenye mikutano yake ya kampeni ni ya kushangaza na inaonyesha vipi mtu aliyetangaza anataka kuilekeza Ufaransa katika muongo mpya, anavyoweza kugeuka ghafla. Tunabaki tu kutumaini kwamba aliyoyasema Sarkozy wakati wa kampeni zake ni ukweli na wakati Ufaransa itakapochukua urais wa Umoja wa Ulaya mwishoni mwa mwezi Juni mwaka ujao, itaweza kutimiza jukumu lake kwa umahiri.

Sarkozy alisema katika hotuba yake baada ya kushinda uchaguzi kwamba atabakia kuwa mtu anyeunga mkono kwa dhati Umoja wa Ulaya. Ulimwengu mzima unatazama.