Sarkozy afanya ziara ya kihistoria Haiti | Masuala ya Jamii | DW | 18.02.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Masuala ya Jamii

Sarkozy afanya ziara ya kihistoria Haiti

Wamarekani waliotuhumiwa kuiba watoto wa Haiti waachiwa huru

Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy

Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy

Rais wa Ufaransa, Nicholas Sarkozy ameahidi kuipa Haiti msaada wa euro milioni 326 katika kipindi cha miaka miwili ijayo, kiwango kinachojumulisha kufutwa deni la nchi hiyo la euro milioni 56. Sarkozy ni rais wa kwanza wa Ufaransa na pia kutoka barani Ulaya kuitembelea Haiti tangu kisiwa hicho kukumbwa na tetemeko la ardhi mnamo Januari 12 mwaka huu, huku akiapa kutimiza ahadi za kihistoria za nchi yake kwa koloni hiyo ya zamani ya Ufaransa.

Ziara ya rais Sarkozy inafanyika zaidi ya mwezi mmoja tangu tetemeko kubwa la ardhi kutokea Haiti mnamo Januari 12 mwaka huu ambalo lilisababisha vifo vya watu 217,000 na kuwaacha wengine takriban milioni 1.2 bila makaazi.

Sarkozy alilakiwa na mwenyeji wake rais wa Haiti Rene Preval wakati alipowasili mjini Port-au-Prince. Rais Preval amesema anamkaribisha rais Sarkozy lakini angependelea kiongozi huyo azuru Haiti katika mazingira mengine na wala sio baada ya kutokea tetemeko la ardhi. "Nimekuja kuwahakikishia Wahaiti na viongozi wao kwamba Ufaransa itaendelea kuwasaidia kwa dhati kujenga upya taifa lenu na kufungua ukurasa mpya katika historia yao", amesema rais Sarkozy na kuongezea,

Kuwepo kwetu katika kisiwa hiki hapo zamani hakukuacha tu kumbukumbu nzuri. Makovu ya ukoloni na mazingira ya kutengana kwetu vimeacha kumbukumbu zisizoridhisha miongoni mwa Wahaiti. Msaada wa kimataifa unatakiwa kuwa mkubwa na utakaodumu kwa muda mrefu, lakini Wahaiti wanaweza kuamua juu ya miradi yao ya kitaifa ya kuijenga upya nchi yao.

Sarkozy amejionea kwa macho yake uharibifu uliotokea mjini Port-au-Prince na maeneo mengine yaliyopigwa na zilzala ya tetemeko la ardhi na kuitembelea hospitali iliyojengwa na maafisa wa misaada wa Ufaransa ambako alikutana na wahanga wa tetemeko hilo.

Maandamano yafanywa

Wakati huo huo, mamia ya waandamanaji wameandamana nje ya ikulu ya rais mjini Port-au-Prince wakimtaka rais Sarkozy atumie ushawishi wake ili rais wa zamani wa Haiti, Jean-Bertrand Aristide arejee nyumbani. Waandamanaji hao ambao walionekana kuwa vijana kutoka maeneo ya walalahoi mjini Port- au-Prince, walibeba mabango yaliyokuwa na ujumbe wa kutaka Arstide arudi Haiti asaidie kuijenga upya nchi hiyo.

Padri huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 56 na aliyependwa na watu maskini, alikuwa rais wa kwanza wa Haiti kuchaguliwa kidemokrasia, lakini akalazimika kuikimbia nchi hiyo kufuatia mapinduzi ya mwaka 2004 na sasa anaishi uhamishoni nchini Afrika Kusini.

Ziara ya rais Sarkozy nchini Haiti ni ya kwanza kuwahi kufanywa na rais wa Ufaransa katika kisiwa hicho cha Karibik kilichopigania na kupata uhuru wake mnamo mwaka 1804, na hivyo kuwa jamhuri ya kwanza ya watu weusi kuwa huru.

Sarkozy amewahimiza Wahaiti wawajibike kuijenga upya na kuiendeleza nchi yao akisema juhudi hizo zinatakiwa kuwa mradi wa kitaifa utakaoelekezwa mikoani na maeneo yaliyo nje ya mji mkuu Port-au-Prince.

Wamarekani waachiwa

Wakati huo huo, wamisionari wanane Wamarekani ambao walituhumiwa kwa kuwateka nyara na kuwasafirisha nje watoto 33 wa Haiti wamewasili Miami Marekani baada ya jaji wa mahakama ya Port-au-Prince kuamuru waachiwe huru. Kwa mujibu wa taarifa ya gazeti la Miami Herald, Wamarekani hao wamewasili muda mfupi baada ya sita usiku wa kuamkia leo. Jamaa zao wamefurahia kuachiwa kwao.

Wamarekani wengine wawili wangali wanazuiliwa kwa sababu hakimu huyo anataka kuchunguza nia yao ya kuitembelea Haiti kabla kutokea tetemeko la ardhi. Wakili wao amesema Wamarekani hao waliitembelea Haiti kusaidia kutoa huduma kwenye kituo kimoja cha kuwatunza watoto kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.

Mwandishi: Josephat Charo/ AFPE/Reuters

Imepitiwa: Hamidou Oummilkheir

 • Tarehe 18.02.2010
 • Mwandishi Josephat Nyiro Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/M4RG
 • Tarehe 18.02.2010
 • Mwandishi Josephat Nyiro Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/M4RG
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com