Sarah Palin ni mgombea mwenza wa uchaguzi wa urais Marekani | Matukio ya Kisiasa | DW | 02.09.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Sarah Palin ni mgombea mwenza wa uchaguzi wa urais Marekani

John McCain apata mgombea mwenza kwa urais wa Marekani

default

Sarah Palin, mgombea mwenza wa urais wa Marekani kwa tiketi ya Chama cha Republican, baada ya kujulishwa kwa wananchi na mgombea wa urais, John McCain

Mtetezi wa urais wa Chama cha Republican katika uchaguzi wa Marekani mwezi Novemba mwaka huu, John McCain, ijumaa iliopita alitimia umri wa miaka 72, hivyo Wamarekani kukumbushwa kwamba pindi watamchagua basi watakuwa na rais aliye mzee. Siku hiyo yake ya kuzaliwa ilikua ni siku moja baada ya yule anayeshindana naye kwa wadhifa huo kutoka Chama cha Democratic, Barack Obama, mwenye umri wa miaka 47, kutawazwa kwa vifijo na mbwembewe na mkutano mkuu wa Chama chake huko Denver, Colorado, kama mtu ambaye anegefaa kuiongoza Marekani katika miaka minne ijayo. Ilibdi John McCain aje na jibu ili kuuzuwia umaarufu anaozidi kuupata Barack Obama ambaye anamlinganisha mtetezi huo wa Republican na rais wa sasa, George Bush, rais ambaye umaarufu wake kwa Wamarekani uko chini kabisa kuwahi kufikiwa na rais yeyote wa hapo kabla. Silaha alioitumia McCain na kuushangaza ulimwengu ni kumteuwa gavana wa Mkoa wa Alaska, Sarah Palin, kama mgombea wake mwenza, akisema huyo ni mtu aliyemtaka kama vile Marekani inavomtaka:

" Ni kwa fahari na kwa shukrani nakuarifuni kwamba nimempata mshirika barabara wa kunisaidia kukabiliana na watu wanaothamini nafasi zao kuliko dhamana zao, wanaoweka madaraka juu ya misingi ya imani zao na kuweka maslahi yao mbele ya mahitaji yenu."

Aliendelea kusema:

"Rafiki zangu na Wamarekani wenzangu. Na furaha na na fahari kukujulisheni makamo wa rais wa baadae wa Marekani, gavana Sarah Palin wa Mkoa mkubwa wa Alaska."

Watu walipolisikia tu jina hilo walianza kuulizana ni nani huyo, ana sifa gani za kukamata wadhifa wa rais wa Marekani pindi McCain atakapokuwa anashindwa kutimiza majukumu yake au kujiuzulu? Si tu Bibi Sarah Palin alikuwa hajulikani katika majukwaa ya kimataifa, lakini hata huko Marekani kwenyewe sio watu wengi wanamjuwa nje ya mkoa wake.

Lakini dau aliwekewa kuweza kuzivutia kura za wanawake na watu wenye mawazo ya Ki-Conservative na pia kuleta mageuzi huko Washington, jambo ambalo Barack Obama anajigamba atalifanya pindi atashinda,

Mwenyewe John McCain alisema pindi watu watamjuwa Bibi Palin, basi watavutiwa naye kama yeye alivovutiwa. Alimuelezea mwanamke huyo kuwa mwanamageuzi, mtu asiyetafuna maneno hata katika kukilaumu chama chake cha Republican ambacho bibi huyo alikielezea wakati mmoja kuwa kina uhaba wa viongozi bora. Kinachojulikana juu ya Bibi Palin ni kwamba alipokuwa kijana aliwania kuwa bibi mrembo kabisa wa kijiji anachoishi cha Wassila, karibu na mji mkuu wa Mkoa wa Alaska, Anchorage, lakini baadae kwa haraka akapanda katika nyadhifa za juu za kisiasa, kuwa meya wa kwanza wa kike wa mji wa Wassilla, baadae kuwa mwenyekiti wa tume ya mkoa ya Gesi na Mafuta, na mwaka 2006 kuwa gavana wa kwanza wa kike wa Mkoa wa Alaska, tena aliye kijana kabisa.

Uamuzi huu unaonekana wazi kuwa ni mbinu ya Seneta John McCain kuzivutia kura za wanawake na wafuasi milioni 18 ambao wamevunjika moyo kwamba mtu waliyemtaka kuwa rais wa Marekani, Bibi Hilary Clinton, hajaweza kuchanguliwa na Wa-Democratic kuwa mtetezi wa urais, na hata hajaambulia kuwa mgombea mwenza wa Barack Obama. Mgombea huyo mwenza wa Chama cha Republican anaunga mkono kuchimbuliwa mafuta ili Marekani isitegemee nchi za nje kwa nishati hiyo. Aliwahi kusema hivi:

"Wanasiasa ambao hawatambuwi kwamba Marekani lazima ijitegemee katika siasa za nishati, wanasiasa hao ni wa kutoka nchi ya ndoto."

Yeye ni mwenye mawazo ya Ki-Conservative katika masuala ya kijamii. Waumini wa madhehebu ya Kiinjili waliusifu uamuzi wa Sarah Palin aliochukuwa mwaka jana wa kuibeba mimba hadi kuzaa mtoto wake wa tano, akijuwa wazi kwamba mtoto huyo atakayemzaa atakuwa na matatizo ya akili taahira. Asilimia 80 ya mimba za watoto wa aina hiyo hutolewa huko Marekani. Hivyo alidhihirisha wazi kwamba anapinga kabisa utoaji mimba. Na pale alipojulishwa kwa waandishi wa habari kama mgombea mwenza, alikuwa na mtoto wake mchanga, akiwaacha waandishi wa habari wangoje kumuuliza masuali wakati anambadilisha winda mwanawe.

John McCain alitaka ubavuni mwake awe na mtu aliye na historia ya kupambana na siasa za ufisadi pamoja na siasa zilizoshindwa hapo kabla, mtu ambaye siasa zake za kabla zimedhihirisha kwamba ni mkakamavu na mwenye ujuzi wa kukabiliana na matatizo magumu. McCaian alimuelezea mshirika wake kuwa ana moyo wa kupigana, tena mwenye huruma kabisa. Hajakosea. Mazungunmzo mengi ya wiki zilizopita yalitwama katika zile tetesi kwamba John McCain anegemteuwa gavanana wa zamanai wa Mkoa wa Massachusetts, Mitt Romney

Lakini kambi ya Barack Obama haijapoteza wakati kabla ya kumshambulia na kumkejeli Bibi Sarah Palin, wakisema bibi huyo alikuwa tu meya wa mji wenye wakaazi 9,000, bila ya kuwa na ujuzi hata kidogo wa siasa za kigeni. Ikiwa Barack Obama alikuwa anatajwa kuwa hana ujuzi wa siasa za kigeni, ni miaka minne tu tangu alipkuwa seneta, mtu atasemaje juu ya Sarah Palin. Na vipi bibi huyu ataweza kuhimili vishindo vya mgombea mwenza wa Chama cha Democratic, Seneta Joe Biden, mtu aliyebobea katika masuala ya siasa za kigeni, pale watakapokutanishwa katika malumbano ndani ya televisheni?

Wahakiki wana wasiwasi kama kweli njama hiyo ya John McCainya kumteuwa Sarah Palin kuwa mgombea mwenza itamsaidia kuvutia kura za wanawake, kwani wengine, kama vile Seneta John Kerry wanaiona mbinu hiyo kuwa ni tusi kwa wanawake wa kila mahala kwa vile inachukulia kwamba jinsia ni muhimu zaidi kuliko siasa anazowakilisha mtu.

Kama Bibi Palin atavutia kura za akina mama kama vile alivovovutia Hilary Clinton, hivyo kumfaidia John McCain, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mkoa wa Indiana, Dr. Alawia Omar alinijibu hivi:

Lakini Sarah Palin alikuwa na hili la kusema kuhusu suala la jinsia:

" Yaonesha wanawake wa Marekani hawajamalizika bado, na tunaweza kuivunja kabisa kabisa ile dari ya glasi ya mtengano."

Onyo limetolewa kwa Wa-demokratic wasimdharau Bibi Palin na kujiamini kushinda kiasi hata kumbeza bibi huyo, kwani hali hiyo inaweza ikampatia huruma miongoni mwa wapigaji kura. Kwa vyovyote John McCain ameingiza ujoto katika msimu huu wa kampeni za chaguzi. Maafisa wa Chama cha Republican wanahisi McCain ametatua tatizo kwa kumteuwa Bibi Palin ambaye amefurahiwa na Wakristo wa madehehbu ya Kiinjili, watu wale wale waliomsaidia sana George Bush kuingia Ikulu mjini Washington mwaka 2000 na mwaka 2004.


 • Tarehe 02.09.2008
 • Mwandishi Othman, Miraji
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/FA0S
 • Tarehe 02.09.2008
 • Mwandishi Othman, Miraji
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/FA0S
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com