1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sarah Palin amshambulia vikali Barack Obama

Saumu Mwasimba4 Septemba 2008

Hotuba yake imewafurahisha sana wafuasi wa chama hicho

https://p.dw.com/p/FB1x
Picha: AP/ABC News

Mkutano mkuu wa chama cha Republican unaendelea huko Minessota ambapo mgombea mwenza wa John McCain Sarah Palin amekubali rasmi uteuzi wa kuwania kiti cha makamu wa rais.

Gavana huyo wa jimbo la Akaska amewahutubia maelfu ya wafuasi wa chama cha Republican baada ya kuandamwa na vyombo vya habari kuhusiana na rekodi yake.

Sarah Palin amemsifu John MCcain akisema ameipigania nchi yake kwa muda mrefu na yuko tayari kuendelea kuipigania katika kuleta mageuzi nchini humo.

Aidha amemkosoa mgombea wa urais wa chama cha Demokratic Barack Obama akisema kwamba hana uzoefu katika masuala yanayohusu sera za nje na pia katika kuilinda Marekani dhidi ya magaidi.

Magavana wa zamani Mitt Romney na Mike Huckabee waliufungua mkutano huo hivi punde wakimuunga mkono na kumsifu mgombea wa chama hicho John McCain na kuwakosoa vikali wademoktas.

John McCain anatazamiwa kuteuliwa rasmi kuwa mgombea wa urais wa chama hicho baadae leo.