1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sababu za Kim Jong Un kutoonekana hadharani zatolewa

Saleh Mwanamilongo
28 Aprili 2020

Huenda hofu ya kuambukizwa virusi vya Corona ndio imesababisha kutoonekana hadharani kwa kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un amesema waziri wa muungano wa Korea ya Kusini baada ya uvumi kuhusu afya ya kiongozi huyo

https://p.dw.com/p/3bWW8
Nordkorea | Machthaber Kim Jong Un
Picha: picture-alliance/AP Photo/Korea News

Kim Jong Un hakuhudhuria katika hafla ya Aprili 15, ambayo huandaliwa kila mwaka ya kumuenzi babu yake na muanzilishi wa taifa hilo, Kim II Sung, jambo ambalo limepelekea uvumi kuhusu afya yake.

Hata hivyo, Korea ya Kusini ilikanusha uvumi huo kuhusu kiongozi wa Korea ya Kaskazini. Kim Yeon-Chul, waziri wa muungano wa Korea ya Kusini na anayeshughulikia maswala ya Korea ya Kaskazini, ameliambia bunge la nchi yake kwamba huenda Kim Jong Un alihofia kuambukizwa na virusi vya Corona , kutokana na hatua kali zilizochukuliwa na nchi hiyo katika kupambana na virusi hivyo hatari.

Yeon-Chul alisema ni kweli kwamba toka achukuwe madaraka Kim Jong Un hajawahi kutohudhuria hafla ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Kim II Sung, lakini sherehe kadhaa na dhifa zilizoandaliwa kwa ajili ya maadhimisho hayo zilifutwa kutokana na tatizo la Corona.

"Sidhani kwamba ni jambo lisilo la kawaida, licha ya kwamba Korea ya Kaskazini ilielezea kwamba haijarikodi mtu hata mmoja aliyeambukizwa corona," aliendelea kusema Kim Yeon-Chul.

Waziri huyo wa Korea ya Kusini ameelezea kwamba toka Januari kuna matukio mawili ambayo Kim Jong Un hajaonekana hadharani kwa kipindi cha takriban siku 20.

Mara ya mwisho kwa Kim Jong Un kuongoza kikao ilikuwa ni April 11

Kim Yo Jong Nordkorea
Dadake kiongozi wa Korea ya Kaskazini Kim Jong Un, Kim Yo JongPicha: Getty Images/P. Semansky

Mara ya mwisho televisheni ya taifa kumuonesha Kim Jong Un akiongoza kikao ilikuwa ni April 11, lakini hatimaye kila siku kumekuwa na ujumbe au barua ya kidiplomasia ya rais huyo inayotangazwa kupitia vyombo vya habari vya kitaifa.

Maafisa wa Korea ya Kusini wamesisitiza kuwa hawajaona tukio lolote lisilo la kawaida kwenye nchi jirani ya Korea ya Kaskazini, na wamepuuzia taarifa kuhusu Kim John Un kwamba ni mgonjwa.

Waziri huyo wa muungano wa Korea ya Kusini aliziita taarifa kuhusu kiongozi huyo wa Korea Kaskazini kufanyiwa upasuaji wa moyo na kwamba madaktari kutoka China walikwenda nchini Korea Kaskazini kuwa za uzushi.

Siku ya Jumatatu, likiwataja maafisa watatu wanaofahamu hali huko Korea ya Kaskaini, shirika la habari la Reuters lilielezea kwamba ujumbe ukiwemo madakatari kutoka China walikwenda Korea ya Kaskazini kutoa ushauri kuhusu Kim Jong Un, lakini haifahamiki wazi kuhusu safari hiyo kulingana na hali ya afya ya kiongozi huyo.

Rais wa Marekani Donald Trump alielezea Jumatatu kwamba anaufahamu kuhusu hali ya afya ya Kim Jong Un na anatumaini kwamba anaendelea vyema.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Japan Shinzo Abe alisema kwamba ana taarifa kuhusu hali ya afya ya Kim na anafuatilia kwa karibu swala hilo.

Korea ya Kaskazini ilifuta baadhi ya matukio kadhaa na kufunga mipaka yake na kuchukuwa hatua za karantini katika juhudi za kuepuka ugonjwa wa COVID-19.

Chad O'Caroll, mkuu wa shirika la Korea Group Crisis, linalofuatiiakwa karibu hali nchini Korea ya Kaskazini, amesema kwamba ikiwa Kim amekuwa akihofia kuambukizwa virusi vya Corona, basi ni rahisi kutoa picha ama video zinazomuonyesha akiwa hai.

Duru mojawapo yenye uhusiano na idara za kiusalama za Marekani ilielezea Jumatatu kwamba inawezekana Kim kajificha kutoonekana hadharani kutokana na ugonjwa wa COVID-19, huku ikielezea kwamba treni ya rais huyo ilionekana kwenye kituo kimoja cha utalii nchini humo cha Wonsan.

"Huenda yuko huko ama alikuwepo huko siku za hivi karibuni", ilielezea duru hiyo.