1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 4 wakamatwa Rwanda wakijaribu kutorosha pembe za ndovu

28 Oktoba 2021

Polisi wa Rwanda inawashikilia watu wanne waliokamatwa Kigali wakijaribu kutorosha pembe za ndovu zenye uzito wa kilo 45. Mzigo huo ulikuwa ukisafirishwa kupitia Rwanda hadi katika nchi za bara la Asia.

https://p.dw.com/p/42HfR
Singapur Beschlagnahmtes Elfenbein
Picha: picture-alliance/Xinhua/Then Chih Wey

Kwa maelezo ya taasisi ya taifa ya upelelezi na makosa ya jinai RIB shehena ya pembe za ndovu zenye uzito huo wa kilo 45 zilikuwa zikisafirishwa kutoka mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo kwenda barani Asia.

Shehena hiyo ilisafirishwa katika gari lenye nambari za usajili wa kampuni ya umeme ya nchi za maziwa makuu, kwa kifupi SINELAC ambayo inazishirikisha nchi za Rwanda, Burundi na Kongo ikiwa na makao yake mjini Bukavu.

Mwanadiplomasia miongoni mwa waliokamatwa

Miongoni mwa waliokamatwa yumo mwanadiplomasia wa Rwanda ambaye ndiye mmiliki wa gari hilo lililobeba shehena hiyo. Hata hivyo, maafisa wa usalama wameomba majina yake yasitajwe wakati akihojiwa na vyombo vya habari. Wote wanne walikamatwa kwa nyakati tofauti kwa mujibu wa maelezo ya msemaji wa taasisi ya taifa ya upelelezi na makosa ya jinai Dk. Thierry Murangira

“Hawa walikamatwa walipokuwa wakijaribu kuingiza shehena hii ya pembe za ndovu. Upelelezi wa awali unatuonyesha kwamba walinuia kuziuza pembe hizi katika mataifa ya Asia, na hapa Rwanda ilikuwa ikitumiwa kama njia ya kupitia tu. Hizi pembe za ndovu hazikuibwa hapa Rwanda, hapana isipokuwa ni njia tu ya wahalifu. Kukamatwa kwa hawa washukiwa kunatoa taarifa kwa watu wengine wenye mipango kama hii kwamba Rwanda si salama kwa wahalifu wanaopora mali za nchi jirani,” alifafanua Dk. Murangira

Soma zaidi: Ndovu barani Afrika waathirika na uwindaji haramu

Msemaji huyo wa taasisi ya upelelezina makosa ya jinai nchini Rwanda amesema kwamba ushirikiano unaendelea kuwepo baina ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo na Rwanda kurahisisha kupunguza visa vya uhalifu ambavyo vimekuwa vikiripotiwa katika mipaka ya nchi hizo mbili.

Mapema mwezi Juni mwaka huu marais wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo na Rwanda walikutana mjini Goma mashariki mwa Kongo ambapo viongozi wa pande hizo mbili walitia saini makubaliano ya ushirikiano katika sekta mbalimbali, zikiwemo usalama na biashara. Matokeo yake sasa ndege ya shirika la ndege la Rwanda, Rwandair inafanya safari za kila wiki katika miji ya Kinshasa, Lubumbashi na Goma mashariki mwa Kongo.