1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rwanda yaongoza katika teknolojia ya habari na mawasiliano barani Afrika

Josephat Charo5 Julai 2007

Kabla miaka 15 kumalizika tangu mauji ya halaiki yaliyoharibu nguvu kazi ya Rwanda, miundombinu na sekta ya kijamii na kiuchumi, Rwanda sasa inakaribia kuwa shina la teknolojia ya habari na mawasiliano, ICT, barani Afrika.

https://p.dw.com/p/CHkJ
Rais Paul Kagame wa Rwanda
Rais Paul Kagame wa RwandaPicha: AP

Ufanisi wa Rwanda katika teknolojia ya habari na mawasiliano inafuatia juhudi za serikali kuendeleza miundombinu ya mawasiliano, ikiwa ni pamoja na simu za mkono, mifumo ya mawasiliano ya fibre optic, kuwawezesha watu kuifikia mitambo ya kompyuta na mtandao wa mawasiliano wa internet. Miundombinu ya mawasiliano nchini Rwanda imekuwa kivutio kikubwa kwa wawekezaji wa serikali za kigeni na wawekezaji binafsi wa kimataifa.

Rwanda imetangazwa kuchukua nafasi ya kwanza katika teknolojia ya habari na mawasiliano kwenye eneo la mashariki ya kati na shirika la biashara na maendeleo la Umoja wa Mataifa, UNCTAD. Nchi hiyo imenufaika kutokana na uwekezaji wa makampuni makubwa ya kimataifa yakiwemo Microsoft, Nokia na Terracom.

Bajeti ya Rwanda ya sekta ya habari na mawasiliano iko katika kiwango cha asilimia 1.6 sawa na mataifa wanachama wa shirika la ushirikiano wa kiuchumi na maendeleo, OECD, kundi la nchi 30 tajiri. Kiwango hicho cha bajeti kiko juu ya kiwango cha nchi za Afrika.

Ikikabiliwa na hali ngumu ya kiuchumi mnamo mwaka wa 1994, Rwanda ilizindua mpango uliojulikana kwa jina Vision 2020 mnamo mwaka wa 2000, ili kuufufua na kuumarisha uchumi wake. Mpango huo pia unalenga kuinua viwango vya mishahara kufikia tabaka la kati ifikapo mwaka wa 2020.

Andrew Mack, mfanyikazi wa zamani wa benki ya dunia na anayechangia mara kwa mara nakala katika jarida kuhusu uchumi barani Afrika la Africa Businnes Week, amesema sehemu moja wapo ngumu ya kazi ni kuhakikisha uwekezaji na hasa sera zinaleta faida kubwa. Rais wa Rwanda, Paul Kagame, amefaulu kufalifanikisha hilo, akihimiza sera nzuri za teknolojia ya habari na mawasiliano na wakati huo huo kuunga mkono mazingira mazuri ya kibiashara.

Huku mpango wa Vison 2020 ukizingatia maswala ya kilimo, viwanda na kijamii, ukosefu wa bandari nchini Rwanda, kodi kubwa inayotozwa bidhaa zinazosafirishwa kwa njia ya ndege na hali ya wasiwasi yote haya yaliilazimu serikali ya Rwanda kuwekeza katika uchumi unaozingatia maarifa shina likiwa teknolojia ya habari na mawasiliano.

Ukizindua miradi ya utafiti wa kisayansi na elimu, uvumbuzi wa kiteknolojia na usambazaji wa mawasiliano ya simu, mpango wa Vision 2020, ulilenga kuandaa wanasayansi wenye ujuzi wa hali ya juu na mafundi ili kukidhi mahitaji ya uchumi wa kitaifa ambao ungejumulishwa katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa Wanyarwandwa wote.

Serikali zinazotoa udhamini wa kifedha nazo pia zimejiunga na juhudi za kuendeleza teknolojia ya habari na mawasilaino. Mwezi uliopita idara inayohusika na maendeleo ya kimataifa, DFID nchini Uingereza, ilitangaza kwamba itazindua mradi utakaogharimu paundi laki saba ikishirikina na serikali ya Rwanda na benki ya dunia kutafiti maendeleo ya kisayansi na kiteknolojia na kukua kwa uchumi nchini Rwanda.