Rwanda na DRC zalaumiana kukiukwa kwa mkataba wa amani
10 Desemba 2025
Hii ni baada ya waasi wa M23 kudaiwa kuukamata mji muhimu wa Uvira unaopakana na Burundi. Rais wa Kongo Felix Tshisekedi, ameitaka jumuiya ya kimataifa kuiwajibisha Rwanda kuhusu kufadhili mauaji katika nchi yake huku Rwanda ikizishutumu Kongo na Burundi kwa kukiuka kwa makusudi mkataba huo wa Washington.
Kauli ya Rais Tshisekedi imetolewa wakati ambapo taarifa za waasi wa AFC/M23 kuingia katika mji wa kimkakati wa Uvira ulioko kwenye jimbo la Kivu Kusini zikiwa zinaripotiwa. Rais wa Kongo amesema kwamba Rwanda imekuwa ya kwanza kuuvunja mkataba wa kuleta amani mashariki mwa nchi yake uliosainiwa mjini Washington Desember 4 mwaka huu kati yake na Rais Paul Kagame wa Rwanda.
Tshisekedi ameendelea kusema kuwa kukamatwa kwa miji muhimu mashariki mwa DRC na jeshi la waasi wa M23 ambao yeye anasema wanasaidiwa na Rwanda ni ushahidi kwamba Rwanda inaendelea kuuvunja mkataba huo.
DRC: Hali ilivyo Uvira ni ushahidi Rwanda haitaki amani
Naye Waziri Mkuu wa Kongo Judith Suminwa Tuluka amesema katika kikao maalum na cha dharura na viongozi wa serikali kuhusu hali ya mambo mashariki mwa nchi hiyo kuwa huu ni ushahidi tosha Rwanda haitaki amani na kwamba serikali yake inajiandaa kutekeleza mikakati yote kuhusu kukabiliana na uvamizi wa waasi hao.
Kwa upande mwingine usiku wa kuamkia leo kundi la mataifa 10 ya Ulaya pamoja na Marekani kupitia muungano wao katika eneo la Maziwa Makuu limetoa tamko kali kuhusu hali ya usalama kuendelea kuharibika mashariki mwa Kongo. Kundi hilo limesema kuwa linasikitishwa na vitendo vya mashambulizi kwa kutumia silaha nzito na droni na kuitaka Rwanda na waasi wa M23 kuondoka eneo la Kivu Kaskazini na Kusini huku pia pande zote zinazohasimiana zikitakiwa kuuheshimu mkataba wa amani.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Goma ambao ni makao makuu ya kundi la AFC/M23 mkuu wa kundi hilo Corneille Nangaa amepuuzilia mbali madai ya serikali ya Kinshasa na wadau wengine kama yasiyo na msingi huku akiongeza kusema kuwa Kinshasa imeshindwa kuwalinda wananchi wake hasa mjini Uvira sababu ambayo wao inawafanya kuingilia kati kwa ajili ya kuwatetea raia.
M23 na madai ya serikali ya DRC kushindwa kuwalinda raia
Nangaa amenukuliwa akisema "Kwa zaidi ya miezi mitatu, kumekuwa na vurugu huko Uvira. Na hili ni kwa sababu ya uwepo wa vikosi tofauti visivyo na uongozi wala mwelekeo. Kwa hiyo, baada ya vikosi vya Burundi kujiondoa, jeshi la Kongo na Wazalendo walianza kupigana wao kwa wao. Inavyoonekana, sasa wameamua kuuacha mji huo kutokana na hofu na kuwatelekeza raia. Labda mtu atajiuliza tutakachokifanya. Sisi tutawalinda wananchi na hatutaruhusu vurugu hizi kuendelea kwa muda mrefu. Lazima tujipange ili kurejesha hali ya utulivu."
Mapema asubuhi ya leo Rwanda imetoa kauli kali katika kile kilichoonekana kama kujibu shutuma dhidi yake. Tangazo la serikali ya Rwanda limezilaumu nchi za Kongo na Burundi kuharibu kwa maksudi utekelezaji wa mkataba wa Washington kwa kuamua kuanzisha mashambulizi dhidi ya wananchi katika maeneo yanayokaliwa na waasi karibu na mpaka wa Rwanda na Kongo.
Msemaji wa serikali ya Rwanda kupitia tangazo hilo akasema ni kutokana na mashambulizi ya jeshi la Burundi na Kongo ambako kuliwafanya wakimbizi elfu 10 wa Kongokukimbilia Rwanda kupitia mpaka wa Bugarama kusini mwa Rwanda ambako sasa wanaendelea kuhifadhiwa katika kambi ya muda ya Nyarushishi.
Rwanda imeilaumu Burundi kwa kuwakusanya wanajeshi wake zaidi ya elfu 20 katika mpaka wake na Rwanda hata wakati ambapo mkataba wa Washington ulikuwa ukisainiwa. Kupitia tangazo hilo, Rwanda imeilaumu pia jumuiya ya kimataifa kwa kufumbia macho ushirika uliopo baina ya Burundi, serikali ya Kongo na kundi la waasi wa kihutu wa FDLR ambao wanaendelea kupanga mikakati ya kuuangusha utawala wa Kigali.