Rwanda kufanya uchaguzi Jumatatu | Matukio ya Kisiasa | DW | 06.08.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Rwanda kufanya uchaguzi Jumatatu

Siku ya Jumatatu , utafanyika uchaguzi wa rais katika nchi ndogo ya Rwanda nchi iliyopo katika eneo la Afrika ya kati.

Rais Kagame akiwa katika mkutano wa kampeni ya uchaguzi.

Rais Kagame akiwa katika mkutano wa kampeni ya uchaguzi.

Siku ya Jumatatu , utafanyika uchaguzi wa rais katika nchi ndogo ya Rwanda, iliyopo katika eneo la Afrika ya kati. Kwa hivi sasa rais Paul Kagame hukusanya maelfu ya makundi ya Wanyarwanda katika kampeni zake. Maelfu ya watu hufurahia na kuimba nyimbo za kumsifu. Kwa watu wa Rwanda, Kagame ni kiongozi pekee ambaye anaweza kuhakikisha hali ya amani na uthabiti.

Lakini bado linatanda wingu la mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 katika historia ya Rwanda. Na Kagame anajiona kuwa ndie binafsi anaweza kutatua na kuhakikisha kwamba wingu hili jeusi halirejei tena nchini humo. Hakuna shaka kabisa kwamba siku ya Jumatatu katika uchaguzi wa rais atashinda kwa asilimia 90. Lakini pia amevitendea ukatili mkubwa baadhi ya vyama vya upinzani , na baadhi kuvifanya kuwa vibaraka wake katika demokrasia inayoonekana kuwa kama mchezo wa kuigiza. Vyama vya upinzani binafsi vimesalim amri, na kumuunga mkono Kagame.

Inasikika kama ni tamasha la muziki katika kampeni za uchaguzi za Kagame. Katika eneo kubwa la wazi baina ya vilima vikubwa, mashariki ya Rwanda, kuna maelfu ya watu waliokusanyika. Wamevalia fulana zenye picha ya Kagame na kupepea vibendera vya rangi ya buluu, nyeupe na nyekundu, rangi za bendera ya chama tawala nchini Rwanda, FPR. Na wanaimba wimbo wa kumsifu Kagame.

Hali ni ya joto majira ya mchana. Na watu wanatoka jasho, na wana kiu. Katika eneo lote, watu hawa wamekuja hapa tangu asubuhi na mapema wakisafirishwa kuja katika eneo hili kwa mabasi. Watoto, wanawake wakiwa na watoto, wazee na wasio jiweza, vilema wakiwa katika vigari vya kujisukuma. Mbinyo kwa jamii ni mkubwa , nchini Rwanda ni wajibu kwa kila mtu kuwa mzalendo na kumuunga mkono Kagame, ambaye anajiona kuwa ndio mtatuzi wa wingu jeusi la mauaji ya kimbari mwaka 1994, na pia kama mtu anayeweza kuhakikisha makabila mawili ya Wahutu na Watutsi kuishi pamoja, anasema Taye Manzi. Mzee huyu yuko katika kundi kubwa la watu na amevaa fulana yenye picha ya Kagame na kofia.

Ametuletea amani, na kuijenga nchi yetu. Yeye ni pekee ambaye ameweza kufanikisha kuwaunganisha watu wetu. Anawasaidia vijana na wanawake. Tunafahamu kuwa demokrasia ni hatua. Na tuna matumaini kwamba atafanikisha kile alichotuahidi pamoja na mambo mengine zaidi.

Kagame binafsi anazungumzia mengi kuhusu demokrasia katika uchaguzi huu. Imekuwa ndio mada kuu, kwa kuwa jumuiya ya kimataifa haikubaliani na demokrasia yenye mapungufu. Kagame alichaguliwa kwa asilimia 90 miaka saba iliyopita. Hakuna mtu mwenye kutia shaka , kwamba mara hii atapata zaidi ya asilimia 90 ya kura . Lakini watu wanamhakikishia kupata asilimia 100 katika mikutano wa hadhara. Na Kagame anasema katika moja ya hotuba zake kuwa asilimia 100 pia ni demokrasia. Kwa jinsi hali inavyoonekana nchini Rwanda hivi sasa ni mchezo wa kuigiza wa vyama vya siasa katika demokrasia. Kwa sababu hata vyama vya upinzani vinamuunga mkono rais.

Kusini mwa Rwanda chama cha Kiliberali kinafanya mkutano wake wa hadhara. Kiasi cha watoto 20 wanacheza katika uwanja , watu wachache wamehudhuria na wanataka kupewa fulana hizi zinatolewa bure. Chama cha Kiliberali kina uwakilishi bungeni. Kinatumiwa na chama tawala cha rais Kagame ili kuonyesha kuwa kuna demokrasia, anasema makamu mwenyekiti wa kundi la vyama vya eneo hilo, ambae kutokana na hofu hakutaka jina lake lijulikane. Yuko kiwanjani hapo na anagawa fulana za rangi ya kijani.

Hatuna wapiga kura wengi , kama unavyoona leo hapa. Tumefadhiliwa na chama tawala cha FPR. Katika chama chetu tunafanya kazi kwa ushirikiano. Kila tunachokifanya ni lazima kiwe kimeidhinishwa na FPR. Hayo ndio makubaliano. Tunafurahi kwa hilo. Uchaguzi kwetu sisi hauna tatizo.

Victoire Ingabire

Victoire Ingabire,mmoja wa wanasiasa wa upinzani aliyewahi kukamatwa.

Nchini Rwanda wapinzani wanahofu dhidi ya kupambana na Kagame na kutoa mtazamo mbadala. Kwa sababu kile ambacho wanasiasa wa upinzani kilichowatokea katika miezi iliyopita ni ukatili wa wazi. Frank Habineza yuko katika ofisi yake ndogo na ana hofu kubwa. Hawezi hata kutembea mitaani. Habineza ni mwenyekiti wa chama cha kijani. Amejaribu katika miezi iliyopita , kukiandikisha chama chake. Wafuasi wake ni wafuasi wa zamani wa chama cha Kagame, ambao wamekihama. lakini sasa Habineza ana wasiwasi na maisha yake. Mmoja wa wawakilishi wake amekutwa amekatwa kichwa wiki tatu zilizopita.

Hali yetu ilikuwa si nzuri tangu kabla ya hapa, lakini hivi sasa hali ni mbaya sana. Tulijaribu kukiandikisha chama chetu mwezi Mei. Hatukupata jibu lolote kutoka serikalini. Siku chache baadaye, makamu wa chama chetu aliuwawa. Tuna matumaini kwamba baada ya uchaguzi huu, hali itakuwa nzuri. Hatukati tamaa. Tunajitayarisha na uchaguzi ujao mwaka 2013. Hata hivyo, inatisha. Kwa sasa tunalalamikia kuhusu hali ya kutokuwa na demokrasia, kwa hivi sasa tuna hofu ya maisha yetu. Naomba nifungwe tu , na sio kupoteza maisha.

Ndio sababu Habineza ameamua, kukimbilia nje ya nchi. Hasa kwa wakati huu wa uchaguzi. Anataka kupata hifadhi ya kisiasa nchini Ujerumani. Mapambano ya uchaguzi yanaendelea nchini Rwanda.

Mwandishi : Simone Schlindwein / ZR / Sekione Kitojo.

Mhariri : Othman Miraji.

 • Tarehe 06.08.2010
 • Mwandishi Sekione Kitojo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Oe7P
 • Tarehe 06.08.2010
 • Mwandishi Sekione Kitojo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Oe7P
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com