Russia: Mwaka mmoja tangu Putin akabidhi madaraka kwa Medvedev | Matukio ya Kisiasa | DW | 06.05.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Russia: Mwaka mmoja tangu Putin akabidhi madaraka kwa Medvedev

Mwaka mmoja tangu Putin kujiengua kama rais wa Russia

Rais Dmitry Medvedev wa Russia( kulia) na waziri mkuu, Vladimir Putin

Rais Dmitry Medvedev wa Russia( kulia) na waziri mkuu, Vladimir Putin

Vladimir Putin alikuwa nyota inayong'ara katika siasa za Russia, lakini mwaka mmoja sasa tangu aache urais wa nchi hiyo na kuwa waziri mkuu, nyota hiyo inapungua mn 'garo wake. Zile picha zake za ushujaa alipokuwa katika mawindo ya wanyama porini, pale alipozitishia kuzishambulia nchi jirani kwa silaha za kinyukliya au pale alipozuwia nishati ya Russia kwenda katika nchi nyingine za Ulaya, yote hayo yalionesha kwamba mwanasiasa huyo ana uwezo wa kubakia akimeremeta katika kilele cha siasa. Lakini, licha ya tetesi zilizosheheni kwamba Vladimir Putin mwishowe atarejea tena kuwa rais wa Russia, mabingwa wa kisiasa wanasema mambo haymwendei uzuri kachero huyo wa zamani wa Shirika la ujasusi la KGB, ikiwa ni mwaka mmoja baada ya yeye kukabidhi wadhifa wa urais kwa Dmitry Medvedev hapo Mei 7, 2008.

Wanadiplomasia na wachunguzi wa mambo wanasema yale mafungamano baina ya Vladimir Putin na Dmitry Medvedev yamepelekea kuweko vurugu juu ya mipaka ya madaraka ya kila mmoja wao. Jambo lililoyadhuru zaidi madaraka ya Putin ni mzozo wa kiuchumi ambapo maelfu ya nafasi za kazi zimepotea, sekta ya mabenki, kwa sehemu, imewacha kuweko, na sarafu ya Russia imekwenda chini thamani yake. Hali ya mambo iliozorota, ukosefu wa nafasi za kazi unaozidi, ughali wa maisha unaopanda, yote hayo yameiharibu sifa yake. Lakini sio kwamba Putin amemalizika. Uchunguzi uliofanywa mwezi uliopita umeonesha asilimia 76 ya watu walioulizwa wanaupenda uongozi wake, kiwango cha umaarufu kinachohusudiwa na wanasiasa wa nchi za Magharibi.

Mzozo wa kiuchumi wa hivi sasa umemchochea Putin aoneshe nguvu zake za kuweza kuwasiliana na watu. Lakini pale Russia itakapokuwa na gwaride la kijeshi la kila mwaka hapo Mei 9, desturi ambayo Vladimir Putin aliianzisha, wananchi hawatavutiwa sana kama ilivokuwa japo zamani. Kuna manunguniko yanayozidi kuhusu Putin, na Dmitry Oreshkin, wa Taasisi ya sayansi ya Russia, anasema katika nchi kama yake, matokeo ya uchunguzi wa maoni ya wananchi hayana umuhimu mkubwa sana kuliko manunguniko yalioko miongoni mwa tabaka la wanasiasa na wafanya bishara. Tatizo ni kukosekana utiifu kutoka upande wa wakuu wa mikoa ambao wanakasirishwa sasa kwa vile misaada inayotolewa na serekali kuu huko Mosko inapunguwa. Kwa vile mapato ya mafuta yanapunguwa na kuna nakisi katika bajeti ya serekali, Vladimir Putin inambidi achukuwe hatua za kimabavu, na kuunda kitu kama vile baraza la kijeshi, ikiwa anataka kuyadhibiti makundi yanayopingana. Njia inayowezekana kwa Putin kujikwamua na hali alio nayo sasa ni kurejea katika urais, katika wadhifa kama ule wa kifalme. Anaweza kupigania tena kuwa rais kwa vile katiba inampiga marufuku tu mtu kupigania urais kwa vipindi viwili mfululizo, ikiruhusu mtu arejee kuwa mkuu wa nchi ikiwa atakuwa na kipindi cha kujipumzisha katikati. Lakini kila miezi ikienda, mambo yatakuwa magumu zaidi kwa Putin, kwani rais wa sasa, Medvedev, ana timu yake; huenda sasa atamsikiliza Putin pindi atamwambia ni wakati auwache wadhifa huo wa urais, lakini hakuna hakika kama Medvedev ataifuata amri hiyo.

Kipindi hiki cha mwaka mmoja pia hakijawa rahisi kwa rais Dmitry Medvedev mwenyewe, kwani Warussia bado wanaamini kwamba mamlaka hasa anayo Vladimir Putin. Bado Medvedev anachukuliwa kuwa ni nambari mbili katika ngazi za uongozi, licha ya kwamba kikatiba yeye ndiye mwenye kushika usukani. Uchunguzi wa maoni ya watu unaonesha thukuthi moja yao wanaamini Putin ndiye mwenye kudhibiti madaraka mengi nchini Russia, huku asilimia 12 tu wanaosema kwamba Medvedev ndiye Bosi. Asilimia 48 wanasema watu wawili hao kila mmoja ana madaraka sawa na mwengine. Hatua alizochukuwa Medevedev, mwenye umri wa miaka 43 katika vita vikali vya Russia na Georgia mwezi Agosti mwaka jana, na katika mzozo mwengine wa gesi ya ardhini na Ukraine hapo Januari mwaka huu, ziliyavunja yale matumaini kwamba kiongouzi huyo kijana ataleta mabadiliko ya kweli hivi karibuni katika nchi yake. Na pale mwezi Novemba mwaka jana Medevedev alipotangaza kwamba anapendelea kipindi cha urais kirefushwe kutoka miaka minne hadi sita, hatua hiyo ilitafsiriwa sana kama ujanja wa kutaka kumfungulia Putin njia baadae arejee kuwa rais wa nchi.
 • Tarehe 06.05.2009
 • Mwandishi Miraji Othman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Hku8
 • Tarehe 06.05.2009
 • Mwandishi Miraji Othman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Hku8
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com