1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Russia: Medvedev/ Simazi kwa wahanga wa Stalin

Othman, Miraji24 Septemba 2008

Simanzi kwa wahanga wa Stalin huko Russia

https://p.dw.com/p/FOFy
mtawala wa zamani wa kidikteta wa iliokuwa Urussi ya zamani, Josef Stalin

Rais Dmitry Medvedev wa Russia leo aliweka shada la mauwa katika makumbusho ya watu waliokufa kwenye makambi ya mateso ya nchi hiyo, kitendo ambacho wanaharakati wa kupigania haki za kiraia wanasema huenda kikaanzisha utayarifu mpya wa kukabiliana na vitendo viovu vilivotendwa nchini humo katika miaka ya zamani. Mamia ya watu walikufa katika makambi ya mateso yalioanzishwa na mdikteta wa Russia, Josef Stalin, lakini jambo hilo halipewi umuhimu mkubwa siku hizi, na uchunguzi wa maoni unaonesha Warussia wengi wanamheshimu Josef Stalin kwa kuifanya nchi yao kuwa yenye nguvu.

Rais Medvedev, akizuru sehemu za Russia zilioko katika mwambao wa Bahari ya Pasifik, aliyaelezea makambi hayo ya mateso kuwa ni ukurasa wa kusikitisha katika historia ya nchi yake. Alikwenda katika jengo la makumbusho ambapo ni mahala wafungwa walipandishwa katika matishali ili kusafiri katika Mto Kolyma hadi kuwasili kwenye makambi ya kazi ngumu, safari ambayo wafungwa hao waliita Barabara ya mifupa. Aliweka mashada ya mauwa mekundu katika nyumba iliojengwa mwaka 1996 inayotoa sura ya uso uliochongwa kutoka kwenye mwamba na ambao unalia, ukiwa katika mfumo wa mafufu ya vichwa vya binadamu.

Ziara hiyo ya Rais Medvedev ni muhimu kwani mtangulizi wake, Vladimir Putin, aliyekuwa shushushu wa Shirika la Ujasusi la Urussi ya zamani, KGB, na ambaye alikuelezea kusambaratika Urussi kama maafa makubwa ya kisiasa, alijiepusha kuyatembelea makumbusho hayo alipolizuru eneo hilo miaka mitatu iliopita. Rais Medvedev alikumbusha kwamba wafungwa katika kambi hizo walipangiwa kufanya kazi katika migodi ya dhahabu na kujenga barabara. Alisema uchumi unaoonekana katika sehemu hiyo ulijengwa kutokana na damu na jasho la mamilioni ya wananchi.

Kinyume na mtangulizi wake, Rais Medvedev anatilia mkazo juu ya uwazi, uhuru na kuheshimiwa haki za kiraia. Hatua hiyo ya rais huyo mpya wa Russia inaangaliwa na baadhi ya watu kuwa itatoa ishara kali kwa wakuu wa kimkoa na wa serekali kuu kwamba walitilie maanani zaidi suala hili ili kuitekeleza ajenda ya kuzin'goa fikra za Stalin

Wanahistoria wanakadiria kwamba hadi watu milioni milioni 13 waliuliwa au kupelekwa kwenye kambi za kazi ngumu katika Urussi ya zamani baina ya mwaka 1921 na 1953, mwaka ambao Stalin laikufa.

Pale Urussi iliposambaratika, Warussia walionesha hamu ya kuutafuta ukweli juu ya kipindi hicho, lakini jambo hilo kwa haraka likagubikwa na wasiwasi wa kila siku juu ya michafuko ya kisiasa na uchumi mbovu. Katika miaka ya karibuni, watu wameanza tena kuukumbuka utawala wa Stalin,watu wengi wakitilia mkazo juu ya namna alivosimamia ushindi dhidi ya Ujerumani ya Wanazi na mchango wake wa kuibadilisha Urussi kuwa dola kuu duniani. Kuna baadhi ya wabunge wa Russia ambao mwezi huu walipendekeza kuurejesha mnara ya sura ya Felix Dzerzhinsky, muasisi wa kikosi cha siri cha polisi wa Urussi, katika mahala pake pa zamani, nje ya makao makuu ya Idara ya Ujasusi ya Russia, katikati ya mji wa Mosko.