1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rushwa ishughulikiwe kwa uwazi Uturuki

28 Desemba 2013

Umoja wa Ulaya umeitaka Uturuki kushughulikia kashfa ya rushwa inayozidi kukuwa kwa njia ya uwazi kutokana na wasi wasi kwamba serikali inajaribu kuzima uchunguzi wa watu walio karibu na Waziri Mkuu Recep Tayyip Erdogan.

https://p.dw.com/p/1Ai0R
Muadamanaji alieavalia kifuniko cha kujikinga na gesi katika maandamano ya Istanbul.(27.12.2013).
Muadamanaji alieavalia kifuniko cha kujikinga na gesi katika maandamano ya Istanbul.(27.12.2013).Picha: picture-alliance/dpa

Maafisa wa Umoja wa Ulaya wameitaka Uturuki kushughulikia kashfa ya rushwa inayozidi kukuwa kwa njia ya uwazi kutokana na kuwepo kwa wasi wasi kwamba serikali inajaribu kuzima uchunguzi ambao umewalenga watu walio karibu na Waziri Mkuu Recep Tayyip Erdogan.

Erdogan wiki hii alilibadilisha baraza la mawaziri na kuwatimuwa mawaziri muhimu baada ya watu 24 wakiwemo watoto wa kiume wa mawaziri wawili wa zamani kukamatwa kwa madai ya rushwa.

Lakini kiongozi huyo wa Uturuki pia amedai kwamba serikali yake ni muhanga wa njama ya kigeni na ya ndani ya nchi kuiyumbisha Uturuki na amechukuwa hatua ambazo wapinzani wanasema zinakusudia kukwamisha uchunguzi, ikiwa ni pamoja na kuondolewa kwa maafisa wa polisi kwenye nyadhifa zao. Erdogan pia amebadili taratibu za polisi kuhakikisha kwamba uchunguzi wa masuala ya rushwa unapitia kwa viongozi wa juu wa polisi na mahakama walio karibu na serikali lakini mahakama kuu ya Uturuki imeutanguwa uamuzi huo.

Serikali yatakiwa kujiuzulu

Watu wanaokadiriwa kufikia 4,000 walikusanyika katikati ya mji mkuu Ankara Jumamosi kwa maandamano yaliyoandaliwa na chama cha watumishi wa serikali kuitaka serikali ijiuzulu kutokana na kashfa hiyo.

Maandamano dhidi ya rushwa Istanbul.(27.12.2013)
Maandamano dhidi ya rushwa Istanbul.(27.12.2013)Picha: Reuters

Hapo Ijumaa polisi wa kutuliza fujo ilitumia gesi ya kutowa machozi,mabomba ya maji na risasi za mpira kuwatawanya mamia ya waandamanaji waliokuwa wakijaribu kuingia kwenye uwanja wa Taksim mjini Istanbul wakati baadhi ya waandamanaji waliwarushia mawe na fataki polisi.

Hapo Jumamosi mwandishi mashuhuri wa tahariri ameandika baruwa ya wazi kwa Erdogan akimuonya kukomesha mfarakano wake na vyombo vya sheria ambapo amewatimuwa maafisa kadhaa wa polisi waliokuwa wameshughulikia uchunguzi huo wa rushwa.

Ahmet Hakan ameandika katika baruwa ya wazi kwenye gazeti la kila siku la Hurriyet " Mzozo huu sio tu utakuangamiza wewe ......Utatuangamiza sote." Ameandika "Huwezi kunusurika mzozo huu kwa kukaidi vyombo vya sheria,kuwakaidi waendesha mashtaka,kukaidi mahakama."Katika baruwa hiyo pia amemuomba aachane na mawazo ya kukataa kuwakabidhi watu walio karibu kwake kwa mkono wa sheria.

Waziri Mkuu wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan katika mkutano wa hadhara wa wafuasi wake mjini Sakarya. (27.12.2013).
Waziri Mkuu wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan katika mkutano wa hadhara wa wafuasi wake mjini Sakarya. (27.12.2013).Picha: picture-alliance/landov

Murat Belge mwandishi makala mashuhuri naye amelaani kile alichokiita kuwa "mazingira hatari ya kisiasa" yaliyoanzishwa kutokana na hatua iliyochukuliwa na Erdogan kukabiliana na mzozo huo.

Amesema "hali ya kisiasa iliyoanzishwa na waziri mkuu baada ya kuibuka kwa madai hayo ni ya hatari zaidi kuliko hata rushwa yeyewe binafsi."

Rushwa ishughulikiwe kwa uwazi

Kamishna anayeshughulikia Kutanuka kwa Umoja wa Ulaya Stefan Fuele ameelezea wasi wasi wake kuhusiana na kashfa hiyo na kusema kwamba "inapaswa kushughulikiwa kwa njia ya uwazi bila ya upendeleo."

Stefan Fuele Kamishna wa Utanuzi wa Umoja wa Ulaya.
Stefan Fuele Kamishna wa Utanuzi wa Umoja wa Ulaya.Picha: Reuters

Amekaribisha uamuzi wa mahakama kuu ya Uturuki wenye kuzuwiya taratibu mpya za polisi na kusema kwamba uamuzi wa serikali unadhoofisha uhuru wa mahakama na uwezo wake wa kupitisha maamuzi.

Fuele ameitaka Uturuki kuchukuwa hatua zote zifaazo kuhakikisha makosa ya yanashughulikiwa bila ya ubaguzi na bila ya upendeleo katika njia ilio wazi isiokuwa na upendeleo.

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank Steinmeir amekaririwa akiliambia gazeti la Jumapili la Ujerumani " Bild Am Sonntag " kwamba mataifa yanapaswa kusafisha madai ya rushwa bila ya kujali mhusika ni nani.

Ameongeza kusema katika Mashariki ya Kati ambayo imetingwa na migogoro na mizozo kunahitajika kuwepo kwa Uturuki kama nanga madhubuti ikiwa imara ndani na nje ya nchi.

Wachambuzi wa kisiasa wanauhusisha uchunguzi huo wa ngazi ya juu na mvutano unaozidi kutokota kati ya serikali ya Erdogan na wafuasi wa mwanachuoni mashuhuri wa dini ya Kiislamu Fethullah Gulen ambaye anaishi uhamishoni nchini Marekani.

Kile kinachojulikana kama vuguvugu la Gulen linawajumuisha wanasheria mashuhuri wa mahakama na polisi.

Mwandishi : Mohamed Dahman AP/AFP/

Mhariri: Bruce Amani