Rusesabagina ashtakiwa kwa ugaidi Rwanda | Matukio ya Afrika | DW | 14.09.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Rusesabagina ashtakiwa kwa ugaidi Rwanda

Kwa mara ya kwanza tangu kukamatwa kwake mmoja wa wapinzani wakuu wa serikali ya Rwanda Paul Rusesabagina amefikishwa kizimbani mjini Kigali nchini Rwanda akikabiliwa na mashitaka ya ugaidi.

Paul Rusesabagina alipata umaarufu mkubwa kupitia filamu maarufu kama Hotel Rwanda. Anashutumiwa kuendesha mauaji ya raia wasio na hatia kupitia mashambulizi ya kundi la wapiganaji wa FLN kusini magharibi mwa Rwanda miaka miwili iliyopita.

Paul Rusesabagina amefikishwa mbele ya hakimu wa mahakama ya mwanzo ya wilaya ya Kicukiro mjini Kigali kujitetea dhidi ya kusikilizwa kesi yake akiwa nje au akiwa rumande. Lakini baada ya kufikishwa kizimbani kutwa nzima ya leo ilikuwa kuhusu ikiwa mahakama hiyo ina mamlaka kwa mujibu wa sheria kusikiliza kesi yake au la. Mawakili wake walionyesha vipingamizi vya aina tatu huku wakishikilia kwamba mahakama hii haina mamlaka ya kuendesha kesi yake. Soma pia: Mawakili wahofia huenda Paul Rusesabagina akateswa Rwanda

Mawakili wake pia wamesema kwamba kesi yake ilipaswa kusikilizwa ktk wilaya jirani ya Gasabo kwa sababu ndipo mtuhumiwa ana makazi. Jambo jingine mawakili wamesema kwamba mashtaka yanayomkabili aliyatenda akiwa nchini Ubelgiji na kwamba kwa kiasi kikubwa ilikuwa ni mikutano ya hadhara ambayo aliifanya na kwamba alikuwa na uhuru na haki ya kuifanya mikutano hiyo.

Bildergalerie Genozid in Ruanda Evakuierung Mille Collines Hotel

Wakimbizi Watutsi wakihamishwa hoteli ya Mille Collines 1994

Kuhusu uraia wa mshukiwa upande wa mashtaka umesema kwamba, Paul Rusesabagina hakuwahi kupoteza uraia wa Rwanda kwa mujibu wa sheria na kwamba kisheria anachukuliwa kama raia wa Rwanda licha ya kuwa na uraia wa nchi nyingine.

Mshukiwa huyu ni maarufu kwa sababu alijulikana sana kupitia filamu aliyoicheza mwaka 2004 kuhusu kuwaokoa watu zaidi ya 1200 katika mauaji ya kimbari dhidi ya watutsi mwaka 94, filamu ambayo licha ya kutambuliwa na Rais wa zamani wa Marekani George W. Bush kumpa tuzo ya ushujaa, manusura wa mauaji hayo walishikilia filamu hiyo likuwa ni uzushi mtupu. Soma pia: Rais Kagame ajitokeza na kukomesha uvumi kuhusu kifo chake

Lakini wiki iliyopita akizungumza na televisheni ya taifa Rais Paul Kagame alisema mtu huyu hapaswi kufuatiliwa kuhusu uongo uliopo kwenye filamu hiyo isipokuwa vitendo vya kuhatarisha usalama wa taifa kupitia kundi lake la wapiganaji wa FLN kwenye wilaya za Nyamagabe na Nyaruguru karibu na mpaka wa Rwanda na Burundi. "Mnatambua kundi la FLN na MRCD mnatambau vitendo vyao,huyu anatambulika kama kiongozi wao na mara kadhaa amejigamba mashambulizi yao, na mtambau pia watu wanaouawa maeneo ya Nyaruguru, Nyamagabe na mahali pengine, hapa kuna hoja shutuma anayotakiwa kujibu."

Paul Rusesabagina ni raia wa Rwanda aliyekuwa na uraia wa Ubelgiji huku pia akiwa na hati rasmi inayompa haki ya kuishi nchini Marekani. Alionyeshwa mbele ya vyombo vya habari mnamo tarehe 31 mwezi uliopita mjini Kigali baada ya kukamatwa ktk nchi ambayo mpaka leo haijajulikana.

Sylvanus Karemera, DW Kigali