1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rubani wa ndege ya Ethiopia alifuata maelekezo: Ripoti

Daniel Gakuba
4 Aprili 2019

Ethiopia imetoa ripoti ya mwanzo kuhusu ajali ya ndege ya shirika lake la ndege iliyotokea Machi 10 na kuwauwa watu wote 157 waliokuwemo. Ripoti hiyo inasema rubani wa ndege hiyo alifuata maelekezo yote ya Boeing.

https://p.dw.com/p/3GFRu
Äthiopien Transportministerin Dagmawit Moges
Waziri wa usafirishaji wa Ethiopia, Dagmawit MogesPicha: picture-alliance/AA/M. Wondimu Hailu

Ripoti hiyo iliyotolewa leo na serikali ya Ethiopia imetokana na uchunguzi wa taarifa zilizopatikana katika kifaa cha kurekodi data za safari za ndege ya Boeing Chapa 737 Max 8. Waziri wa usafirishaji wa nchi hiyo Dagmawit Moges amesema mbele ya mkutano wa waandishi wa habari mjini Addis Ababa, kwamba marubani walifanya kila kitu kulingana na maelekezo ya watengezaji, lakini hawakufanikiwa kuidhibiti ndege hiyo. Ripoti kamili ya uchunguzi uliofanywa inatarajiwa kuchapishwa kesho Ijumaa.

Ndege ya Boeing 737 Max 8 inaongoza miongoni mwa ndege za Boeing zilizouzwa sana, imekuwa ikikumbwa na mashaka makubwa baada ya ajali hiyo ya ndege ya Ethiopia, ambayo ilitokea miezi mitano tu baada ya ajali ya ndege nyingine kama hiyo iliyomilikiwa na shirika la Lion Air la nchini Indonesia, katika mazingira yanayofanana.

Ndege ilikidhi vigezo vyote vya kiufundi na kitaalamu

Äthiopien Flugzeugabsturz Ethiopian Airlines Flight ET 302
Mabaki ya ndege ya Ethiopia chapa Boeing 737 Max 8 iliyoanguka Machi 10Picha: Reuters/T. Negeri

Waziri Dagmawit amesema uchunguzi huu wa mwanzo umethibitisha kwamba ndege iliyoanguka ilikuwa imetimiza vigezo vyote vya kitaalamu na vya kiufundi kwa ajili ya safari, na ilikuwa imepaa katika hali ya kawaida kabisa, na wakati wote marubani walifuata maelekezo kwa njia sahihi. Waziri huyo amesema kwa msingi wa matokeo ya uchunguzi uliofanywa, wanayo mapendekezo mawili muhimu ya kiusalama.

''La kwanza; kwa vile uchunguzi huu umeonyesha kwamba ndege hii ilikuwa na hali ya kujishusha yenyewe kichwa chini mara kadhaa, mtengenezaji wake anashauriwa kuutazama upya mfumo wa kuendeshea ndege hiyo, na uwezekano wa kuidhibiti. La pili, mashirika ya ndege yanashauriwa kuhakikisha kwanza kwamba mfumo huo umerekebishwa na mtengenezaji, kabla ya kuzirejesha tena ndege katika ratiba ya safari.'' Amesema waziri huyo.

Hakuna aliyelaumiwa

Boeing 737 MAX 8
Boeing 737 Max 8 imesimamishwa hadi uchunguzi utakapokamilikaPicha: Getty Images/AFP/J. Redmond

Katika ripoti hiyo wachunguzi wa Ethiopia hawakuulamu upande wowote kwa ajali iliyotokea, kwa kuheshimu kanuni za kimataifa za uchunguzi wa kiraia, ambazo zinahimiza kujikita tu katika mapendekezo ya kiufundi kuhusu usalama wa ndege. Vile vile hawakutoa maelezo ya kina kuhusu safari ya ndege hiyo iliyoanguka, ambayo yumkini yakachukua miezi kadhaa kukamilika.

Familia za wahanga wa ajali za ndege za Shirika la ndege la Ethiopia na ya Lionair ya Indonesia, waratibu wa safari na pia wasafiri wamekuwa na shauku ya kuona ishara zinazounganisha ajali hizo, na mchango wa kiufundi upande wa Boeing, na wa kiuendeshaji upande wa Ethiopia, katika ajali hiyo mbaya. Kampuni ya Boeing imesema itaipitia kwanza ripoti hiyo iliyotolewa, kabla ya kutangaza chochote.

ape, rtre