1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

RPF Yaongoza uchaguzi wa bunge Rwanda

Saumu Mwasimba
5 Septemba 2018

Sio matokeo ya kushangaza kwa RPF ingawa kwa chama cha kijani kimejiwekea historia ya kuingia bungeni kwa mara ya kwanza baada ya kufanikiwa kunyakua viti viwili kwa kushinda asilimia 5 ya kura

https://p.dw.com/p/34KOa
Ruanda Wahlen
Picha: Picture alliance/Zumapress/G. Dusabe

Chama tawala nchini Rwanda kinachoongozwa na rais Paul Kagame kinatarajiwa kushinda kwa kishindo uchaguzi wa bunge uliofanyika kwa siku tatu.Matokeo ya awali yanaonesha  chama hicho kinajiandaa kushinda thuluthi tatu ya viti vya bunge.Pamoja na  matokeo hayo  chama cha upinzani Green Party kwa mara ya kwanza kimeshinda viti bungeni.

Matokeo rasmi  yanatarajiwa kutangazwa tarehe 16 ya mwezi huu wa Septemba lakini matokeo ya awali yaliyotoka hapo jana Jumanne yanaonesha kwamba chama cha Rais Paul Kagame cha Patriotic Front RPF pamoja na vyama vingine saba vidogo washirika wake wamenyakuwa kwa ujumla asilimia 74 ya kura baada ya uchaguzi wa jumatatu.Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Prof Kalisa Mbanda alitangaza matokeo kama ifuatavyo.

"RPF imepata asilimia 74% ya kura zote zilizopigwa sawa na viti 40 bungeni, chama cha kiliberali kimepata viti 4, chama cha kishoshalist kimepata viti 5 wakati chama cha kijani kikipata viti 2 na huku chama cha kijamaa social part y nacho kimepata nafasi 2. Wagombeaji binafsi wote hakuna aliyefikisha asilimia moja na nataka niseme tu kwamba haya ni matokeo ya muda.

Ruanda Wahlen Wahllokal in Kigali
Picha: TONY KARUMBA/AFP/Getty Images

Matokeo kwa upande wa chama cha RPF yameporomoka kwa kiasi kidogo ikilinganishwa na miaka mitano iliyopita.Vyama vingine vitatu vingavyounga mkono sera ya serikali ya Kagame viligawana viti vingine vingi vilivyobakia.Kwa ujumla vyama nchini humo vilikuwa vikigombea viti 53 vya moja kwa moja vya bunge la viti 80 na  vingine 24 vilivyotengewa wanawake na viwili viko kwa ajili ya vijana na kiti kimoja ni kwa ajili ya walemavu ambavyo voyte kawaida wawakilishi wake huchaguliwa na baraza maalum na kamati za kitaifa.

Licha ya chama cha RPF kuuhodhi uchaguzi huo na kuvisomba viti vingi chama cha kijani kimekuwa chama cha kwanza cha upinzani kuingia bungeni mara hii kwa mujibu wa matokeo kikijipoatia asilimia 5 ya kura na viti viwili.Kiongozi wa chama hicho Frank Habineza ambaye binafsi aliwahi kuwa mwanachama wa chama cha RPF ambaye amegeuka kuwa mpinzani na mkosoaji mkubwa wa sera za rais Kagame amesema ushindi wa chama chake ni dalili kwamba Rwanda inafungua wigo wake wa kisiasa. Na kwa hatua hiyo kwa mtazamo wake wamefikia lengo muhimu katika kupata nafasi bungeni.

Ruanda Präsidentschaftswahlen Frank Habineza
Kiongozi wa Green Party-Frank HabinezaPicha: Reuters/C. Uwiringiyimana

Hata hivyo wananchi wengi wa Rwanda wanauangalia uchaguzi wa bunge kama hatua ya kawaida isiyokuwa na umuhimu mkubwa kwasababu wabunge hawana mamlaka yoyote bungeni. Idadi ya waliojitokeza kupiga kura vituoni katika mji mkuu Kigali haikuwa kubwa ingawa zaidi ya watu milioni 7 walijiandikisha kupiga kura kote nchini huku zaidi ya wagombea 500 kutoka vyama vitano vya kisiasa  na wagombea huru 5 walijitokeza kuwania viti vya bunge hilo.

Mwandishi:Saumu Mwasimba/AFPE

Mhariri Mohammed AbdulRahaman