Ripoti ya utawala bora barani Afrika | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 05.10.2009
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Timu Yetu

Ripoti ya utawala bora barani Afrika

Taarifa ya utafiti uliofanywa na Mfuko wa Mo Ibrahim ambao hutoa ripoti kila mwaka juu ya serikali yenye uwajibikaji na utawala bora barani Afrika, imetoa ripoti yake.

default

Mo Ibrahim Muasisi wa Taasisi ya Mo Ibrahim akizungumzia kuhusu tuzo ya uongozi katika bara la Afrika.

Serikali ya Mauritius kwa ushirikiano na sekta binafsi imeweza kutoa huduma bora yenye manufaa kwa wananchi wake, na hivyo kutajwa kuwa nchi ya kwanza barani Afrika kwa utawala bora.

Kisiwa hicho kilicho katika Bahari ya Hindi kimechukuwa nafasi ya kwanza kutokana na kukidhi vigezo vikuu vinne vilivyozingatiwa katika utafiti huo, kikivibwaga visiwa vingine vilivyoonekana kukidhi vigezo hivyo, ambavyo ni Cape Verde na Seychelles.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo nafasi ya nne imechukuliwa na Botswana wakati nafasi ya tano imechukuliwa na nchi yenye uchumi mkubwa barani Afrika, Afrika Kusini.

Ripoti hiyo ambayo ina miaka mitatu sasa tangu kuanzishwa kwake, na awamu hii ikiwa imehusisha nchi zote 53 za bara la Afrika, mwaka huu imepima viashiria 84, ambavyo vimegawanywa katika ulinzi na usalama, ushiriki na haki za binadamu, fursa thabiti za kiuchumi pamoja na maendeleo ya watu.

Ikiwa imetolewa katika Chuo Kikuu cha Cape Town, imeonesha kuwa nchi za ukanda wa Kusini mwa Afrika zimeibuka bora kwa asilimia 58.1, zikifutaiwa kwa ukaribu na ukanda wa Kaskazini mwa bara hilo ambazo zina asilimia 57.7.

Nchi zilizoripotiwa kufanya vibaya zaidi ni kutoka ukanda wa Afrika ya Kati, ambazo zimeibuka na asilimia 40.2, huku ukanda wa Afrika Magharibi ukikamata nafasi ya tatu kwa asilimia 51.7 wakati nchi za Afrika Mashariki zikiwa katika nafasi ya nne kwa asilimia 46.9.

Nchi saba zinazounda Afrika ya Kati zikiwemo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Equatorial Guinea, zote zipo nje ya nafasi 20 bora, huku Gabon ikiwa katika nafasi ya kipekee, kwa kushindwa kabisa kufikia wastani uliowekwa kwa bara la Afrika.

Nchi yenye machafuko ya kiutawala ya Somalia, ikiwa ni ukanda wa maharamia kuanzishia mashambulizi dhidi ya meli za kigeni, ambapo pia waasi wa kiislamu wameifanya nchi hiyo kushindwa kabisa kuwa na serikali imara, imeibuka na asilimia 15.2.

Somalia imeorodhesha kiwango cha chini kabisa katika bara la Afrika cha 0.9 za fursa za kiuchumi, na asilimia 9.1 za usalama na utawala wa kisheria.

Katika nafasi ya 52 baada tu ya Somalia ipo Chad, ikifuatiwa na Zimbabwe ambayo serikali ya umoja wa kitaifa ya Rais Robert Mugabe na hasimu wake mkubwa Waziri Mkuu Morgan Tsvangirai, inakabiliwa na kibarua kizito cha kuujenga upya uchumi wa nchi hiyo ulioharibika vibaya kutokana na mfumuko wa bei uliovunja rekodi duniani.

Orodha hiyo ya Mo Ibrahim juu ya utendaji wa serikali za kiafrika, iliundwa kuvisaidia vyama vya kiraia kufuatia kwa ukaribu uwajibikaji wa serikali hizo kwa wananchi wake.

Ripoti ya mwaka huu imeandaliwa kwa ushirikiano wa Afrobarometer and the American University cha mjini Cairo.

Mohamed Ibrahim ni mfanyabiashara mashuhuri wa sekta ya mawasiliano, ambaye ni mzaliwa wa Sudan.

Mwandishi: Lazaro Matalange/RTRE

Mhariri: Abdul-Rahman.

Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com