Ripoti ya Umoja wa mataifa kuhusu hali ya hewa inatisha | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 06.04.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Timu Yetu

Ripoti ya Umoja wa mataifa kuhusu hali ya hewa inatisha

bahari itaenea,joto kali litavuruga mzunguko wa damu mwilini na ukame-ni miongoni mwa madhara ya kubadilika hali ya hewa.

Milima ya barafu imeanza kuyayuka

Milima ya barafu imeanza kuyayuka

Halmashauri ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia masuala ya hali ya hewa imechapisha sehemu ya pili ya ripoti yake kuhusu kubadilika hali ya hewa.Yaliyotajwa ndani ya ripoti hiyo yanatisha:Kipeo cha bahari kitapanda kwa namna ambayo watu watalazimika kuhamia maeneo ya ndani ya nchi zao , ukame utaangamiza mazao na joto kali litavuruga mzunguko wa damu ya binaadam.

Muda wamejua kuuchagua,ili watu wagutuke,seuze tena sehemu ya mwanzo ya ripoti hiyo iliyotangazwa mwezi wa February bado haijasahauliwa.Wakati ule wataalam waliwaondolea watu shaka shaka zote walizokuwa nazo kuhusiana na madhara yanayoweza kusababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa:”Madhara ya moshi wa viwandani si hadithi ya kubuni na wakulaumiwa ni sisi binaadam”-ndio kiini cha yale yaliyoandikwa katika ripoti ya mwanzo.

Katika ripoti hii ya pili watafiti wa Umoja wa Mataifa wanazungumzia juu ya madhara jumla ya kuzidi ujoto duniani-matokeo yake ni pamoja na joto kali kupita kiasi,dharuba,misitu kushika moto na ukame.Na wanasisitiza wataalam hao wa Umoja wa Mataifa,hata kama mkondo mpya wa siasa ya kuhifadhi hali ya hewa utasaidia kupunguza madhara hayo-lakini hautazuwia yasitokee.Habari hizo za kutisha zilitangazwa Ijumaa Kuu.

Lakini ujumbe wa ripoti ya hali ya hewa si mpya hivyo.Kipya ni vile jinsi walimwengu walivyotega masikio kutaka kujua kilichomo.Hadi ifikapo mwezi June ujao,viongozi wa mataifa tajiri watakapokutana nchini Ujerumani,itadhihirika kama wanasiasa wako tayari kujifunza kutokana na makosa yaliyofanyika.

La mwanzo kabisa itakua kupunguza moshi unaotoka viwandani.Ujerumani inayoamini inafanya mengi kuhifadhi mazingira-inakumbwa na kizungumkuti:Hata kama nchi hii itaamua kukifunga kama ilivyoahidi kinu chake cha nishati ya kinuklea-kiwango kilichowekwa cha kupunguza moshi wa viwandani hakitaweza kufikiwa.

Ingawa nishati ya kinuklea si njia bora ya kujipatia nishati na kuhifadhi mazingira kwa wakati mmoja,lakini angalao haichafui hali ya hewa.Na panapohusika na suala la takataka za kinuklea,mtu anaweza kusema linaweza kuwekwa kando watu wakitilia maanani umuhimu uliopo katika suala la mabadiliko ya hali ya hewa.

Nishati mbadala inayotokana na jua,upepo na maji ni njia nyengine ya maana inayoweza kutuliza hali ya hewa.Nchini Ujerumani teknolojia hiyo inazidi kupata nguvu miongoni mwa njia za kujipatia nishati.Licha ya hayo lakini mwaka jana moshi uliotoka viwandani nchini Ujerumani unasemekana uliongezeka-hayo yakiwa ni matokeo ya ukuaji wa kiuchumi uliokua ukisubiriwa kwa hamu.

Kwa hivyo kilichosalia ni suala la namna ya kufanikiwa.Juhudi zote za kuepusha madhara yanayotokana na kuchafuliwa hali ya hewa yasiwe makubwa hivyo zitaweza kuleta tija kwa kutia njiani mbinu zinazofaa katika matumizi ya nishati na teknolojia.Badala yake hakuna kutia ila lengo la kufikia ukuachi wa kiuchumi.

Bila ya shaka hakuna anaeweza kuzishawishi China ,India na nchi nyengine zinazoinukia zisizidishe neema nchini mwao. Mjadala kuhusu ukuaji wa kiuchumi katika nchi tajiri kwa viwanda umeonyesha hakuna wakati wowote ambapo mtu atasema “sitaki tena neema”.Anaeamini kwamba ukuaji wa kiuchumi utasalia milele kua neema ya nchi fulani tuu basi mtu huyo ama ameingiwa na kichaa au ni mwanauchumi—kama alivyowahi kusema wakati mmoja Kenneth Boulding-ambae binafsi ni mtaalam wa kiuchumi.

 • Tarehe 06.04.2007
 • Mwandishi Oummilkheir
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CB4r
 • Tarehe 06.04.2007
 • Mwandishi Oummilkheir
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CB4r

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com