1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ripoti ya Shirika la UNCTAD kwa mwaka 2007

20 Julai 2007

Nchi maskini duniani zinatiwa kabari kwa kunyimwa uwezo wa kiteknolojia zinazouhitaji ili kujikwamua na mitego ya umaskini ili kuweza kuzikimbilia nchi nyingine za dunia. Hayo yamesemwa na ripoti iliochapishwa punde na Shirika la Umoja wa Mataifa juu ya Biashara na Maendeleo Duniani, UNCTAD.

https://p.dw.com/p/CHk5

Lakini ripoti hiyo pia imegusia donda ndugu kwa nchi nyingi za Afrika, nalo ni tatizo la kuhama wasomi na mabingwa wa nchi hizo kuja katika nchi zilizoendelea na ambazo tangu hapo hazina uhaba wa watu kama hao.

Kuhama watu wenye ujuzi na maarifa fulani ni njia ya kuzibakisha nchi za Kiafrika katika hali duni ya kiteknolojia, inasema ripoti ya UNCTAD. Nchi hupata hasara kutokana na kuhama kabisa wasomi wake. Ilivokuwa nchi za Kiafrika hazina idadi kubwa ya watu kama hao, basi kuhama kwao, hata kidogo, kunabakisha athari kubwa. Nchi yeyote inayojipatia wasomi wa aina hiyo, hujipatia rasil mali ya bongo, huwa na msingi madhubuti wa kupiga hatua za maendeleo za muda mrefu na pia kutanua biashara yake.

Wasomi na wajuzi wengi kutoka nchi maskini wanahamia katika nchi zilizoendelea, hasa Ulaya na Marekani.

Lakini ikiwa watu wa aina hiyo tangu walipokuwa makwao wanakuwa hawana kazi, basi hasara inazopata nchi zao za kuzaliwa zinakuwa sio kubwa mno, zinafidiwa na hali nyingine , kama vile kutuma fedha nyumbani kwa jamaa zao, na baadae nchi hiyo kufaidika na ujuzi wa wahamiaji hao wanaporejea nyumbani na labda kwa muda kufungua biashara. Pia wanapokuwa ngambo wanakuwa kama kiungo cha kutiririka, maarifa, uwekezaji na teknolojia katika nchi zao za asili. Kutiririka zaidi maarifa hayo pamoja na uwekezaji na biashara kunaweza kuonekana pale panapojengwa viwanda vinavozalisha bidhaa.

Laki ripoti hiyo ya UNCTAD inasema mambo hayo mazuri yanaweza tu kujitokeza pale nchi hizo zitakapokuwa zimefikia kiwango fulani cha maendeleo na uchumi wao kukuwa.

Uhamiaji huo wa kimataifa unatokana na mbinyo wa watu hao kutaka kuzihama nchi zao, na nchi zinazowapokea kuwahitaji sana. Makwao hakuna nafasi za kazi, masharti ya kazi ni mabaya, mustakbali wa kazi sio mzuri, hakuna utulivu wa kisiasa katika nchi zao na mishahara ni midogo, licha ya kutaja lile pengo kubwa baina ya mapato ya wafanya kazi wa nchi maskini na nchi tajiri.

Msikilize Profesa Chacha Nyaigoti Chacha, mwenyekiti wa Baraza la Vyuo Vikuu vya Afrika Mashariki, mjini Nairobi, Kenya:

Nchi za viwanda, licha kuwa na wingi wa wataalamu, lakini bado zina kiwi cha wasomi na wafanya kazi wenye ujuzi. Nchi za viwanda, hasa za Ulaya, Japan, Marekani, Kanada na Australia wafanya kazi wake wengi wanazeeka na uzazi umepungua miongoni mwa vijana wao. Wafanya kazi wa mitambo ya kompyuta na mawasiliano ya habari, yaani IT, wanahitajiwa sana; pia wahandisi, mafundi, mafundi bomba, wauguzi na waalimu.