1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ripoti ya mwaka 2006 juu ya wakimbizi duniani

12 Julai 2007

Kwa mwaka wa pili mfululizo ghasia na mateso nchini Iraq zimechochea ongezeko kubwa la idadi ya wakimbizi duniani.

https://p.dw.com/p/CHB3
wakimbizi wa Iraq waliokimbilia kwenye mpaka na Kuwait
wakimbizi wa Iraq waliokimbilia kwenye mpaka na KuwaitPicha: AP

Hayo ni kwa mujibu wa ripoti mpya juu ya wakimbizi duniani iliyotolewa na kamati inayohusika na masuala ya wakimbizi na wahamiaji ya Marekani (USCRI)

Ripoti hiyo inasema kufikia mwishoni mwa mwaka 2006 kiasi cha watu millioni 14 walikuwa wakimbizi.Idadi hiyo ni kubwa kabisa kuwahi kuonekana duniani tangu mwaka 2001 na imeongezeka kwa kiasi cha watu milioni mbili ikilinganishwa na ile ya mwaka 2005.

Kati ya watu millioni 2 waliokimbia nchi zao katika kipindi cha mwaka takriban nusu yao ni wairaq. Marekani nchi ambayo ilianzisha uvamizi Iraq iliwakubali wakimbizi sio zaidi ya 202 mwaka jana ijapokuwa nchi hiyo imetoa ahadi ya kuwapa makazi mapya wairaq 3000 zaidi kufikia mwishoni mwaka huu.

Kinyume na Marekani,Syria nchi jirani ya Iraq imewapokea takriban wakimbizi laki nne na nusu kutoka Iraq mwaka jana na kuifanya idadi ya wakimbizi kutoka Iraq nchini humo kufikia kiasi cha laki nane,ilhali Jordan nayo imewachukua takriban wakimbizi laki mbili na nusu kutoka Iraq mwaka jana na kuifanya idadi yao nchini humo kufikia sio chini ya laki saba.

Kiasi cha wairaqi laki nane waliingia nchini Misri.

Mwenyekiti wa kamati hiyo ya USCRI Lavinia Limon anasema suala hilo la wakimbizi wa Iraq linatatanisha kama ilivyo vita vyenyewe huko Iraq kwani suala hilo ni zito na halielekei kuwa na mwisho na wala sio rahisi kulitatua.

Aidha bibi Lavinia amesema kwenye ripoti hiyo kwamba suala la wakimbizi wa iraq limepuuzwa na vyombo vya habari,linazungumziwa kwa uchache tu na bunge la Marekani na kupuuzwa kistaarabu na serikali ya rais Gorge Bush,nchi za Ulaya,nchi kubwa za mashariki ya kati na jumuiya ya kimataifa.

Mbali na Iraq ripoti hiyo pia imezungumzia Wakimbizi Palestina,Afghanstan,Somalia ambako opresheni ya wanajeshi wa Ethiopia mwishoni mwa mwaka jana ilisababisha wimbi la wakimbizi katika nchi za Yemen,Kenya na Ethiopia.

Kupamba moto kwa mapigano nchini Sri Lanka kati ya serikali na waasi wakitamil Tiger kumesababisha watu kiasi cha 26 elfu kukimbilia India.Nchini Jamahuri ya Afrika ya Kati vita vya mpakani vinavyosambaratisha taifa hilo,Chad na Sudan vimetimua maelfu ya watu kwenye makaazi yao.

Kati ya wakimbizi wote millioni 14 kote duniani pamoja na wanaomba hifadhi ni chini ya 70 elfu walioweza kupata makao rasmi katika mwaka 2006.

Marekani imewapokea wakimbizi 41 elfu kotoka nchi mbali mbali ikifuatiwa na Australia iliyochukua wakimbizi 12,133,Canada 10,600,Sweden imepokea watu 1,555 na Norway imepokea wakimbizi 924.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ambayo katika kipindi cha miaka kadhaa imekuwa ikiziangalia nchi ikiwa zinazingatia haki za binadamu chini ya mkataba wa mwaka 1951 unaohusu hali ya wakimbizi imebainisha kuzorota kwa hali jumla ya haki za binadamu kwa wakimbizi katika mataifa mengi mwaka 2006.