1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Richard Holbrooke aaga dunia

14 Desemba 2010

Kwa miaka 50 Holbrooke ambaye alikuwa na umri wa miaka 69, alitumika kama mjumbe na alianza kufanya kazi katika wizara ya nje, huko Vietnam.

https://p.dw.com/p/QXXm
Richard Holbrooke, amefariki.Picha: AP

Mjumbe wa Marekani nchini Afghanistan na Pakistan Richard Holbrooke, ameaga dunia. Holbrooke alifariki usiku wa kuamkia leo baada ya kufanyiwa upasuaji, kurekebisha mpasuko katika mshipa mkubwa wa damu wa upande wa kushoto wa moyo. Holbrooke alianguka na kupoteza fahamu alipokuwa katika afisi ya Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Hillary Clinton siku ya Ijumaa. Holbrooke ambaye alilazwa katika hospitali ya George Washington alifanyiwa upasuaji uliochukua muda wa saa 20. Mapema jana Bi Clinton alisema mjumbe huyo alikuwa katika hali mbaya. Kifo cha Holbrooke kinatokea wakati rais Barack Obama anajitayarisha kuzindua awamu ya pili ya mkakati wa vita nchini Afghanistan. Holbrooke ambaye pia alihudumu kama balozi wa zamani hapa Ujerumani, anafahamika zaidi kwa mchango wake katika kupatikana ule mkataba wa amani wa Dayton mwaka 1995 uliomaliza vita vya miaka mitatu huko Bosnia. Katika risala yake Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Hillary Clinton amesema Marekani imempoteza mtu shujaa na shupavu.