Rice aelekea mashariki ya kati, baada ya Israel kuihujumu Gaza. | Matukio ya Kisiasa | DW | 03.03.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Rice aelekea mashariki ya kati, baada ya Israel kuihujumu Gaza.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Condoleezza Rice, anaondoka kuelekea mashariki ya kati leo, huku machafuko baiana ya Israel na wanaharakati wa Hamas yanautia hatarini utaratibu wa amani katika eneo hilo

default

Baadhi ya majengo yalioharibiwa katika juhuma za kijeshi za Israel.

Ziara ya Waziri huyo wa mambo ya nchi za nje wa Marekani katika mashariki ya kati inakuja katika wakati ambao Wapalestiana wametangaza kusitisha mazungumzo na Israel baada ya hujuma kubwa za kijeshi za Israel katika eneo la Gaza.

Ikulu ya Marekani imezitaka pande zote mbili kumaliza machafuko na matumizi ya nguvu, kutatoa nafasi ya kuanza kwa mazungumzo ya amani ya mashariki ya kati.

Lakini mapema leo asubuhi msemaji wa jeshi la Israel alisema harakati kubwa za kijeshi huko Gaza taratibu zinaanza kumalizika na redio ya nchi hiyo ilisisitiza kwamba harakati hizo sasa zimemalizika kabisa.

Kwa mujibu wa ripoti tangu Jumatano wapalestina 116 waliuwawa wakiwemo watoto 22 na Israel ilipoteza wanajeshi 2 na raia mmoja.

Waziri wa ulinzi wa Israel Ehud Barak amelilaumu kundi la Hamas kuwa chanzo kutokana na hujuma za maroketi ndani ya Israel na akitetea hatua ya serikali ya Israel na kusema,"Tunatarajia alau ukanda wa Gaza ambao sasa uko mikononi mwa wapalestina wa Hamas utakua shwari, lakini imegeuka vyenginevyo. Hauwezi kukaa tu na wala siamini kuna nchi yoyote huru duniani angeruhusu hujuma za aina hiyo dhidi ya raia wake."

Wakati Israel ikisitisha harakati zake za kijeshi, chama cha Hamas kinasema hatua hiyo inadhihirisha kushindwa kwa wanajeshi wa Israel mbele ya wapiganaji wake wa kikosi cha Ezzadine Al-Qassam.

Kwa wakati huu kuna dalili ndogo ya maendeleo katika mazungumzo ya amani ya mashariki ya kati na matumaini ya hapo awali ya kuundwa dola ya Palestina kandoni mwa Israel ifikapo 2008 yameanza kufifia. Hata waziri mkuu wa Israel Ehud Olmert anaelekea kuwa na shaka shaka kama makubaliano yataweza kufikiwa ifikapo 2008.

Msemaji wa Rais wa mamlaka ya utawala wa wapalestina Abu Rudeina amesema kwamba hatua zinazochukuliwa na Israel ukiwemo mradi wa makaazi mapya zinahujumu wajibu wake wa kuwa na mazungumzo thabiti na hivyo kuyavuruga mapatano yaliopatikana katika mkutano wa Annapolis.

Wito unazidi kutolewa kuitaka Marekani ijihusishe zaidi katika mwenendo wa amani na akatika hotuba yakle ijumaa iliopita katika chuo kikuu cha Princeton, Mfalme Abdullah II, wa Jordan alisema hatua hiyo itasaidia kujenga daraja la kufikiwa makubaliano ya mwisho ifikapo 2008.

Hadi sasa waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Rice, anasita sita kuchukua mamlaka ya kusimamia mazungumzo kati ya Israel na Wapalestina akipendelea zaidi kuwaachia wahusika, akisisitiza wapatanishi wa Marekani waliotangulia wameshindwa. Lakini wanaomkosoa wanahoji kwamba shinikizo linahitajika na pande hizo haziwezi kuachwa peke yao kufikia suluhisho, Ni jambo lisilowezekana.

Bibi Rice anatarajiwa mjini Cairo kesho kwa mazungumzo na viongozi wa Misri juu ya hali ya mambo kabla ya kuelekea Ramadhallah kukutana na viongozi wa kipalestina na baadae Jerusalem kuzungumza na wenzao wa Israel. Baadae ataelekea Brussels kuhudhuria mkutano wa mawaziri wa Jumuiya ya kujihami ya magharibi NATO ambao inasemekana utazingatia zaidi masuala ya Afghanistan na Kosovo.








 • Tarehe 03.03.2008
 • Mwandishi Abdulrahman, Mohamed
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/DGtB
 • Tarehe 03.03.2008
 • Mwandishi Abdulrahman, Mohamed
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/DGtB
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com