1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Reus arejea mazoezini Dortmund

Bruce Amani
9 Januari 2023

Nahodha wao Marco Reus amesema amepona jeraha la kifundo cha mguu na analenga kucheza tena wakati timu hiyo itashuka dimbani Januari 22 dhidi ya Augsburg. Dortmund imeweka kambi Marbella Uhispania

https://p.dw.com/p/4LuZJ
Borussia Dortmund vs. FC Copenhagen | UEFA Champions League
Picha: Alex Grimm/Getty Images

Reus mwenye umri wa miaka 33 amecheza mara mbili pekee katika Bundesliga tangu katikati ya Septemba na ilibidi amwambie kocha wa timu ya taifa ya Ujerumani Hansi Flick kuwa asingeweza kucheza katika Kombe la Dunia nchini Qatar. Lakini sasa yuko fiti na anafanya mazoezi kamili katika kambi ya timu yake mjini Marbella, Uhispania.

Reus amesema morali ya timu pia imepigwa jeki na kurejea kwa mshambuliaji Sebastian Haller baada ya kufanyiwa upasuaji mara mbili na matibabu ya saratani ya tezidume kabla ya kuanza msimu.

Wakati Dortmund wamekita kambi Uhispania, mahasimu wao Bayern Munich wako mashariki ya Kati ambapo Afisa Mkuu mtendaji Oliver Kahn amesema ana uhakika timu hiyo itafikia malengo yao msimu huu hata bila ya wachezaji kadhaa muhimu waliojeruhiwa, akiwemo nahodha Manuel Neuer.

Mabingwa hao wa Ujerumani, wanaowinda taji lao la 11 mfululizo, wanajiandaa kuangushana na RB Leipzig Januari 20 kwa kuweka kambi ya mazoezi mjini Doha, Qatar. Neuer alivunjika mguu baada ya Kombe la Dunia na atakuwa nje kwa kipindi kilichobaki cha msimu.

AFP, Reuters