Republican wavutana kumuunga mkono Trump | Matukio ya Kisiasa | DW | 06.05.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Republican wavutana kumuunga mkono Trump

Spika wa baraza la wawakilishi la Bunge la Marekani Paul Ryan amekataa kumuunga mkono Donald Trump akisema kuwa mfanyabiashara huyo anayo kazi ya ziada ya kukiunganisha chama cha Republican.

Spika wa baraza la wawakilishi la Bunge la Marekani Paul Ryan

Spika wa baraza la wawakilishi la Bunge la Marekani Paul Ryan

Spika wa baraza la wawakilishi la Bunge la Marekani Paul Ryan amekataa kumuunga mkono Donald Trump kama mgombea wa kiti cha urais wa chama cha Republican akisema kuwa mfanyabiashara huyo anayo kazi ya ziada ya kukiunganisha chama hicho.

Ryan amesema hayuko tayari kwa sasa kumuunga mkono bali kinachotakiwa ni kuleta mshikamano katika chama. Trump amejibu kauli ya Spika huyo kwamba hata yeye hayuko tayari kuuunga mkono ajenda za Spika huyo. "Labda katika siku za usoni tunaweza kufanya kazi pamoja na kufikia makubaliano ya kitu gani ni bora kwa Wamarekani" alisema Trump. Akiongeza kuwa raia wa Marekani wamewekwa kando kwa muda mrefu na kwamba ni muda sasa kwa wanasiaa kuwafikiria kwanza.

Hata katika mchakato wa uchaguzi ndani ya chama hicho cha Republican ambao umeonyesha mgawanyiko , uamuzi wa Ryan wa kutomuunga mkono Trump umeoneka kuwa wa ajabu kwa kiongozi wa juu.

Mgomba anayeongoza Republican Donald Trump

Mgomba anayeongoza Republican Donald Trump

Ryan amekuwa kimya tangu Trump afanye vyema katika jimbo la Indiana hapo siku ya jumanne ambapo iliwalazimu wapinzani wake waliokuwa wamesalia kubwaga manyanga. Viongozi wengine wa Republican akiwemo Seneta Mitch McConnel wameonyesha kumuunga mkono kwa shingo upande mgombea huyo , hali ambayo inaonekana inaweza kufanywa na Ryan mwishoni ." Tutahitaji kuwa na bendera itakayowaunganisha wanarepublican wote, wahafidhina , na matawi yote ya chama chetu ili tuwe na ajenda moja" amesema Ryan , akiongeza kuwa mgombea wao anapaswa kuongoza jitihada hizo.

Mwenyekiti wa kamati ya taifa ya chama hicho Reince Priebus ambaye yupo karibu na Spika Ryan amesema amezungumza na wote wawili juu ya kumaliza tofauti zao na kwamba watakutana wiki ijayo kwa mazungumzo. Mvutano baina ya mgombea ambaye anaonekana ndiye mwakilishi wa chama hicho katika kuingia Ikulu na Spika wa Baraza unakuja wakati ambapo wanachama wote wanapaswa kuacha vita ya uteuzi na kuunganisha nguvu ya chama katika uchaguzi wa mwezi Novemba.

Mgombea Hillary Clinton wa Democratic

Mgombea Hillary Clinton wa Democratic

Hata hivyo Ryan ameweka wazi kuwa hamuungi mkono Clinton jambo linaloonyesha dhahiri kuwa mwishoni atakuwa upande wa Trump.Amekiri wazi kuwa ushindi wa mgombea huyo dhidi ya wanasiasa waliokuwa na uzoefu unaonyesha kuwa kigogo huyo aliingia katika kitu kilichokuwa na nguvu. Ryan aliyekuwa mteule wa nafasi ya umakamu wa rais kwa mwaka 2012 alikuwa anaonekana kama mbadala wa Trump, hata hivyo alijitoa mwezi uliopita. Trump sasa anacho kibarua cha kushawishi kura ya wajumbe 1237 watakaoamua iwapo awe mgombea katika uchaguzi wa chama hicho hapo Julai mjini Cleveland.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi

Mhariri: Yusuf Saumu

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com