Real Madrid yatimiza ndoto ya ″La Decima″ | Michezo | DW | 25.05.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Real Madrid yatimiza ndoto ya "La Decima"

Real Madrid ilifufuka kutoka kwa wafu na kuandika sura mpya katika historia yake wakati ilipoizaba Atletico Madrid magoli 4-1 katika muda wa ziada. Matokeo ya mwisho hata hivyo siyo taswira ya namna mechi ilivyokuwa

Mchango wa magoli kutoka kwa Gareth Bale, Marcelo na Cristiano Ronaldo uliwapa ulitimiza ndoto ya Real ya kunyakua kombe la kumi la Ulaya maarufu kama La Decima katika fainali iliyochezwa uwanja wa Estadio da Luz mjini Lisbon.

Wakati Atletico wakionekana kuwa na nafasi kubwa ya kushinda kombe hilo kwa mara ya kwanza baada ya kuwa kifua mbele kupitia goli lililofungwa kwa njia ya kichwa naye Diego Godin katika kipindi cha kwanza, Real ilisawazisha baada ya kufanya shambulizi baada ya jingine, wakati Sergio Ramos alipotikisa wavu kwa njia ya kichwa katika dakika ya tatu ya dakika za nyongeza.

UEFA Champions League-Finale Real Madrid vs. Atletico de Madrid

Atletico Madrid walionekana kulitwaa kombe hilo kupitia goli la Diego Godin katika kipindi cha kwanza

Hivyo fainali hiyo ikalazimika kuingia katika muda wa ziada na huku Atletico walioonekana kuishiwa pumzi wakisalimu amri, Real walitawala na kufunga magoli matatu katika dakika kumi za kuumaliza mchezo.

Gareth Bale aliyenunuliwa kwa kitita kikubwa cha pesa alifunga kwa njia ya kichwa baada ya dakika 110, Marcelo akafanya mambo kuwa 3-1 baada ya kuingia katika kijisanduku dakika nane baadaye kabla ya Ronaldo, nahodha wa Ureno akicheza katika mji wa nyumbani, kufunga penalty katika dakika ya mwisho, baada ya kuchezewa visivyo kwenye kijisanduku.

Goli hilo lilikuwa lake la 17 katika msimu mmoja wa Champions League, ambayo ni rekodi na kwa hivyo CR7 anaingia katika madaftari ya kumbukumbu kama mchezaji wa kwanza katika historia ya dimba hilo ya miaka 59 kuwahi kuzifungia timu mbili zilizotwaa kombe hilo katika fainali. Aliifungia Manchester United wakati waliposhinda taji hilo mwaka wa 2008.

Goli la kusawazisha lake Sergio Ramos liliivunja mioyo ya wapenzi wa Atletico Madrid

Goli la kusawazisha lake Sergio Ramos liliivunja mioyo ya wapenzi wa Atletico Madrid

Ushindi huo pia ulimaanisha kuwa Carlo Ancelotti amekuwa kocha wa pili kuwahi kushinda Kombe la Ulaya mara tatu baada ya Bob Paisley wa Liverpool aliyeshinda katika mwaka wa 1977,1978 na 1981.

Muitaliano Ancelotti pia alishinda kombe hilo kama mchezaji akiwa na AC Milan mwaka wa 1989 na 1990, wakati Real ikiwa timu ya kwanza kufunga magoli manne katika fainali tangu ushindi wa Milan wa magoli wa manne kwa sifuri dhidi ya Barcelona mwaka wa 1994.

Naye kocha wa Atletico Madrid Diego Simeone aliamrishwa kuondoka uwanjani na refarii Bjorn Kuipers kwa kuingia ndani ya uwanja baada ya Atletivo kufungwa goli la nne, lakini baadaye akatulia wakati akiwahutubia waandishi wa habari.

Muargentina huyo alisema alikasirishwa kwa sababu beki wa Real Raphael Varane aliupiga mpira katika upande wake lakini akaongeza kuwa hakustahili kuonyesha tabia hiyo. Maelfu ya mashabiki wa Real Madrid wamesherehekea Kombe lao la Kumi la mabingwa wa barani Ulaya mapema leo katika mji mkuu wa Uhispania, Madrid. Walikusanyika katika uwanja wa Cibeles kuilaki timu yao iliyowasili na kombe hilo ndani ya basi lililoandikwa "Mabingwa". Uwanja wa Cibeles kwa desturi hutumiwa na mashabiki na wachezaji wa Madrid kusherehekea ushindi wao.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Mohammed Dahman