1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Real Madrid yashinda kombe la Mabingwa barani Ulaya

Josephat Charo
26 Mei 2018

Gareth Bale alitoka kwenye mbao ndefu na kuja kuipatia ushindi Real Madrid. Katika lango la Liverpool, Loris Karius wa Ujerumani alikuwa na usiku mbaya ambao angependa ausahau haraka.

https://p.dw.com/p/2yNtc
Champions League Final - Real Madrid v Liverpool - Real Madrid gewinnt Finale
Nahodha wa Real Madrid, Sergio Ramos, akilinyanyua kombe la mabingwa Ulaya baada ya kutawazwa mabingwa mjini KievPicha: Reuters/K. Pfaffenbach

Mshambuliaji wa Real Madrid Gareth Bale alifunga bao la pili kupitia "mbilimbili" kwa guu lake la kushoto na bao lake la pili kupitia mkwaju alioupiga pia kwa guu lake la kushoto na kuipa timu yake ushindi wa mabao 3-1 katika fainali ya kombe la mabingwa Ulaya, Champions League. Huu ni ushindi wa tatu mfululizo wa Real Madrid.

Bale, ambaye ametokea katika mbao ndefu, na ambaye pia alifunga bao wakati wa fainali ya mwaka 2014 kati ya Real na Atletico Madrid, alikuwa amekaa uwanjani kwa dakika tatu hivi wakati aliporuka juu mbilimbili na kuupiga mpira kufuatia pasi maridadi majimaji kutoka kwa Marcelo, nje kidogo na eneo la hatari la lango la Liverpool. Mpira ukautikisa wavu wa Liverpool na kuiwezesha Real kuongoza kwa mabao 2-1 dakika ya 64 katika uwanja wa Olympic Stadium mjini Kiev nchini Ukraine.

Kipindi cha pili kilianza kwa kisa cha kushangaza ambapo Karim Benzema aliipatia timu yake ya Real bao la kwanza baada ya kosa kubwa lililofanywa na mlinda lango wa Liverpool, Loris Karius. Sadio Mane alisawazisha dakika chache baadaye, lakini Bale akaiweka tena Real kifua mbele.

Cristiano Ronaldo sasa ameshinda mataji matano ya ligi ya mabingwa wa Ulaya katika maisha yake ya kusakata soka, lakini hata yeye hawezi kuhoji kwamba usiku wa leo ulikuwa wake Gareth Bale. Mchezaji huyo kutoka Wales alitarajiwa kucheza katika kikosi cha kwanza cha Real lakini akaachwa nje na nafasi yake ikachukuliwa na Isco. 

Jeraha la Salah pigo kwa Liverpool

Jurgen Klopp na Liverpool walipata pigo wakati Mohamed Salah alipoumia katika kipindi cha kwanza, na kulazimika kutoka nje ya uwanja baada ya dakika 30 alipojiumiza katika bega lake.

Huu haukuwa usiku wa Salah, huku Real wakimuwezesha Zinedine Zidane kuwa kocha wa kwanza kuwahi kushinda kombe la mabingwa wa Ulaya miaka mitatu mfululizo. Madrid ni timu ya kwanza kufaulu kufanya hivyo tangu Bayern Munich mnamo mwaka 1976. Hili ni taji lao la nne katika kipindi cha miaka mitano, na ni la 13.

Champions League Final - Real Madrid v Liverpool - Verletzung Salah
Mohamed Salah, wa pili kutoka kulia, akiwa na Cristiano Ronaldo (Real Madrid) na Sadio Mane (Liverpool)Picha: Reuters/P. Noble

Kwa upande wa Liverpool, mechi hii itakumbukwa kwa janga lililomkuta mlinda lango Loris Karius katika kipindi cha pili, na kwa machozi ya Salah wakati alipokuwa akitoka uwanjani Olympic Stadium. Raia huyo wa Misri ambaye ameifungia Liverpool mabao 44 msimu huu, alijiumiza bega lake alipokuwa akianguka chini baada ya kukabiliana na Sergio Ramos dakika ya 25. Dakika tano baadaye akampisha Adam Lallana. 

Uwezekano wa Salah kushiriki mashindano ya kuwania kombe la dunia nchini Urusi umeingia mashakani, pamoja na Dani Carvajal, beki wa kulia wa Real aliyetoka nje ya uwanja baada ya kupata jeraha katika misuli kabla kipindi cha mapumziko. Majeaha hayo yaliifanya kasi ya mchezo kupwaya na kupoteza utamu uliokuwepo tangia mwanzo, huku Liverpool ikidhibiti mchezo. 

Kocha wa Liverpool Jurgen Klopp amedokeza kwamba jerah ala Mohamed Salah ni baya. "Ni jeraha baya. Yuko hospitalini akifanyiwa vipimo na kupigwa picha ya X-ray. Huenda ameumia mfupa unaoiunganisha shingo na bega au bega lenyewe," alisema Klopp baada ya kupoteza mechi ya fainali na Real Madrid. 

Real walitiwa tumbo joto na kutolewa kijasho, lakini baada ya Salah kutoka, wakahisi wana fursa ya kushinda. Walifaulu kushinda bao dakika ya 43, lakini halikukubaliwa baada ya kuonekana walikuwa wameotea.

 Mwandishi: Josephat Charo/rtre/afp