1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rasimu dhidi ya silaha za nyuklia yaanza kutekelezwa

Saumu Mwasimba
22 Januari 2021

Utekelezaji wa rasimu ya kwanza kabisa inayopiga marufuku silaha za Nyuklia unaanza Ijumaa. Na hatua hiyo imetajwa kuwa ya kihistoria kuelekea juhudi za kuondowa kabisa silaha hizo duniani.

https://p.dw.com/p/3oGxc
Symbolbild Atombombe
Picha: Getty Images/AFP/F. Naeem

Ni hatua iliyopongezwa ikitajwa kama mwanzo wa kuelekea kuziondowa kabisa silaha hizo za maangamizi duniani, lakini pia imepingwa na nchi zinazomiliki silaha hizo duniani.

Mkataba huo wa kupiga marufuku na kuzuia silaha za nyuklia sasa ni sehemu ya sheria ya kimataifa uliotokana na kampeni ya muda mrefu ya kutaka kuzuiwa kujirudia kwa matukio yaliyofanywa na Marekani ya mashambulizi ya mabomu ya nyuklia huko Hiroshima na Nagasaki nchini Japan mwishoni mwa vita vya pili vya dunia.

Soma pia: Nchi zenye silaha za nyuklia zinazifanya za kisasa zaidi: SIPRI

Hata hivyo, katika mazingira ya sasa duniani, imekuwa vigumu kama sio kutowezekana kabisa, kuyashawishi mataifa yote kuidhinisha mkataba huo unaozihitaji nchi hizo kutomiliki kabisa silaha hizo. Wakati rasimu hiyo ilipoidhinishwana Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mnamo mwezi Julai mwaka 2017, zaidi ya nchi 120 zilishiriki kutia saini.

Soma pia: Ujerumani yaelezea wasiwasi kuhusu silaha za nyuklia

Kuanzia Ijumaa 22.01.2021 silaha za nyuklia zimepigwa marufuku katika nchi 60 zilizosaini mkataba unaopinga matumizi yake.
Kuanzia Ijumaa 22.01.2021 silaha za nyuklia zimepigwa marufuku katika nchi 60 zilizosaini mkataba unaopinga matumizi yake.Picha: picture-alliance/dpa/T. Frey

Lakini hakuna hata nchi moja kati ya zile tisa zinazojulikana au kuaminika kumiliki sialaha hizo iliyounga mkono rasimu hiyo, yaani Marekani, Urusi, Uingereza, China, Ufaransa, India, Pakistan, Korea Kaskazini na Israel. Na pia hakuna mwanachama yoyote wa jumuiya ya kujihami ya NATO yenye wanachama 30 aliyeunga mkono.

Japan nchi pekee duniani iliyowahi kuathirika na mashambulizi ya mabomu ya nyuklia nayo pia haiuungi mkono makataba huo licha ya kwamba raia wake walionusirika katika mashambulizi hayo ya mwaka 1945 ambao ni wazee waliishinikiza sana iunge mkono.

Japan binafsi inapinga matumizi na umiliki wa silaha za nyuklia lakini serikali inasema kupataka makubaliano ya kupiga marufuku kabisa silaha hizo sio jambo linalowezekana katika hali ambapo yanashuhudiwa mataifa yanayomiliki silaha hizo na yale yasiokuwa na silaha hizo yakiwa katika mgawanyiko mkubwa kuhisiana na suala hilo.

Japan ambayo ni nchi pekee duniani iliyowahi kuathirika na mashambulizi ya mabomu ya nyuklia haiuungi mkono mkataba unaopiga marufuku silaha za nyuklia.
Japan ambayo ni nchi pekee duniani iliyowahi kuathirika na mashambulizi ya mabomu ya nyuklia haiuungi mkono mkataba unaopiga marufuku silaha za nyuklia.Picha: AP Photo/picture-alliance

Beatrice Fihn, mkurugenzi mtendaji wa shirika la harakati ya kimataifa ya kuziondowa kabisa silaha za nyuklia, ukiwa ni muungano uliotunukiwa mwaka 2017 tuzo ya amani ya Nobel, ambao shughuli zake zilisaidia kuisimamia rasimu hiyo, anasema kuanzishwa utekelezaji wa mkataba huo ni siku nzuri kwa sheria ya kimataifa, kwa Umoja wa Mataifa na kwa walionusurika katika mashambulizi ya Hiroshima na Nagasaki.

Oktoba 24 mwaka jana mkataba huo ulipata saini ya 50 iliyochochea mchakato wa kuanza kuhesabiwa siku 90 kabla ya kuanzishwa utekelezaji wake yaani leo Januari 22. Kufikia jana Alhamisi, Fihn aliliambia shirika la habari la Associated Press kwamba nchi 61 tayari zilikuwa zimekwishasaini rasimu hiyo huku ukiwepo uwezekano wa nchi nyingine kuusaini hii leo.

Kwa maana nyingine ni kwamba kuanzia leo silaha za nyuklia zimepigwa marufuku katika nchi hizo zote kwa mujibu wa sheria ya kimataifa. Rasimu hii inazitaka nchi zote zilizosaini kutojishuhisha kwa namna yoyote na silaha hizo.