Ramaphosa: Afrika pia inahitaji chanjo ya COVID-19 | Matukio ya Kisiasa | DW | 26.01.2021
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Ramaphosa: Afrika pia inahitaji chanjo ya COVID-19

Rais wa Afrika Kusini na mwenyekiti wa Umoja wa Afrika Cyril Ramaphosa ameyatolea wito mataifa tajiri kutohodhi dozi za ziada za chanjo ya Covid-19, akisema dunia inahitajimkuja pamoja kupambana na janga hilo.

Ramaphosa ametoa wito huo katika hotuba yake kwa mkutano wa jukwaa la kiuchumi la kimataifaunaofanyika kwa njia ya mtandao, ambapo pia amezumgumzia juhudi za Umoja wa Afrika kupata chanjo hiyo pamoja na athari za janga la covid-19 barani humo.

Afrika Kusini imerikodi karibu nusu ya vifo vyote vinavyotokana na virusi vya corona barani Afrika, na bara hilo kwa ujumla linapambana kupata dawa za kutosha ili kuanzisha programu za utoaji chanjo nchi nzima kwa ajili ya wakaazi wake bilioni 1.3. Ramaphosa amezita nchi zinazohodhi dawa hizo kuziachia ili mataifa mengine yaweze pia kuzipata.

Mataifa tajiri duniani yalinunua chanjo nyingi kutoka kwa watengenezaji wa dawa hizo. Na baadhi ya mataifa yamekwenda mbali kwa kuchukuwa hadi mara nne zaidi ya wanachohitaji raia wake kwa lengo la kuhodhi dawa hizi na hili linafanyika kwa kuzitenga nchi nyingine duniani ambazo zinahitaji zaidi dawa hizi.

Mkurugenzi mkuu wa shirika la afya duniani WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus, wiki iliyopita aliuelezea upatikanaji huu usio wa usawa kama janga la kushindwa kwa kimaadili, akizihimiza nchi na watengenezaji kusambaza dawa hizo kwa usawa zaidi kote duniani.

Weltwirtschaftsforum Davos | Angela Merkel in Videokonferenz

Kansela Merkel katika kongamano la kimataifa la uchumi

Ramaphosa ni mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, ambao mwezi huu ulipata dozi milioni 270 za dawa ya chanjo hiyo kwa bara hilo kuongezea juu ya milioni 600 zinazotoka kwenye mpango wa Covax unaoongozwa kwa pamoja na WHO.

Dozi hizo zinatarajiwa kupatikana mwaka huu lakini bado hazijawasili, huku baadhi ya maeneo ya Ulaya, Asia na Amerika yakiwa tayari yameshaanza kutoa chanjo kwa raia wake.

Uingereza imeagiza dozi milioni 367 za chanjo tofautitofauti kwa ajili ya wakaazi wake milioni 67, huku Umoja wa Ulaya ukiwa tayari umepata karibu dozi bilioni 2.3 kwa ajili ya wakaazi wake milioni 450.

Akizungumza kwenye mkutano huo, kansela wa Ujerumani Angela Merkel amehimiza pia kuwepo na usambazaji wa haki wa chanjo duniani, na kuonya kuwa kumbukumbu za mataifa yalioachwa katika mbio za kupata chanjo hiyo inayookoa maisha zitaendelea kuwepo.

Merkel amesema pesa ni kitu kimoja, lakini kitu kingine katika wakati wa uhaba, ni upatikanaji wa chanjo, na katika mazingira haya kilichomuhimu ni usambazaji unoazingatia haki na usawa, na siyo suala la pesa.