1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Wulff ahudhuria kumbukumbu ya Auschwitz

28 Januari 2011

Rais wa Ujerumani Christian Wulff leo amehudhuria kumbukumbu ya miaka 66 tangu kukombolewa kwa kambi ya Auschwitz ya mateso dhidi ya Wayahudi nchini Poland, kulikofanywa na majeshi ya lililokuwa Shirikisho la Kisovieti.

https://p.dw.com/p/Qw6F
Bundespraesident Christian Wulff legt am Donnerstag (27.01.11) in Auschwitz (Polen) auf dem Gelaende des ehemaligen Konzentrationslagers (KZ) Auschwitz-Birkenau bei der offiziellen Gedenkfeier zur Befreiung des Konzentrationslagers am Denkmal der Opfer des Konzentrationslagers Auschwitz-Birkenau eine Kerze nieder. Die Befreiung des KZ Auschwitz durch die Rote Armee jaehrt sich am Donnerstag zum 66. Mal. Anlaesslich des Holocaust-Gedenktags reist Bundespraesident Wulff nach Polen und haelt in Auschwitz als erstes deutsches Staatsoberhaupt eine Rede. (zu dapd-Text) Foto: Michael Gottschalk/dapd
Rais Wulff alipohudhuria kumbukumbu ya AuschwitzPicha: dapd

Rais Wulff na rais mwenzake wa Poland, Bronislaw Komorowski, walikutana na wafungwa wa zamani wa kambi hiyo na vijana kutoka Ujerumani na Poland. Wanafunzi wa shule ya sekondari ya Jacob-Grimm kutoka Kassel, nchini Ujerumani wamekamilisha wiki moja katika mji wa Auschwitz. Wamehuzunishwa kwa yale waliyoshuhudia wakati wa ziara yao katika kambi kuu ya Auschwitz, kambi ya zamani ya maangamizi huko Birkenau na hata mazungumzo yao mbali mbali pamoja na vijana wenzao wa Poland. Msichana mmoja alisema:

"Inahuzunisha sana na hata ukubwa wa kambi yenyewe. Hasa kambi ya Birkenau ni kubwa kweli. Tulizunguka huko, nusu siku na ilituhuzunisha sana."

Wulff akumbuka utotoni

Walipokutana na marais Christian Wulff na Bronislaw Komorowski, ambao wote wawili walizaliwa baada ya Vita Vikuu vya Pili, vijana hao walitaka kujua lini na kwa sababu gani wanasiasa hao, walianzisha mdahalo wa maangamizi ya Wayahudi. Wulff, alizungumzia kwao nyumbani Niedersachsen. Amesema, karibu na Kanisa la Kikatoliki kulikuwepo jamii ya Wayahudi.

"Tangu ujanani mwangu, niliona kuwa jamii hiyo ya Wayahudi ilikuwa na eneo kubwa lakini halikuwa na wakaazi wengi. Kwa hivyo, nikauliza kipi kilichotendwa na Wajerumani katika historia yao."

Naye, Komorowski alieleza kuhusu baba yake, aliyepigana vita dhidi ya Wajerumani. Hata hivyo, baadaye aligombea suluhu. Hiyo ni njia pekee iliyo sahihi, alisisitiza Zofia Posmysz, aliyenusurika kutoka kambi ya Auschwitz. Mkaazi huyo wa Warsaw ambaye sasa ana umri wa miaka 87, ameandika vitabu mbali mbali, hiyo ikiwa ni kama njia ya kukabiliana na yale aliyoshuhudia kama mfungwa namba 7566. Mara kwa mara, yeye huenda mji wa mkutano wa kimataifa wa Auschwitz ambako hukutana na hujadiliana na vijana kutoka Poland na Ujerumani.

"Mikutano yangu na vijana hao inanipa matumaini kwani wanakuja kwa hiyari kwa sababu wanataka kujua ukweli kuhusu Auschwitz na hivyo kujikinga dhidi ya itikadi za uhalifu." Anasema Posmysz.

Wulff amesema, kwake ni heshima kubwa kama Rais wa Ujerumani kuwepo Auschwitz siku ya leo. "Licha ya Wajerumani kusababisha huzuni mkubwa miongoni mwa Wapoland na Wayahudi, tumenyoshewa mkono wa upatanisho. Wakati huo, hakuna alietarajia hilo, haikutazamiwa kutokea hata baada ya miongo kadhaa. Ni zawadi kubwa na ninatoa shukrani zangu."

Mwandishi: Kazmierczak, Ludger/ZPR
Mpitiaji: Mohammed Abdul-Rahman