1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais William Ruto atetea uongozi wake wa miaka miwili

16 Septemba 2024

Rais William Ruto wa Kenya ametetea rikodi yake ya miaka miwili madarakani akisema hakuna serikali ya nchi hiyo iliyowahi kuweka mikakati madhubuti ya kuiendeleza Kenya kuliko ile anayoiongoza.

https://p.dw.com/p/4keKS
Kansela wa Ujerumani na Rais wa Kenya
Rais William Ruto alikuwa nchini Ujerumani ambapo pamoja na mengineyo amesaini mikataba inayofungua fursa za ajira kwa watu wa KenyaPicha: epd

Rais Ruto ameyasema hayo kwenye mahojiano maalumu na Idhaa ya Kiswahili ya DW yaliyofanyika mjini Berlin wakati alipofanya ziara ya siku mbili nchini Ujerumani wiki iliyopita.

Alipozungumzia malalamiko ya umma juu ya gharama kubwa za maisha na ukosefu wa ajira, amesema rikodi ya serikali yake haina mpinzani, akijinadi kwamba tangu alipoingia madarakani ameweka mikakati ya makusudi ya kushughulikia changamoto zinazolikabili taifa hilo.

Rais wa Kenya William Ruto aadhimisha miaka miwili madarakani

Alikuwa mjini Berlin kushiriki Tamasha la Wananchi wa Ujerumani ´BürgerFest´ ambalo huandaliwa kila mwaka na Ofisi ya Rais wa Ujerumani, pamoja na kutia saini mkataba utakaowezesha maelfu ya Wakenya wenye ujuzi kupata kazi nchini Ujerumani.