1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa zamani wa Iran alaumiwa kuhusu hotuba yake

P.Martin5 Mei 2008

Rais wa zamani wa Iran Mohammad Khatami amelaumiwa vikali na wafuasi wa siasa kali,baada ya matamshi yake kutafsiriwa kama ni kuwashutumu viongozi wa kidini wa Iran kuwa wanawaunga mkono waasi katika Mashariki ya Kati.

https://p.dw.com/p/Du3N
Iranian President Mohammad Khatami, gestures during his speech at Tehran university in Tehran, Iran Monday, Dec. 6, 2004. In his final months in office, Iran's embattled President Mohammad Khatami admitted Monday he failed to implement his program of democratic reforms but said he refused a head-to-head collision with his hard-line opponents to save the ruling Islamic establishment. (AP Photo/Hasan Sarbakhshian)
Mohammad Khatami aliekuwa rais wa Iran.Picha: AP

Khatami alipowahotubia wanafunzi wa chuo kikuu siku ya Ijumaa,katika wilaya ya Gilan kaskazini mwa Iran,alizungumzia azma ya kiongozi wa mapinduzi ya Iran Ayatollah Ruhollah Khomenei,kueneza mapinduzi ya Kiislamu ya mwaka 1979 kote duniani.Wakati huo huo Khatami akasema kuwa ana hofu kwamba nia hiyo inaeleweka visivyo.

Akauliza matamshi ya Ayatollah Khomeini "kueneza mapinduzi" humaanisha kitu gani.Je,ni kunyanyua silaha na kuripua majengo katika nchi zingine au kuunda makundi ya kuhujumu mataifa mengine? Hapo hapo lakini akaongezea kuwa yote hayo ni mambo yanayopingwa vikali na Khomeini.

Hata hivyo,mhariri mkuu wa gazeti la Kayhan lenye msimamo mkali wa kihafidhina,amemtuhumu Khatami kuwa ametia doa sifa na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.Si hilo tu bali amethibithisha shutuma za madola kiburi,ambazo hazina msingi wo wote.Kwani kwa maoni ya baadhi ya wachambuzi,hotuba hiyo inawatuhumu viongozi wa Iran kuwa inawachochea wanamgambo kusababisha vurugu katika Mashariki ya Kati na hasa nchini Iraq na Lebanon.

Hata tovuti ya wahafidhina Tabnak imekituhumu kituo cha televisheni cha Al Arabiya kinachogharimiwa na Saudi Arabia,kuwa kimepotosha hotuba ya Khatami kama ni shutuma kuwa Iran inaeneza machafuko na migogoro katika nchi zingine.

Kwa kweli,mabishano hayo yamezuka wakati mbaya,kwani Marekani imezidi kuishutumu Iran yenye wakaazi wengi wa madhehebu ya Kishia kuwa inatoa silaha na mafunzo kwa wanamgambo wa Kishia nchini Iraq-na inasababisha mivutano huko Lebanon kupitia kundi la Kishia la Hezbollah.

Iran lakini inakanusha vikali shutuma hizo kuwa inasababisha machafuko nchini Lebanon na Iraq. Inasema,migogoro katika nchi hizo mbili ni matokeo ya kuvamiwa na mataifa ya kigeni.