Putin atangaza sitisho la mapigano Pasaka
10 Aprili 2026
Amri ya Putin, iliyotolewa na Ikulu ya Urusi, inaelekeza majeshi ya nchi hiyo kuheshimu usitishaji mapigano kuanzia saa 10 jioni Jumamosi hadi mwisho wa Jumapili. Mapema wiki hii, Rais wa Ukraine Volodymir Zelenskyy alipendekeza kila upande uache kushambulia miundombinu ya nishati ya mwenzie wakati wa sikukuu, akisema alitoa pendekezo hilo kupitia Marekani, ambayo ni mpatanishi katika mazungumzo kati ya wajumbe wa Moscow na Kyiv huku uvamizi wa Urusi ukiingia mwaka wake wa tano.
Taarifa ya Kremlin iliyotangaza usitishaji mapigano ilisema kuwa "maelekezo yametolewa kwa kipindi hiki kusitisha mapigano katika pande zote,” na ikaongeza kuwa "wanajeshi wanapaswa kuwa tayari kujibu uchokozi wowote unaoweza kufanywa na adui, pamoja na vitendo vyovyote vya mashambulizi.”
Makubaliano ya kuweka bunduki chini yatatekelezeka?
Nikiendelea na nukuu hapa inasema "Tunahisi kuwa upande wa Ukraine utafuata mfano wa Shirikisho la Urusi,” taarifa hiyo ilisema. Urusi imekataa kwa kiasi kikubwa pendekezo la kusitisha mapigano kwa siku 30 bila masharti, lililopendekezwa mwaka jana na Marekani na Ukraine kama hatua ya kuelekea amani, ikisisitiza badala yake suluhu ya kina.
Kupitia mitandao ya kijamii rais Zelensky ameandika "Ukraine imesema mara kadhaa kuwa iko tayari kuchukua hatua za mwafaka kwa pande zote mbili. Tumependekeza usitishaji mapigano wakati wa sikukuu za Pasaka mwaka huu na tutachukua hatua kulingana na hilo. Wananchi wanahitaji Pasaka isiyo na vitisho na yenye hatua za kweli kuelekea amani, na Urusi ina nafasi ya kutoanza tena mashambulizi baada ya Pasaka pia".
Mzee wa umri wa miaka 80 aliyetambulishwa kwa jinja moja la Andrii anasema "Unawezaje kumwamini mtu ambaye amewaangamiza watu wake mwenyewe, ameshambulia Ukraine, na kimsingi ndiye gaidi namba moja. Unawezaje kumwamini? Anasema uongo tu.”
Mwaka uliopita wakati wa Pasaka, Putin alitangaza kwa upande mmoja usitishaji mapigano wa saa 30, lakini kila upande uliushutumu mwingine kwa kuuvunja.
Mapigano makali yanaendelea katika eneo la urefu wa kilometa 1,250
Mazungumzo yanayoongozwa na Marekani hayajapiga hatua katika masuala muhimu, na Washington sasa imeelekeza umakini wake kwenye mzozo wa Mashariki ya Kati, huku majeshi ya Urusi na Ukraine yakiendelea kupigana kwenye mstari wa mbele wenye urefu wa takriban kilometa 1,250.
Katika hatua nyingine Rais Zelenskiy amesema kuwa miezi ya masika na kiangazi itakuwa migumu kwa Ukraine, kwani itakabiliwa na shinikizo kubwa uwanjani vitani pamoja na shinikizo la kidiplomasia la kumaliza vita. Zelenskiy alisema kuwa washirika wa Ukraine wameiomba Kyiv kupunguza mashambulizi yake dhidi ya sekta ya mafuta ya Urusi, wakati bei za mafuta duniani zikiongezeka kutokana na vita nchini Iran na kuongezeka kwa mvutano katika Mashariki ya Kati.
Hakutaja majina ya washirika hao.Hata hivyo, amesema kwamba iwapo Urusi inataka kupunguza mvutano, inapaswa kusitisha mashambulizi yake dhidi ya miundombinu ya nishati ya Ukraine na kukubali kurejea kwenye mazungumzo ya amani ya pande tatu, yanayosimamiwa na Marekani.
Lakini pia ameonea kuwa kwa sasa Marekani inaonekana kusita kutenga muda zaidi kwa ajili ya mchakato wa amani nchini Ukraine.