Rais wa Ujerumani ziarani nchini Brazil | Matukio ya Kisiasa | DW | 09.03.2007
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Rais wa Ujerumani ziarani nchini Brazil

Rais Horst Köhler wa Ujerumani anaendelea na ziara yake nchini Brazil ikiwa ni ziara rasmi ya kwanza kufanywa na kiongozi huyo barani Amerika ya Kusini.

Mada kuu za rais wa Ujerumani hasa ni juhudi za kupiga vita umasikini pamoja na sera zinazohusika na nishati.

Mjini Brasilia,rais Horst Köhler alikutana na rafiki wake wa zamani Rais Lula da Silva wa Brazil.Ingawa kiongozi huyo wa Brazil hufuata siasa za mrengo wa kushoto,urafiki wa viongozi hao wawili ulianza wakati ambapo Köhler alikuwa mkuu wa Shirika la Fedha la Kimataifa IMF.Köhler amesema umasikini na ukosefu wa usawa katika jamii ni matatizo makuu ya Brazil na amesifu bidii za mwenyeji wake kutaka kuibadilisha hali hiyo kuwa bora.Vile vile amesifu juhudi za serikali ya Brazil kutumia pesa zaidi katika sekta ya elimu na kuendeleza huduma za afya yaani kugombea kuleta usawa wa kijamii.

Mada nyingine kuu iliyojadiliwa na rais Köhler ni ushirikiano kati ya Ujerumani na Brazil katika sekta ya nishati mbadala.Kwa maoni yake ushirikiano huo unapaswa kuimarishwa kwani Brazil ina malighafi,hasa miwa inayoweza kutumiwa kutengeneza nishati mbadala-bioethanol.Makampuni ya Kijerumani bila shaka yanataka kushiriki katika biashara hiyo.Kuhusu suala hilo Köhler amesema anaamini kuwa Ujerumani,kwa sababu ya ujuzi wake wa kifundi,ni mshirika dhahiri linapohusika suala la ufanisi wa nishati;nishati mbadala na hata mashine.

Lakini hata rais Lula da Silva alieleza matakwa yake.Yeye amesema,Ujerumani ingejitahidi zaidi kugombea utaratibu wa haki katika Shirika la Biashara Duniani hasa kuhusika na Marekani.Lakini kwa maoni ya Rais Köhler,tayari juhudi zinachukuliwa kuwa na uhuru katika masoko ya kimataifa.Kwa maoni yake,Mkataba wa Doha kuhusika na biashara duniani ni ufunguo wa kupiga vita umasikini kwa mafanikio.

Rais Lula da Silva lakini hajakubaliana na maoni hayo.Yeye amesema ilimradi hakuna makubaliano ya kuzipa nafasi nchi zilizo masikini kabisa duniani,basi itakuwa shida kupiga vita umasikini na njaa na kukomesha ugaidi.

Wakati huo huo ni matumaini ya rais wa Brazil kuwa makampuni ya Kijerumani ambayo tayari ni wawekezaji wakuu nchini humo,yataweka vitega uchumi zaidi.Rais Lula ameeleza kuwa hivi sasa nchini Brazil kuna makampuni ya Kijerumani 1,200 amabayo huchangia kama asilimia 8 ya pato la ndani la Brazil.Amesema ushirikiano wa ufundi katika sekta ya mazingira vile vile ungeweza kuimarishwa.Kwani ulinzi wa mazingira na ukuaji wa kiuchumi ni mambo yasiopingana aliongezea Lula da Silva.Rais Köhler kwa upande wake amewaambia wenye mali wa Kibrazil na Kijerumani kuwa sekta ya kiuchumi inapaswa kuwa na dhima zaidi kuhusu jamii.

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com