Rais wa Ujerumani Horst Köhler ajiuzulu | Matukio ya Kisiasa | DW | 31.05.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Rais wa Ujerumani Horst Köhler ajiuzulu

Rais wa Ujerumani Horst Köhler amejiuzulu leo kufuatia ukosoaji wa matamshi yake ya hivi karibuni kuhusu jukumu la wanajeshi wa Ujerumani nchini Afghanistan. Köhler ni rais wa kwanza wa Ujerumani kujiuzulu wadhifa wake.

default

Rais Horst Köhler akitangaza kujiuzulu kwake mjini Berlin

Kulikuwa na hali ya sintofahamu wakati waandishi habari walipokusanyika mwendo wa saa nane leo mchana katika ikulu ya rais mjini Berlin. Muda wa saa nzima unusu kabla, rais Köhler alikuwa amewaalika waandishi habari bila kutaja mada aliyotaka kuizungumzia. Lakini kiongozi huyo alipojitokeza pamoja na mke wake, Luis, ikabainika wazi kwamba anataka kusema jambo zito.

"Natangaza kujiuzulu kwangu kama rais wa Ujerumani mara moja. Nawashukuru watu wengi nchini Ujerumani walioniamini na kuiunga mkono kazi yangu. Nawaomba wanielewe kwa uamuzi wangu"

Katika hatua ya kushangaza rais wa Ujeruamani Horst Köhler amesema anajizulu mara moja kwa sababu ukosoaji mkali uliojitokeza baada ya kutoa kauli kuhusu tume ya jeshi la Ujerumani nchini Afghanistan, umevuruga hadhi ya ofisi yake.

Rais Köhler amesema amemfahamisha kansela wa Ujrumani Angela Merkel kuhusu uamuzi wake na kuwashukuru watu wengi nchini Ujerumani waliomuamini na kumuunga mkono kazi yake. Rais Köhler aidha amewataka Wajerumani wamuelewe kwa uamuzi wake.

Akizungumza kuhusu kijiuzulu kwa rais Köhler, kansela Merkel amesema, "Nimeshangazwa na aliyoniambia rais Köhler kwenye simu na nilijaribu kumshawishi abadilishe msimamo wake, lakini kwa bahati mbaya sijafanikiwa. Nasikitika sana kwa uamuzi huo na naheshimu uamuzi wake."

Bundeskanzlerin Angela Merkel Rücktritt Horst Köhler

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel akizungumzia kuhusu kujiuzulu kwa rais Köhler

Rais Köhler aliwekwa katika kiti moto kwa kusema kwamba kwa nchi inayotegemea uuzaji wa bidhaa katika nchi za nje kama Ujerumani, kuna haja mara kwa mara kuyalinda masilahi yake ya kiuchumi kwa kuzuia mizozo ya maeneo mbalimbali kama ule wa nchini Afghanistan. Kiongozi huyo aliiambia redio ya Ujerumani mnamo Mei 22 mwaka huu kwamba mizozo kama hiyo bila shaka inawaathiri Wajerumani kupitia biashara, ajira na mapato.

Akizungumzia kauli yake hiyo wakati wa mkutano wa waandishi hbari mjini Berlin rais Köhler amesema, "Nasikita kwamba matamshi yangu kuhusu suala muhimu na gumu kwa nchi yetu yangeweza kusababisha kueleweka vibaya. Lawama zimekwenda mbali kiasi kwamba ofisi yangu imepoteza heshima yake muhimu."

Rais Köhler, ambaye alianza kushika wadhifa wa urais wa Ujerumani mnamo mwaka 2004, alichaguliwa kwa mara ya pili kuendelea na wadhifa huo mwaka jana. Spika wa baraza la wawakilishi la majimbo kutoka Bremen, Jens Böhrnsen, atachukua majukumu ya rais Köhler mpaka rais mpya atakapochaguliwa baada ya siku 30. Kabla rais Köhler kuondoka chumba cha mkutano pamoja na mke wake, amesema ilikuwa heshima kubwa kwake kuitumikia Ujerumani kama rais.

Mwandishi:Nina Werkhäuser/ZR/Josephat Charo

Mpitiaji :M.Abdul-Rahman

 • Tarehe 31.05.2010
 • Mwandishi Josephat Nyiro Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Ne7U
 • Tarehe 31.05.2010
 • Mwandishi Josephat Nyiro Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Ne7U

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com