1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa Ujerumani azuru Tanzania

3 Februari 2015

Rais wa Ujerumani Joachim Gauck yuko nchini Tanzania kwa ziara rasmi ya siku sita. Kiongozi huyo amepokewa na mwenyeji wake Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania.

https://p.dw.com/p/1EUrA
Gauck in Tansania 03.02.2015 Daressalam
Rais wa Ujerumani, Joachim Gauck na mwenyeji wake rais Jakaya Kikwete wa TanzaniaPicha: DW/M. Khelef

Rais Gauck ambae anatarajiwa kufanya mazungumzo na matabaka mbalimbali ya viongozi nchini Tanzania amewasili jana jioni. Baada ya hafla ya mapokezi iliyofanyika katika Ikulu ya Dar es Salaam viongozi hao wawili, Rais Kikwete na Gauck, walifanya mazungumzo ya faragha, na baadae kukutana na waandshi habari.

Pembezoni mwa mazungumzo ya viongozi hao wawili, kulifanyika pia mazungumzo ya wake wa marais, Mama Salma Kikwete na Bibi, Daniela Schadt, mke wa rais Gauck. Mke huyo wa Rais Gauck atazitembelea taasisi tatu, ikiwemo WAMA, inayosimamiwa na rais mke wa Rais Kikwete na kisha hospitali ya tiba maalum za viungo ya CCBRT ya jijini Dar es Salaam.

Pamoja na tiba ya macho hospitali hiyo inafanya upasuaji kwa watoto wenye kuzaliwa na kasoro ya kinywa, maarufu kama midomo sungura na tatizo la fistula kwa wanawake. Katika ziara hiyo ya siku sita pamoja na mambo mengine Rais Gauck anapata fursa ya kuzungumza na wadau kutoka katika asasi za kiraia.

Tansania Daressalam Empfang von Bundespräsident Gauck 2.2.2015
Wakazi wa jiji la Dar es Salaam wakimpokea rais wa UjerumaniPicha: picture-alliance/dpa/Wolfgang Kumm

Matarajio ya Watanzania

Mkurungezi wa Idaya ya Habari na maelezo ya nchini Tanzania anasema kikubwa kinachotarajiwa kwa Watanzania wengi ni kuimarika kwa ushirikiano baina ya mataifa hayo mawili hasa kwa kuzingatia fursa ziliopo za maendeleao.

Historia ya uhusuano wa Ujerumani na Tanzania

Kihistoria Ujerumani na Tanzania zimekuwa na uhusiano wa karibu tangu zama za Ukoloni. Tanganyika ilikuwa koloni la Ujerumani kwa takribani miaka mia moja iliyopita. Ushirikiano huo umekuwa katika nyanja tofauti kuanzia kisiasa, kiutamadauni, kiuchumi na hata katika suala la imani za kidini. Lakini mchambuzi kutoka wakfu wa Kijerumani wa Konrad Adenauer i, ofisi ya Dar es Salaam, Richard Shaba anasema kwa hivi sasa mambo yamebadilika kabisa " Ujerumani haijihusishi tena na Ukoloni.

Baada ya Tanganyika kuwa taifa huru, mahusiano ya kidiplomasia yalianza baina yake na Ujerumani. Kulikuwa na wakati mgumu mwaka 1964 pale ambapo Tanganyika na Zanzibar zilipoungana. Zanzibar ilikuwa na uhusiano na Ujerumani Mashariki na Tanganyika ikiegemea Ujerumani Magharibi. Wakati ule wa Vita Baridi, Ujerumani Magharibi ilikataa washirika wake wawe na uhusiano na Ujerumani Mashariki. Rais wa Tanzania Hayati Julius Kambarage Nyerere aliona hayo kuwa ni kuingilia masuala ya ndani ya taifa lake. Na maneno yake katika kuepusha hilo yalikuwa "Huwezi kutuchagulia marafiki".

Symbolbild Deutschland Tansania
Gari yenye kuonesha nembo ya ishara ya ushirikiano kati ya Ujerumani na TanzaniaPicha: picture-alliance/dpa/Michael Kappeler

Katika kusimamia kauli yake hiyo aliagizia Wajerumani wote waondoke nchini mwake, isipokuwa wafanyakazi wa Ubalozi.

Wakati mwingine mgumu

Awamu nyingine ngumu katika uhusiano wa Ujerumani na Tanzania ilikuwa mwaka 2013. Kipindi hicho Tanzania ilikataa kumpokea aliyeteuliwa kuwa balozi wa Ujerumani nchini humo, pasipo kutaja sababu yoyote, ingawaje sheria za kimataifa zinaruhusu nchi yenye kupokea balozi kuwa na haki ya kufanya hivyo. Wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani iliulezea uamuzi huo kuwa usioeleweka. Watanzania wanaitambua Ujerumani katika ujenzi wa demokrasia ya taifa lao.

Umuhimu wa ziara ya Gauck

Ziara ya siku tano ya rais Gauck inakoja baada ya kushindikana kwa ile ya mtangulizi wake Christian Wulff ambae alishindwa kukamilisha ziara yake nchini Tanzania baada ya kujiuzulu siku chache kabla ya kukamilisha ziara kama hiyo. Ziara hiyo ina umuhimu wa kukuza ushirikiano wa kibiashara,kiuchumi na kisiasa baina ya mataifa yote mawili. Hata hivyo mchambuzi na mtaalamu wa masuala ya siasa kutoka Tanzania Profesa Mwesiga Baregu,amesema uhusiano wa kibiashara kati ya matiafa hayo mawili bado mdogo, lakini unakuwa. Anasema wawekezaji wa Kijerumani wanaonesha kuvutiwa na nia ya uwekezaji katika rasilimali mpya ya gesi nchini humo.

Rais Gauck akipokea shada la mauwa
Rais Gauck na mkewe wakipokea mashada ya mauwaPicha: picture-alliance/dpa/Wolfgang Kumm

Naye Richard Shaba wa Konrad Adenauer anasema umuhimu wa nishati mbadala nchini Tanzania unaweza kuunganisha mataifa hayo mawili katika mipango ya siku za usoni. Ameongeza kwamba Ujerumani ina ujuzi mkubwa katika sekta hiyo yenye kujumuisha nishati itokanayo na jua, upepo na maji, nishati ambazo vyanzo vyake vinapatikana kwa wingi nchini Tanzania

Mwandishi: Sudi Mnette/ DW

Mhariri:Mohammed Abdul-rahman