1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Gauck kukutana na Obama

Admin.WagnerD7 Oktoba 2015

Rais wa Ujerumani Joachim Gauck amezitaka Marekani na Ujerumani ziimarishe uhusiano baina yao hasa wakati huu ambapo dunia inakabiliwa na vita na ugaidi.

https://p.dw.com/p/1Gk4V
Rais wa Ujerumani Joachim Gauck kwenye kengele ya uhuru ,Philadelphia
Rais wa Ujerumani Joachim Gauck kwenye kengele ya uhuru ,PhiladelphiaPicha: picture-alliance/dpa

Bwana Gauck amesema ikiwa watu ni wakweli watakubali kwamba uhusiano baina ya Marekani na Ulaya haukushughulikiwa kwa uangalifu wa kiasi kilichokuwa cha lazima.

Akihutubia kwenye chuo kikuu cha Pennysylvania mjini Philadelphia Gauck alisisitiza kuwa mfungamano na Marekani ndiyo nguzo ya uwepo wa Ulaya huru, ikiwa pamoja na Ujerumani.

Kiongozi huyo wa Ujerumani ametilia maanani kwamba mfungamano wa kijeshi wa NATO sasa unakabiliwa na changamoto mpya,kama vile ugaidi ,kuibuka kwa madikteta,kuanguka kwa mataifa na sehemu zinazotumbukia katika vurumai.

Rais wa Ujerumani anaetarajia kukutana na Rais Obama baadae leo pia ameitaka Marekani ijihusishe zaidi na mgogoro wa wakimbizi unaolikabili bara la Ulaya. Amesema mjadala juu ya mgogoro wa wakimbizi haupaswi kuwa suala la Ulaya peke yake, na ametamka wazi kwamba kujiingiza kwa Marekani katika Mashariki ya Kati kumechangia kuleta vurumai iliyowafanya maalfu ya watu waikimbie sehemu hiyo.

Hii ni mara ya kwanza,baada ya miaka 18,kupita kwa Rais wa Ujerumani kukutana na Rais wa Marekani kwenye Ikulu ya nchi hiyo. Rais Gauck pia atakutana na Makamu wa Rais, Joe Biden na Waziri wa mambo ya nje John Kerry.

Marekani iyafuate maadili inayoyahubiri

Rais wa Ujerumani aliuchagua mji wa Philadelphia kuwa kituo cha kwanza cha ziara yake ya Marekani kutokana na umaarufu wa mji huo kuwa chimbuko la demokrasia nchini Marekani. Ni katika mji huo ambako waanzilishi wa taifa la Marekani waliliandika tamko la uhuru.

Gauck in Washington
Picha: picture-alliance/dpa

Katika hotuba yake Bwana Gauck pia aliitaka Marekani irejeshe imani iliyoipoteza kutokana na kashfa ya udukuzi wa simu za wananchi wa Ujerumani uliofanywa na idara ya Marekani ya usalama wa taifa. Ameitaka Marekani iyafuate maadili ambayo yenyewe inayahubiri.

Mwandishi:Mtullya abdu/ZA,DPA,

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman