1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa shirikisho Horst Köhler ziarani nchini India

Oumilkher Hamidou2 Februari 2010

Rais Köhler aisifu India kuwa "nyota inayong'ara"katika siasa ya dunia

https://p.dw.com/p/LpkH
Rais wa shirikisho atembelea kumbusho la Mahatma Gandhi mjini New DelhiPicha: AP

Rais wa shirikisho la jamhuri ya Ujerumani Horst Köhler,akianza ziara yake rasmi nchini India, ametoa mwito wa kuanzishwa mkakati wa pamoja kukabiliana na changamoto ya utandawazi.Rais Köhler ameitaja India na wananchi wake zaidi ya bilioni moja kuwa ni " dola linaloibuka kuwa kuu".

""Tusifikirie kwamba sisi wa kutoka nchi za magharibi ndio peke yetu tunaodhibiti hekma"-matamshi hayo ameyatoa rais wa shirikisho Horst Köhler alipotembelea mahala alikochomwa moto Mahatma Gandhi mjini New-Delhi.Mwanaharakati huyo wa amani,aliyepigania uhuru wa India hadi kuundwa taifa hilo miaka 62 iliyopita,ameuliwa na mfuasi wa itikadi kali wa kibaniani.Rais Köhler na mkewe Eva Luise walilizunguka kumbusho hilo na kumwagia mauwa bamba la marmar nyeusi lililopambwa kwa mauwa.Kabla ya hapo rais Kohler alilahikiwa kwa hishma za kijeshi na rais Pratibha Devisingh Patil wa india.

Waziri mkuu Manmohan Singh na mawaziri kadhaa wa serikali yake walishiriki pia katika sherehe hiyo.

Indien Deutschland Horst Köhler in New Delhi Pratibha Patil
Rais Köhler anaamkiana na rais Pratibha Patil wa India na waziri mkuu Manmohan Singh (kutoka kushoto)Picha: AP

Akizungumza na waandishi habari rais Köhler amesema baadae amekuja ili kudhihirisha umuhimu anaotoa kwa India.India ni "nyota inayong'ara katika siasa ya dunia".Anataraji uhusiano kati ya Ujerumani na India utazidi kuimarishwa.Rais wa shirikisho Horst Köhler ameendelea kusema:

"India ni mshirika wa kimkakati kwetu na zaidi ya hayo ni rafiki pia.Na tunaamini urafiki huu na ushirikiano huu wa kimkakati,kwa pande zote mbili,kwa Ujerumani na hasa kwa India,una fursa kubwa zaidi ya kuzidi kuimarishwa kwa masilahi ya nchi zetu mbili na hasa katika sekta ya kiuchumi,uwekezaji,na hata kuchangia hapa hapa nchini India kuupiga vita umaskini."

Kiini cha ziara ya siku sabaa ya rais wa shirikisho la jamhuri ya Ujerumani katika bara Hindi ni kutaka kuimarisha uhusiano wa kiuchumi kati ya Ujerumani na India.Akizungumza mbele ya wawakilishi wa mashirika ya kiuchumi na halmshauri ya biashara ya Ujerumani na India,rais Köhler amesema ingawa utandawazi unasaidia kuchochea ukuaji wa kiuchumi na kwa namna hiyo kuzidisha neema,hata hivyo neema hiyo inabidi izinufaishe pande zote sawa bin sawa.Rais wa shirikisho amesisitiza kila la kufanywa lifanywe ili kuepusha watu wasijihisi wananyimwa neema hiyo.

Mbali na uhusiano wa kiuchumi rais Horst Köhler anapanga pia kuzungumzia umuhimu wa kuimarishwa maingiliano katika sekta ya utamaduni na sayansi.

Baada ya kuutembelea mji mkuu New Delhi,rais wa shirikisho Horst Köhler anapanga pia kufika katika mji mkuu wa kiuchumi Mombai,mji wa Pune kunakotengenezwa magari na kuyatembelea pia maeneo ya mashambani ya India kabla ya kuondoka jumapili ijayo kuelekea Korea ya kusini.

Mwandishi:Bettina Marx(DW-ZPR)/ Hamidou Oummilkheir

Imepitiwa na:Abdul-Rahman