Rais wa mpito wa mali yuko salama baada ya shambulio | Matukio ya Afrika | DW | 20.07.2021
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Rais wa mpito wa mali yuko salama baada ya shambulio

Rais wa mpito wa Mali Assimi Goïta ameponea chupuchupu kuuawa kwa kisu. Watu wawili walijaribu kumshambulia wakati wa ibada ya Eid lakini hawakufanikiwa.

Shambulizi hilo lilitokea kwenye Msikiti Mkuu wa Bamako, ambako kiongozi huyo alihudhuria sala ya siku Kuu ya iddi. Walipoulizwa na shirika la habari la AFP juu ya kitendo hicho kama ni jaribio la mauaji ya rais, wasaidizi wake wamejibu, bila shaka yoyote rais alilengwa.

Maafisa wamelezea kuwa uchunguzi umeendeshwa na kubaini kwamba rais Assimi Goita yuko salama na mzima wa afya. Akiwa katika eneo la tukio, Waziri wa Masuala ya Kidini, Mamadou Koné, aliliambia shirika la habari la AFP kwamba mshambuliaji alidhibitiwa kabla ya kutekeleza uhalifu huo.

Kwa upande wake Latus Touré, msimamizi wa Msikiti Mkuu wa Bamako,alithibitisha tukio hilo akisema kuwa lilijiri baada ya sala na mahubiri ya imamu, wakati imamu alikuwa akijianda kwenda kuchinja kondoo wake, ndipo kijana huyo alijaribu kumchoma Assimi Goïta mgongoni, lakini mtu mwingine ndiye alijeruhiwa.

Usalama wa Mali bado kwenye njiapanda

Goita alikuwa ameongoza mapinduzi ya mwezi Agosti, wakati yeye na maafisa wengine wa jeshi walipomwondoa mamlakani rais aliyechaguliwa Ibrahim Boubacar Keita baada ya maandamano ya wiki kadhaa juu ya ufisadi na mzozo wa muda mrefu wa wanajihadi.

Mali imeshuhudia majaribio mawili ya mapinduzi katika kipindi cha mwaka mmoja. Jaribio la kwanza lilifanyika mwezi wa Agosti 2020 na kisha Mei mwaka huu, majaribio ambayo yaliongozwa na kanali Assimi Goïta, ambaye tangu wakati huo ni rais wa mpito.