1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ndoto ya Marekani yawezekana Afrika

27 Julai 2015

Ziara ya rais wa Marekani Barack Obama barani Afrika na hujuma za Uturuki dhidi ya wafuasi wa itikadi kali wa dola ya kiislamu IS na wanamgambo wa kikurdi PKK ni miongoni mwa mada zilizohanikiza magazetini.

https://p.dw.com/p/1G58X
Äthiopien Barack Obama Hailemariam Desalegn PK
Picha: Getty Images/AFP/de Souza

Tuanzie lakini Mashariki mwa Afrika ambako rais wa Marekani anaendelea na ziara yake nchini Ethiopia baada ya kuitembelea hapo awali nchi alikozaliwa babake, Kenya. Gazeti la "Neue Osnabrücker" linaandika:"Ratiba ya ziara ya rais wa Marekani barani Afrika imepangwa kwa hikma.Jana jumapili amefika Ethiopia ambako njia,ghala ya kuhifadhia nafaka,na hata jengo la fahari la Umoja wa Afrika katika mji mkuu Addid Abeba,yamegharimiwa kikamilifu na China.Dola hilo kuu la Asia limegeuka ndugu mkubwa wa Afrika;halikosoi uvunjwaji wa haki za binaadam,kama zinavyofanya nchi za magharibi.Madola ya zamani ya ukoloni barani Ulaya na hata Marekani yameitambua hali hiyo .Huo ndio umuhimu wa ziara fupi ya rais Obama jumamosi iliyopita nchini Kenya alikokumbusha mizizi yake ya kiafrika na uhusiano kati ya Marekani na Afrika.Anaiangalia Afrika kuwa ni bara la kunawiri na sio la kudhoofika-kuambatana na ndoto ya kimarekani...

Masilahi ya Marekani ndio kipa umbele

Gazeti la "Rheinpfalz " linaiangalia ziara ya Obama barani Afrika kwa jicho jengine kabisa. Gazeti linaandika:"Mataifa ya Afrika yanapewa umuhimu na Marekani pale tu yanapokidhi masilahi ya usalama ya dola hilo kuu.Na hilo Obama ambae babaake anatokea Kenya hawezi kulibadilisha.Mataifa yanayojiunga na mpambano dhidi ya ugaidi,yanaweza kutegemea bila ya wasi wasi,msaada wa Marekani,au kaka mkubwa.Bila ya shaka Obama anautambua unafiki wa siasa yake,ndio maana ametafuta mbinu nyengine bila ya kuwakera washirika wake.Msimamo wa Kenya dhidi ya mashoga ni mojawapo ya mbinu hizo.Kwa namna hiyo rais wa Marekani ataendelea kuubainishia ulimwengu wa magharibi msimamo wake wa kupigania maadili ya kiutu.

Uturuki yanyunzia mafuta katika cheche za moto

Mada yetu ya mwisho magazetini inahusu hujuma za ndege za kivita za Uturuki katika viwanja viwili vya mapigano; dhidi ya wafuasi wa itikadi kali wa dola ya kiislamu IS na dhidi ya wanamgambo wa kikurdi - PKK. Gazeti la "Thüringische Landeszeitung" linaandika:" Erdogan anaitumia fursa iliyojitokeza kuvunja nguvu matumaini ya wakurd ya kuwa na taifa lao.Kwasababu wafuasi wa itikadi kali wa dola ya kiislam-IS hawajawahi kuangaliwa kuwa ni maadui wa kweli-wakurd lakini tangu zamani wanajulikana kuwa maadui wakubwa wa Uturuki.Kila shambulio linalotokea Uturuki,hata bila ya kuchunguzwa hutajwa limefanywa na PKK na wanaamgambo wa kikurd nchini Syria na Irak wanaangaliwa kuwa ni kitisho kwa Uturuki.Yadhihirika kana kwamba Erdogan hataki tena kuingia katika madaftari ya historia kama malaika wa amani-ananyunnyizia mafuta katika cheche za moto-na Uturuki ndio itakayoungua.Nchi ambayo haina utulivu wa ndani,haikawii kugeuka lengo la wafuasi wa itikadi kali wa IS.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri:Josephat Charo