1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa China ziarani Marekani

18 Januari 2011

Rais wa China anafanya ziara rasmi Marekani, wakati uhusiano kati ya nchi hizo mbili ukijikuta katika hali ya mvutano na Marekani ikikumbana na athari za mzozo wa kiuchumi, huku China ikizidi kuwa na sauti duniani.

https://p.dw.com/p/QtJp
Chinese President Hu Jintao waves while arriving in the Ural Mountains city of Yekaterinburg, Russia, Sunday, June 14, 2009. Hu Jintao arrived in Russia for the first summit of leaders of Brazil, Russia, India and China, the so-called BRIC group of rapidly developing economies.(AP Photo/Mikhail Metzel)
Rais wa China, Hu JintaoPicha: AP

Rais Hu Jintao atapokewa kwa heshima kubwa na Rais Barack Obama atakapowasili baadae leo hii mjini Washington, lakini masuala kuhusu haki za binadamu, thamani ya sarafu ya China, Yuan, na mzozio juu ya Korea ya Kaskazini, yanazidisha mvutano katika uhusiano wa mataifa hayo mawili. Kwa maoni ya wadadisi, ziara ya Rais Hu Jintao ni ziara muhimu kabisa kupata kufanywa na kiongozi wa China tangu miaka 30, nchi hiyo ikizidi kuwa na ushawishi wa kijeshi na kidiplomasia, huku uchumi wake ukichukua nafasi ya pili duniani.

Bila shaka, wawekezaji watakuwa wakingojea ishara za kupunguza mvutano kati ya nchi hizo mbili wakati wa ziara hii mjini Washington. Lakini wadadisi wanaonya kutotazamia zaidi ya maneno ya kirafiki na mikataba ya kibishara yenye thamani ya mabilioni ya dola.

A bank clerk counts renminbi banknotes at a bank outlet in Hefei in central China's Anhui province Tuesday Nov. 17, 2009. China's Commerce Ministry rejected calls for the yuan to appreciate on Monday. Photo via Newscom Picture-Alliance Renminbi (chin. 人民幣 / 人民币, Rénmínbì „Volkswährung“) ist die Währung der Volksrepublik China und wird von der Chinesischen Volksbank herausgegeben. Die internationale Abkürzung nach ISO 4217 ist CNY, in China wird RMB verwendet, das Symbol ist ¥. Die Einheiten der Währung sind Yuán (元, formell: 圓 / 圆), Jiǎo (角) und Fēn (分). Ein Yuan entspricht 10 Jiao bzw. 100 Fen. Umgangssprachlich wird anstatt Yuán häufig Kuài (塊 / 块, Stück) und anstatt Jiǎo wird Máo (毛, Haar) verwendet.
Karani wa benki akihesabu noti za YuanPicha: picture-alliance / Newscom

Mada kuu katika ajenda ya mazungumzo yao ni biashara na thamani ya sarafu ya Yuan iliyoongezeka kwa takriban asilimia 3.5 dhidi ya dola ya Marekani, tangu China kuacha kuiambatanisha sarafu yake na dola mnamo mwezi wa Juni. Hicho ni kiwango kidogo sana kulinganishwa na kile kinachodaiwa na wakosoaji wa Marekani.

Lakini msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya China, Hong Lei, amesema kwamba ukosefu wa uwiano katika biashara ya China na Marekani hausababishwi na sera ya kuzuia thamani ya sarafu ya Yuan kupanda juu.

Siku ya Jumatatu, kundi la wabunge wa Marekani wamependekeza mswada wa sheria ili China iweze kuadhibiwa iwapo itaendelea kuzuia thamani ya sarafu yake kupanda na hivyo kunufaika kibiashara katika masoko ya dunia. Lakini haitokuwa rahisi kupitisha sheria kama hiyo, kwani serikali inapendelea kuwa na majadiliano. Hata viongozi wa Chama cha Republikan hapo awali walipinga pendekezo la sheria hiyo.

Kwa maoni ya baadhi ya wadadisi, kufuatia mivutano ya mwaka jana kuhusu sarafu, biashara, Taiwan, Korea ya Kaskazini na haki za binadamu, uhusiano wa Marekani na China iliyoibuka kuwa na nguvu kiuchumi, daima utakuwa wa tahadhari na mashaka.

Mwandishi: Martin,Prema/RTRE/AFPE

Mpitiaji: Miraji Othman