1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa China Xi na kongamano la kiuchumi la St.Petersburg

Oumilkheir Hamidou
7 Juni 2019

Rais wa China Xi Jinping anahudhuria kongamano la kiuchumi la Urusi mjini St.Petersburg akiwa mgeni wa heshima wa rais Putin katika wakati ambapo nchi hizo mbili zinajenga nguzo ya pamoja dhidi ya vishindo vya Marekani.

https://p.dw.com/p/3K0qa
Russland Moskau | Präsidenten Wladimir Putin & Xi Jinping, China
Picha: Reuters/E. Novozhenina

 

Rais wa China Xi Jinping amewasili Moscow tangu jumatano iliyopita kwa ziara ya siku tatu  kwa lengo la kumtembelea rais Vladimir Putin aliyemtaja kuwa "rafiki yake mkubwa."

Akikamilisha ziara yake hiyo rais Xi na mwenyeji wake rais Putin wanapanga kuhudhuria kwa pamoja kikao cha hadhara cha kongamano la kiuchumi linaloitishwa kila mwaka mjini St.Petersburg, ambapo viongozi wa mjini Moscow wanataraji kuwavutia wawekezaji  licha ya hali ambayo si imara ya kiuchumi.

Rais Xi anapanga kuzungumzia fikra kuhusu maendeleo endelevu na ushirikiano kati ya nchi tofauti atakapohutubia kongamano hilo.

Kongamano la mwaka huu wa 2019 linatoa picha ya jinsi ulimwengu ulivyogawika " anasema Chris Weafer, mtaalam wa shirika la ushauri .

Ziara ya rais wa jamhuri ya China nchini Urusi inafanyika miaka mitano tangu Urusi ilipoivamia raasi ya Ukraine ya Crimea na kusababisha mfarakano mkubwa pamoja na nchi za magharibi. Imesadifu pia wakati viongozi wa mjini Beijing wanajikuta katika vita vya kibiashara pamoja na Marekani.

Rais Xi na mwenyeji wake rais Putin wakitembelea bustani ya wanyama mjini Moscow
Rais Xi na mwenyeji wake rais Putin wakitembelea bustani ya wanyama mjini MoscowPicha: picture-alliance/dpa/Tass/A. Vilf

Jukumu la pamoja la Urusi na China kudhamini mkakiati jumla wa utulivu ulimwenguni

Msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje ya China, Gen Shuang anazungumzia azma ya  China na Urusi ya kuzidi kuimarisha ushirikianao wa kimkakati na hali ya kuaminiana kati yao:"Wakiwa wanachama wa kudumu wa baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, China na Urusi wana jukumu la pamoja na wanalazimika kudhamini mkakati jumla wa utulivu. China na Urusi hawatafuti faida za kibinafsi kwa kuamua kushirikiana kulinda mkakati jumla wa utuilivu. Uhusiano kati ya nchi kuu ni muhimu kwa mkakati jumla wa utulivu.Tunadhamiria kuendeleza ushirikiano, bila ya mivutano na malumbano lakini kwa kuheshimiana na kwa faida ya kila upande."

Rais wa Xi amefuatana na ujumbe wa watu elfu moja katika ziara yake hii ya mjini Moscow. Mikataba kadhaa ya kibiashara imetiwa saini ,katika sekta yaa mawasiliano, gesi na sekta nyenginezo.

 

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/AFP

Mhariri: Mohammed Khelef