Rais wa China Xi Jinping ziarani Marekani | Matukio ya Kisiasa | DW | 25.09.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Rais wa China Xi Jinping ziarani Marekani

Rais Barack Obama wa Marekani amemkaribisha ikulu ya White House kiongozi mwenzake wa China Xi Jinping,katika wakati ambapo viongozi hao wa madola makuu wanajaribu kupunguza mivutano kati ya nchi zao.

Rais Barack Obama na rais Xi Jinping wakiangalia gwaride la jeshi katika abustani ya White House

Rais Barack Obama na rais Xi Jinping wakiangalia gwaride la jeshi katika abustani ya White House

Ili kushadidia cheo cha China mjini Washington,mizinga 21 imefyetuliwa kumkaribisha rais Xi pamoja na kuandaliwa baadae karamu ya chakula cha usiku-hishma na sherehe zitakazomsaidia pia rais Xi nyumbani mjini Beijing.

Ziara hii ya kwanza rasmi kuwahi kufanywa na rais Xi nchini Marekani,inatokea wakati uchumi wa jamhuri ya umma wa China unaanza kudhoofika katika masoko ya dunia na katika wakati ambapo Washington na Beijing zinakumbwa na matatizo kadhaa kuanzia hujuma za mitandao hadi kufikia mvutano wa China na majirani zake katika bahari ya kusini.

Lakini ikulu ya Marekani inataraji mkutano huu wa kilele utasaidia kuleta maridhiano angalau katika suala moja: Mabadiliko ya tabia nchi.

Rais Xi kutangaza mpango ziada kupunguza moshi wa sumu

Xi Jinping und Barack Obama in Washington

Rais Obama akiamkiana na rais Xi

Akizungumza na waandishi habari katika bustani ya ikulu ya Marekani,rais Barack Obama alisisitiza juu ya umuhimu wa kushirikiana madola haya mawili makuu ya kiuchumi duniani na kusema:"Ushirikiano wetu katika kuzidisha biashara,kuimarisha hali jumla ya kiuchumi ,kupambana na mabadailiko ya tabia nchi na kuzuwia kuenea silaha za kinuklea,umedhihirisha kwamba ikiwa Marekani na China zinashirikiana,mataifa haya mawili na ulimwengu kwa jumla unaneemeka na kuzidi kuwa salama."

Rais Barack Obama amemwambia mgeni wake wa kutoka Beijing anaamini wanaweza kuzungumzia kwa uwazi kabisa tofauti zao,akishadidia hasa kuhusu umuhimu wa kuheshimiwa haki za binaadam.

Baada ya mazungumzo katika bustani ya ikulu viongozi hao wawili wameongozana kwa mazungumzo ya pande mbili

Rais Xi Jinping anatazamiwa kutangaza mpango ziada wa nchi yake katika juhudi za kupunguza moshi wa sumu unaotoka viwandani,mpango utakaoanza kufanya kazi mwaka 2017.

Uhusiano wa pande mbili mazungumzoni

Xi Jinping und Barack Obama in Washington

Rais Obama akaikutana na rais Xi katika nyumba ya wageni ya Blair House

Mbali na mada ya mabadiliko ya tabia nchi,marais Obama na Xi wanatazamiwa kuzungumzia jinsi ya kuimarisha ushirikiano wao katika kuzuwia miradi ya nuklea ya Iran na Korea ya kaskazini na uhusiano kati ya nchi zao.

Viongozi hawa wawili walikutana kwa mara ya kwanza jana huko White House kwa karamu isiyo rasmi ya chakula cha usiku ,ambapo rais Obama na mgeni wake wa kutoka Beijing walibadilishana tai pamoja na kutembea katika mtaa wa West Ring kupitia njia mashuhuri ya Pennsylvania hadi katika nyumba wanakofikia wageni wa rais,Blair House.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP/Reuters

Mhariri.Yusuf Saumu

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com