1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa Catalonia ataka mazungumzo na Madrid

Sylvia Mwehozi
11 Oktoba 2017

Usiku wa Jumanne, kiongozi wa Catalonia Carles Puigdemont amelieleza bunge la mkoa wake kwamba Catalonia itatangaza uhuru wake lakini anatoa muda zaidi kwa ajili ya majadiliano na serikali kuu ya Madrid.

https://p.dw.com/p/2lc52
Spanien Parlament in Barcelona Carles Puigdemont
Picha: Getty Images/D. Ramos

Baada ya hotuba yake, viongozi wa mkoa huo wanaounga mkono kujitenga wamesaini kile walichokiita ni hati ya kujipatia uhuru kutoka Uhispania lakini rais wake anasema utekelezaji wake utachelewa kwa wiki kadhaa ili kuyapatia nafasi majadiliano.

Katika hotuba yake iliyokuwa ikingojewa kwa shauku, rais Puigdemont amesema ushindi mkubwa wa kura ya maoni ya oktoba mosi umeipatia serikali yake misingi ya kutekeleza dhamira yake ya muda mrefu ya kujitenga na Uhispania.

Lakini akapendekeza kwamba bunge la mkoa "lisogeze mbele utekelezaji wa matokeo ya kura ya maoni ili kuanza majadiliano, si kwasababu tu ya kupunguza mvutano lakini pia kufikia makubaliano ya suluhisho la kusonga mbele na madai ya watu wa Catalonia." "Tunapaswa kusikiliza sauti za wale ambao wameomba kuyapatia nafasi majadiliano na taifa la Uhispania", amesema Puigdemont.

Soraya Saéz spanische Vize-Ministerpräsidentin
Naibu waziri mkuu wa Uhispania Soraya Saéz de SantamariaPicha: imago/Agencia EFE/A. Diaz

Serikali kuu mjini Madrid ilitoa kauli mara moja ikisema kuwa haikubaliani na suala la kujitangazia uhuru na kwamba haitambui kura ya maoni na matokeo yake kama kitu kilichokuwa halali. Naibu waziri mkuu Soraya Saenz de Santamaria amesema kikao cha dharura cha baraza la mawaziri kimeitishwa leo Jumatano, wakati huo akimuelezea kiongozi wa Catalonia kuwa mtu asiyefahamu wapi alipo, anakokwenda na akina nani anakwenda nao.

Saenz de Santamaria ameongeza kuwa serikali haiwezi kukubaliana na uhalali wa kura ya maoni ya Catalonia kwasababu ilikatiliwa na mahakama ya kikatiba au matokeo ya kura hiyo kwamba yalikuwa ni kinyume na sheria na batili.

Anasema kiongozi wake Puigdemont ameiweka Catalonia katika hali ya wasiwasi kuwahi kushuhudiwa. Moja ya hatua zinazoweza kuchukuliwa katika kikao cha leo cha baraza la mawaziri itakuwa ni kutumia kifungo cha 155 cha katiba ambacho kinaruhusu serikali kuu kuchukua udhibiti mzima au baadhi ya mikoa yake 17 ikiwa haitii matakwa ya kisheria.

Spanien Parlament in Barcelona Carles Puigdemont
Wabunge wa Catalonia wakimpigia makofi rais Carles Puigdemont Picha: Getty Images/D. Ramos

Hili litaanza na mkutano wa baraza la mawaziri kisha kuitishwa kwa seneti litakalopitisha hatua hizo. Kiongozi wa Catalonia anaweza kukamatwa na pia kuhojiwa mahakamani.

Kufuatia hotuba yake kiongozi huyo amekuwa wa kwanza kutia saini hati ya uhuru na kisha kufuatiwa na wabunge wengine kadhaa wanaotaka kujitenga, ingawa haijafahamika ikiwa hati hiyo ina misingi ya kisheria.

Puigdemont amerejerea katika hotuba yake kuikosoa serikali ya Uhispania namna ilivyopinga kura hiyo ya maoni na vurugu za polisi ambazo zilisababisha mamia ya watu kujeruhiwa siku hiyo ya kura, na kueleza kwamba Wacatalonia hawana nia mbaya na Uhispania ila wanataka pande zote mbili kuelewana.

Kiongozi wa upinzani Ines Arrimas ameikosoa hotuba ya kiongozi huyo akisema hayo ni mapinduzi kwasababu hakuna mtu anatambua matokeo ya kura na hakuna mtu yeyote barani Ulaya anayeunga mkono harakati hizo.

Watu karibu milioni 2.3 wa Catalonia sawa na asilimia 43 walipiga kura oktoba mosi. Mamlaka za kimkoa zinasema asilimia 90 waliunga mkono kujitenga na hivyo kutangaza kwamba matokeo yalikuwa ya halali. Utafiti wa hivi karibuni hata hivyo unaonyesha kwamba Wacatalonia wamegawanyika juu ya suala hilo la kujitenga.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/AP