1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa Armenia aitisha mazungumzo kutatua mzozo wa kisiasa

Caro Robi
2 Mei 2018

Armenia imekumbwa na mzozo wa kisiasa tangu mwezi Aprili kufuatia Serzh Sargisyan kuteuliwa kuwa Waziri mkuu na baaadaye kuondolewa kufuatia shinikizo la umma.

https://p.dw.com/p/2x2p0
Armenien Opposition Protest in Jerewan
Picha: Reuters/G. Garanich

Rais wa Armenia Armen Sarkissian ametoa wito wa mazungumzo  wiki hii, ili  kutatua mzozo wa kisiasa ambao umeikumba nchi hiyo ndogo iliyokuwa ya Kisovieti tangu yalipoitishwa maandamano ya umma ambayo hatimaye yamemuondoa madarakani Waziri mkuu Serzh Sargisyan.

Taarifa kutoka ofisi ya Rais imesema Rais Sarkissian anasikitishwa na kuendelea kwa mzozo wa kisiasa licha ya kila mmoja kuzungumzia kuhusu hatari ya kuendelea kwa mgogoro kuathiri mustakabali wa siku za usoni wa Armenia.

Raia wazidi kuishinikiza serikali

Maelfu ya Warmenia wamekusanyika katika mji mkuu wa nchi hiyo Yerevan, wakifunga barabara na majengo ya serikali kuandamana ili kuonesha hasira zao kufuatia chama tawala kupinga azma ya Nikol Pashinyan kuwa waziri mkuu.

Armenien Nikol Pashinyan Opposition
Kiongozi wa upinzani Nikol PashinyanPicha: picture-alliance/dpa/TASS/A. Geodakyan

Kiongozi huyo wa upinzani amewataka Warmenia kuendelea kuandamana dhidi ya chama tawala cha Republican baada ya uteuzi wake wa kuwa waziri mkuu kupingwa bungeni jana.

Bunge lilipiga kura 55 dhidi ya 45 kumpinga Pashinyan kuchukua wadhifa huo. Chama hicho cha Republican kinachoongozwa na Serzh Sarkisyan ndicho kilicho na idadi kubwa ya wabunge bungeni.

Bunge hilo litakuatana kwa kikao maalumu tarehe 8 mwezi huu kumchagua waziri mkuu mpya baada ya jaribio la jana kushindwa.

Pashinyan amewasilisha tena azma yake ya kuteuliwa kuwa waziri mkuu baada ya jaribio la kwanza kushindwa bungeni akiahidi kuendelea na uasi wa kiraia, kupitia maandamano. Iwapo bunge litashindwa kwa mara ya pili kumteua waziri mkuu, litavunjwa na chaguzi za mapema kuitishwa.

Viongozi wa serikali wataka kuumaliza mzozo

Kaimu waziri mkuu Kerna Karapetyan amewataka vigogo wa kisiasa nchini humo kusogea kwa meza ya mazungumzo ili kuutatua mzozo huo wa kisiasa ambao umeighubika nchi hiyo kwa takriban majuma matatu sasa tangu Pashinyan kuyaongoza maandamano ya umma kumuondoa madarakani Sargasiyan wiki iliyopita ambaye aliteuliwa na bunge kuwa waziri mkuu bada ya kuhudumu kama rais kwa miaka kumi iliyopita.

Armenien Proteste in Eriwan
Maelfu ya watu wakiandamana mjini YerevanPicha: picture-alliance/TASS/dpa/A. Geodakyan

Kiongozi huyo wa upinzani ameionya serikali dhidi ya kuyatuma majeshi kukabiliana na maelfu ya waandamanaji waliomiminika katika barabara za mji mkuu Yerevan na kwingineko nchini humo kuishinikiza serikali kuondoka madarakani na kumruhusu Pashinyan kuwa waziri mkuu.

Pashinyan amesema mzozo uliopo hauwezi kutatuliwa kwa nguvu za kijeshi akiongeza kuwa chama tawala kimejiangamiza chenyewe kwa kupinga azma yake ya kuingoza Armenia.

Waandamanaji wameziba barabara ya kuelekea katika uwanja wa ndege, barabara kuu za mji wa Yereven, vituo vya treni na kukwamisha shughuli katika majengo ya serikali. Pashinyan amewahimiza wafuasi wake kujiendesha kwa njia ya amani wakati wa maandamano.

Mwandishi: Caro Robi/afp/Reuters/dpa/ap

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman