1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Trump anavyofunika kombe kuhusu mkasa wa Khashoggi

Oumilkheir Hamidou
17 Oktoba 2018

Mkasa wa kupotea kwa mwandishi habari Jamal Khashoggi na jinsi rais wa Marekani Donald Trump anavyofunika kombe ni kati ya mada kuu ambazo zimeangaziwa na wahariri magazetini

https://p.dw.com/p/36gDh
Saudi-Arabien Riad Ankunft US-Außenminister Mike Pompeo
Picha: Getty Images/AFP/L. Millis

Mkasa wa Jamal Khashoggi na jinsi rais wa Marekani Donald Trump anavyofunika kombe, siasa ya nje ya Ujerumani na jinsi chama cha Social Democratic, SPD wanavyoshusha pumzi kuelekea uchaguzi wa bunge la ulaya ni miongoni mwa mada magazetini.

Tunaanza na kisa cha mkosoaji mkubwa wa mwanamfalme wa Saudi Arabia, Mohammed bin Salman, mwandishi habari Jamal Khashoggi. Uturuki imekamilisha uchunguzi wake katika ubalozi mdogo wa Saudi Arabia mjini Istanbul na imeahidi kuipekua pia nyumba ya balozi mwenyewe hasa. Wahka mjini Ryadh ambako waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Mike Pompeo alikutana na mfalme Salman na pia  mwanawe, mrithi wake, Mohammed bin Salman. Gazeti la "Badische Zeitung" linaandika: "Kwamba baba mkongwe anamtetea mwanawe wa kiume, inaingia akilini. Haingiii akilini lakini hata kidogo pale rais wa Marekani Donald Trump anaposema anaamini ni kweli yaliyosemwa na mfalme Salman kwamba mwanawe hahusiki na kwamba kuuliwa kikatili Khashoggi ni ajali ya kuhuzunisha.

Jumuiya ya kimataifa inabidi kujitenga na wanaotoa amri ya kuuwa nchini Saudi Arabia kama viongozi kadhaa wa makampuni ya kimataifa walivyofanya kwa kukataa kushiriki katika mkutano wa kiuchumi mjini Ryadh. La sivyo kijana huyo mrithi wa kiti cha ufalme atazidi kupata nguvu na kuutafsiri woga wa nchi za magharibi kama ridhaa ya kuendelea na visa vyake dhidi ya wale wote wenye maoni tofauti na yake."

Marekani na pia Ulaya waaminike vipi

Gazeti la "Freie Presse "linaonya: "Yaliyomfika Khashoggi si kisa ni kashfa. Kwa jinsi gani Marekani au hata nchi za Ulaya wataweza kuaminika siku za mbele, watakapotaka kuzungumzia tena kuhusu haki za za binaadam au demokrasia?"

Siasa ya nje ya Ujerumani imemulikwa pia magazetini. Gazeti la "Stuttgarter Nachrichten" linaandika: "Kizungumkuti kinaendelea kwa karibu mwaka mmoja na nusu sasa; kampeni za uchaguzi, uchaguzi mkuu, usumbufu wa kuunda serikali na tangu wakati huo mivutano isiyokwisha ndani ya serikali kuu ya muungano. Kinachoshuhudiwa katika uwanja wa kisiasa mjini Berlin ni ushahidi wa mwanya mpana unaoigawa jamii na kishindo cha kutojua vipi kuisawazisha hali hiyo. Kila mmoja anavuta upande wake wakiamini labda kwa namna hiyo matatizo yatatoweka. "

SPD washusha pumzi

Mada yetu ya mwisho magazetini inakimulika chama cha SPD ambacho baada ya zilzala kinaonyesha kushusha pumzi. Gazeti la "Hannoversche Allgemeine" linaandika: Andrea Nahles ameshusha pumzi japo kidogo. Kwa kumteuwa Katarina Barley awe mshika bendera wa SPD katika uchaguzi wa bunge la Ulaya, mwenyekiti huyo wa chama hicho kikongwe kabisa cha kisiasa nchini Ujerumani amefanikiwa kuutoa mwiba uliokuwa umemsakama kooni. Na wakati pia aliouchagua hakuna bora kama huu; baada ya zilzala katika uchaguzi wa Bavaria, viongozi wa SPD sasa wanavuta pumzi na kuwafumba midomo wale wanaotaka Andrea Nahles na Olaf Scholz waang'atuke.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/INlandspresse

Mhariri. Josephat Charo