1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Trump abadili msimamo kuhusiana na barakoa

22 Julai 2020

Idadi ya maambukizi ya virusi vya corona imepindukia milioni 13 na vifo vilivyotokana na virusi hivyo ni zaidi ya laki sita kote duniani wakati ambapo wanasayansi wako mbioni kutafuta chanjo.

https://p.dw.com/p/3ffaX
USA I Bethesda I Präsident Donald Trump I COVID-19
Picha: picture-alliance/AP/P. Semansky

Kwa sasa baadhi ya chanjo zilizobuniwa ziko katika hatua ya majaribio kwa binadamu.

Tukianzia Marekani, Rais Donald Trump ameubadili msimamo wake kuhusiana na uvaaji wa barakoa na sasa anawataka Wamarekani wazivae kila wanapokuwa katika mikusanyiko. Katika kikao chake cha kwanza na waandishi wa habari cha kuzungumzia hali ya virusi vya corona Marekani baada ya miezi kadhaa, Trump ameonya kwamba kabla maambukizi kupungua nchini humo, hali itakuwa mbaya zaidi.

"Nitaivaa nikiwa kwenye kundi la watu, nikiwa na walinzi wangu nataka kuwalinda pia kwa hiyo nitavaa barakoa, sina tatizo na barakoa. Mtazamo wangu ni huu, kitu chochote kinachoweza kusaidia na bila shaka barakoa inaweza kusaidia, ni kitu kizuri. Sina shida, ninaibeba, ninaivaa, mumeniona nikiivaa mara kadhaa na nitaendelea," alisema Trump.

Rais Bolsonaro wa Brazil anafanyiwa kipimo cha tatu

Trump lakini ameshikilia kwamba virusi hivyo vitatokomea tu wakati mmoja.

Na huko Amerika Kusini katika nchi ambayo imeathirika zaidi, Brazil, maafisa wa afya wameanza majaribio ya miezi mitatu ya chanjo ya corona iliyotengenezwa na kampuni ya madawa ya China Sinovac. Mratibu wa zoezi hilo Dimas Covas anasema iwapo chanjo hiyo itazuia maambukizi na itaonekana kuwa salama, Brazil itapokea chanjo milioni 120 kutoka China kuanzia mwanzoni mwa mwaka ujao.

Brasiliens Präsident Bolsonaro unterzieht sich Corona-Test
Rais wa Brazil Jair BolsonaroPicha: picture-alliance/dpa/E. Peres

Wakati huo huo Rais Jair Bolsonaro ambaye anasema amefanyiwa kipimo cha tatu kubaini iwapo bado anaugua virusi hivyo. Alipokuwa akizungumza na wafuasi wake waliokuwa wamekusanyika nje ya ikulu, Bolsonaro amesema mnamo Julai 15 alifanyiwa kipimo cha pili na akaonekana bado ana virusi hivyo.

Huko Mashariki ya Kati Jordan imesema kuwa itaanza kufungua viwanja vyake vya ndege kuanzia Agosti kwa ajili ya wasafiri wa kimataifa baada ya kufunga mipaka yake mnamo mwezi Machi ili kuzuia kuenea kwa virusi vya corona. Wasafiri kutoka orodha ya nchi zinazosemekana kuwa na idadi ndogo ya maambukizi watalazimika kufanyiwa vipimo masaa 72 kabla kusafiri na kuingia Jordan na watakapofika watapimwa virusi hivyo aidha.

Idadi ya maambukizi imepungua pakubwa Italia

Na huko Afrika kuna wasiwasi kwamba hospitali za Afrika Kusini, nchi iliyo na zaidi ya asilimia 50 ya maambukizi ya bara la Afrika hazitoweza kuhimili idadi ya wagonjwa wa Covid-19 wanaotarajiwa katika miezi miwili ijayo. Afrika Kusini inashikilia nafasi ya tano duniani katika nchi zenye maambukizi mengi zaidi.

Süfafrika Johannesburg | Covid-19 Impfstoff Tests beginnen
Huenda hospitali z Afrika Kusini zikalemewa na mzigoPicha: picture-alliance/AP Photo/S. Sibeko

Barani Ulaya, kuna habari njema kutoka Italia kwani nchi hiyo ambayo wakati mmoja ilikuwa kitovu cha maambukizi na hata vifo duniani, imeandikisha siku ya tatu ya idadi ndogo zaidi ya maambukizi mapya. Ni visa 129 tu vya maambukizi mapya vilivyoandikishwa nchini humo tangu Jumatatu.