Rais Talabani wa Iraq atakutana na Bush | Matukio ya Kisiasa | DW | 25.06.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Rais Talabani wa Iraq atakutana na Bush

Marais wa Marekani na Iraq, George Bush na Jalal Talabani, watakutana punde.

default

Rais wa Iraq, Jalal Talabani.

Rais George Bush wa Marekani leo atakutana na Rais Jalal Talabani wa Iraq na atazungumza pamoja naye juu ya mkataba wa usalama wa muda mrefu ambao, kati ya mambo mengine, utawezesha majeshi ya Kimarekani kubakia Iraq. Kipindi cha Umoja wa Mataifa kubakia Iraq kinamalizika mwisho wa mwaka huu, na Wa-Iraqi wamesema hawataki kukirefusha. Wakati huo huo, watu kumi waliuwawa leo, wakiwemo watumishi wawili wa serekali ya Marekani katika mkutano wa baraza la mji wa Baghdad kwenye eneo ambalo ni ngome ya shehe wa Kishia, Muqtada al-Sadr. Zaidi anayo Othman Miraji...

Msemaji wa Ikulu ya Marekani, Gordon Johndroe, amesema upendeleo wa serekali ya Iraq ni kuwa na mkataba na Marekani juu ya kujiingiza Marekani siku za mbele huko Iraq, kwa hivyo viongozi hao wawili watazungumzia jambo hilo. Nchi mbili hizo zimekuwa zikishauriana juu ya mkataba mpya wa amani ili kuweko msingi wa kisheria kwa wanajeshi wa Kimarekani kubakia Iraq baada ya muda wa kuweko Umoja wa Mataifa utakapomalizika Disemba 31 mwaka huu. Pia kunatakiwa kuweko makubaliano mepya juu ya maingiliano ya kisiasa, kiuchumi na kiusalama baina ya nchi hizo mbili.

Rais Bush na waziri mkuu wa Iraq, Nuri al-Maliki, wiki iliopita walizungumza pamoja kwa njia ya simu na walikubaliana kwamba mazungumzo juu ya mkataba huo yanaendelea vizuri. Tamko hilo lilitolewa baada ya Nuri al-Maliki mwanzoni mwa mwezi huu kuonya kwamba mazungumzo hayo yamekwama kukiweko wasiwasi kwamba Iraq itapoteza mamlaka ya utawala wake. Baadae Marekani iliregeza kamba juu ya ombi la kutaka kinga ya kisheria kwa Wamarekani walioajiriwa na wanaofanya kazi Iraq. Marekani imetaka iwe na vituo vya kijeshi huko Iraq, jambo ambalo limepingwa na Wa-Iraqi wengi. Pia viongozi wengi wa Kishia wamelipinga pendekezo la mkataba huo kwa vile Marekani haitoi uhakikisho wa usalama pindi Iraq itachokozwa na dola ya nje. Maafisa wa Kishia wamekuwa na wasiwasi kwa muda mrefu kama Marekani kweli itasaidia kuhakikisha utawala unaodhibitiwa na Washia huko Iraq unabakia madarakani dhidi ya njama za nchi za Kiarabu na Uturuki zilizo chini ya watawala wa madehehbu ya Kisunni kutaka kuwarejesha Wasunni madarakni huko Iraq.

Na kati ya watu kumi waliouliwa jana usiku katika na mripuko wa bomu katika eneo la ngome ya shehe wa Kishia, Muqtada al-Sadr, mjini Bagdad, wawili walikuwa watumishi wa serekali ya Marekani. Serekali ya Marekani imewalaumu wanamgambo wa Kishia kwa hujuma hiyo ambao inadaiwa wanapewa silaha na fedha na pia mafunzo na Iran. Jambo hilo linakanushwa na watawala wa Tehran.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani, Condoleezza Rice, alisema vifo vya raia wa Kimarekani, mmoja wa kutoka wizara ya mambo ya kigeni na mwengine wa wizara ya ulinzi, ni ukumbusho mchungu juu ya hatari zinazokabiliwa kila siku na Wamarekani katika kuendeleza malengo ya siasa yao ya kigeni inayobishwa. Ilisemwa kwamba lengo la shambulio hilo lilikuwa mwanachama wa cheo cha juu wa baraza la mji wa Baghdad. Haijulikani kama mtu huyo alinusurika.

Rais Jalal Talabani wa Iraq aliwasili Marejkani wiki moja iliopita kwa ajili ya kutibiwa goti lake.
 • Tarehe 25.06.2008
 • Mwandishi Othman, Miraji
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/EQk4
 • Tarehe 25.06.2008
 • Mwandishi Othman, Miraji
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/EQk4
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com