1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Steinmeier ziarani Mashariki ya Kati

Oumilkheir Hamidou
9 Mei 2017

Rais wa shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani anakamilisha ziara yake ya Mashariki ya kati kwa kuyatembelea maeneo ya utawala wa ndani ya Palastina. Kabla ya hapo alizungumza na waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu .

https://p.dw.com/p/2cebs
Deutschland Steinmeier bei Abbas in Ramallah
Picha: Reuters/M. Torokman

Baada ya mazungumzo yake ya kisiasa nchini Israel ambako Frank-Walter Steinmeier alianzia ziara yake rasmi jumapili iliyopita, rais wa shirikisho la jamhuri ya Ujerumani ameelekea katika maeneo ya utawala wa ndani hii leo ambako pamoja na mkewe Elke Büdenbender waliitembelea shule ya wauguzi inayogharimiwa na Ujerumani huko Kubeiba katika Ukingo wa magharibi.

Rais wa shirikisho Steinmeier amelizuru kaburi la kiongozi wa zamani wa utawala wa ndani Yasser Arafat na kuweka shada la mauwa. Kwa mujibu wa mwakilishi wa Ujerumani mjini Ramallah, hii ni mara ya kwanza kabisa kwa rais wa shirikisho la jamhuri ya Ujerumani kulitukuza hivyo kaburi la kiongozi huyo wa zamani wa utawala wa ndani wa Palastina.

Rais wa shirikisho Steinmeier na waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu
Rais wa shirikisho Steinmeier na waziri mkuu wa Israel Benjamin NetanyahuPicha: picture alliance/dpa/Newscom/R. Zvulun

Steinmeier kukutana na Mahmoud Abbas Ramallah

Baadae amepangiwa kukutana na kiongozi wa utawala wa ndani wa Palastina Mahmoud Abbas mjini Ramallah. Mada kuu katika mazungumzo hayo inatarajiwa kuhusiana na jinsi ya kuyafufua mazungumzo ya amani yaliyokwama kati ya Israel na Palastina na mustakbal wa ufumbuzi wa madola mawili. Mazungumzo ya amani kati ya Israel na Palastina yamekwama tangu mwaka 2014. Juhudi za amani za mzozo wa mashariki ya kati ni miongoni mwa mada alizozungumzia rais wa shirikisho Steinmeier alipokutana na waziri mkuu wa Israel Benjamini Netanyahu jumapili iliyopita mjini Jerusalem.

Rais wa shirikisho Frank-Walter Steinmeier na mkewe Elke Büdenbender wakitembelea kituo cha mafunzo cha Givat Haviva
Rais wa shirikisho Frank-Walter Steinmeier na mkewe Elke Büdenbender wakitembelea kituo cha mafunzo cha Givat HavivaPicha: picture-alliance/dpa/B. von Jutrczenka

Steinmeier atetea uhuru wa mtu kuzungumza na amtakaye

Itafaa kusema hapa kwamba wiki mbili zilizopita Benjamin Netanyahu alifutilia mbali mazungumzo yake na waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Sigmar Gabriel akilalamika dhidi ya mazungumzo waziri Gabriel aliyokuwa nayo pamoja na shirika linalokosoa sera za  serikali ya Israel katika maeneo ya wapalastina-"Breaking the Silence".

Steinmeier alizungumza mara mbili na waziri mkuu wa Israel kabla ya kukutana mjini Tel Aviv na wasomi na waandishi vitabu wanaoikosoa serikali na kuutembelea baadae mradi wa amani wa wayahudi na waarabu. Katika mkutano huo walihudhuria pia wawakilishi wa yale mashirika yasiyomilikiwa na serikali waliokutana wiki mbili zilizopita na waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Sigmar Gabriel. Mwishoni mwa mazungumzo hayo, rais wa shirikisho la jamhuri ya Ujerumani ametilia mkazo umuhimu wa kuendelezwa uhuru wa mtu kuzungumza na amtakaye." Rais wa shirikisho Frank-Walter Steinmeier anapanga kurejea Berlin baadae leo.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/dpa/AFP
Mhariri: Iddi Ssessanga