1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JangaAfrika

Rais Samia azindua chanjo ya COVID-19 Tanzania

Hawa Bihoga28 Julai 2021

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amezindua rasmi kampeni ya taifa ya chanjo ya Covid-19 na kuwa wa kwanza kuchanjwa akinuwia kuuhakikishia umma kuwa chanjo hiyo ni salama, wakati mjadala kuhusu chanjo ukihanikiza.

https://p.dw.com/p/3yB1i
Tanzania's President Samia Suluhu Hassan receives her Johnson & Johnson vaccine against the coronavirus disease (COVID-19) at State House in Dar es Salaam
Picha: REUTERS

Ingawaje kuna mjadala mkali unaendelea juu ya chanjo hiyo ya corona, lakini taifa hilo la Afrika Mashariki linaipambazua siku kwa kujidhatiti kwa asilimia mia moja katika jumuia za kimataifa kwamba lipo tayari kupambana na janga la corona kwa kufuata muiongozo iliowekwa na shirika la afya ulimwenguni WHO na sasa likiwa limeidhinisha rasmi chanjo kwa kuanza uchanjaji hiyari.

Katika viwanja vya ikulu ya Dar es salaam Rais Samia amekuwa wa kwanza kuchanjwa chanjo hiyo inayokwenda kwa jina la Jonson Jonson ambayo ilipokelewa na serikali mwishoni mwa juma lililopita zipatazo dozi milioni moja, elfu hamsini na mia nne kutoka nchini Marekani inaonekana kupata upinzani mkali kwa wanaopinga mpango wa chanjo katika kukabiliana na janga hilo.

Soma pia: Aina mpya ya corona yagunduliwa kwa msafiri toka Tanzania

Awali kabla ya kuchoma chanjo hiyo amewaambia watanzania kwamba, chanjo ni imani, hivyo ameipa jukumu wizara ya afya kutoa elimu kwa umma juu ya umuhimu wa chanjo hiyo, huku akisisitiza kuwa bado hali ni mbaya nchini huku mikoa ilioathirikla zaidi ni mpamoja na kilimanjaro, Dar es salaam na Kagera ambapo hadi sasa vifo vinashuhudiwa katika wimbi hili la tatu.

Tansanian Präsident Samia Hassan Suluhu  Impfung
Picha: Ericky Boniphase/DW

"Mimi niko tayari kuchanja sasa hivi," alisema rais Samia alipozungumza kabla ya kuchoma chanjo, na kusema yeye mwenyewe asingekubali kuhatarisha maisha yake iwapo chanjo hiyo ya Jensen isingekuwa salaama.

Upinzani dhidi ya chanjo

Hadi sasa bado kuna vuguvugu linaloendelea katika mitandao ya kijamii na katika mijadala ya ana kwa ana, ikionesha baadhi ya watu kupinga vikali chanjo ya corona, huku msimamo wa mwendazake Rais John Magufuli ambae alionesha kuwa kuna haja ya kuwa na utafiti wa kina kabla ya kukubalina na mpango wa chanjo katika kukabiliana na janga hili ukitumika kuleta uzito wa hoja.

Soma pia:Hatua ya Samia kuhusu Covid ni ya kupongeza 

Waziri wa afya dokta Doroth Gwajima akitumia jukwaa hilo amesema hashangai juu ya hoja na mtazamo hasi unaotolewa na watu kwenye mitandao ya kijamii juu ya chanjo hiyo aina ya Johnson & Johnson, hivyo wataalamu wake wamejipanga vema ili kujibu kila hoja inayotolewa kwa hekima kubwa, kwani kuna haja ya elimu kutolewa kwa kila mmoja mwenye swali.

Tansania Daressalam | Coronavirus | Impfung Hawa Bihoga, DW-MItarbeiterin
Mwandishi wa DW Hawa Bihoga akichoma chanjo katika ikulu ya Dar es Salaam, Tanzania, Julai 28, 2021.Picha: Iddi Ismail/DW

Waziri Gwajima amenukuliwa kwenye mitandao ya kijamii akitetea msimamo wa aliekuwa rais wa nchi hiyo hayati John Magufuli, ambaye alikuwa mpinzani mkubwa wa chanjo, akisema Maguguli hakupinga chanjo ila alikuwa akisisitiza tu haja ya kuwa makini katika kuchagua aina ya chanjo.

Viongozi wengine waliochanjwa ni pamoja na waziri mkuu Kassim Majaliwa, wakuu wa vyombo vya ulinza na usalama, viongozi wa dini, wakuu wa mikoa, viongozi wa chama cha mapinduzi, wataalamu wa afya na hata wanahabari wote walichoma kwa hiyari.

Soma pia: Tanzania yakamilisha miongozo ya utoaji chanjo

Idadi kubwa ya mataifa ya Africa yaliridhia kuingia katika mpango wa chanjo ili kukabiliana na janga la corona ambalo limeendelea kuwaathiri mamilioni ya watu barani humo.

Tanzania ilikuwa ni miongoni mwa mataifa matatu ambayo yalionesha msimamo mkali wa kukataa chanjo hiyo kuingia nchini ambayo ni Burundi na Eritrea. Lakini sasa chanjo ni hiyari kwa mujibu wa mamlaka nchini humo.