1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Samia awakosoa wanaombeza kuhusu miradi ya Magufuli

George Njogopa23 Machi 2022

Kwa mara nyingine Rais Samia amewakosoa vikali wale wanaombeza kwamba hataweza kutekeleza miradi iliyoachwa na mtangulizi wake, akisema watu wanaodhani hivyo hawana upeo wa kufikiri.

https://p.dw.com/p/48vy2
Tansania l Neue Präsidentin Samia Suluhu Hassan
Picha: AP/picture alliance

Rais Samia aliyeko ziarani jijini Dar es Salaam kufungua miradi mbalimbali amesema baadhi ya wale wanaombeza wamekuwa wakimtazama  kwa sura kwamba hatafanikisha miradi hiyo.

Bila kuwataja watu hao Rais Samia amesema haingiii akilini kuona baadhi ya watu wakianzisha chokochoko juu ya ukamilishaji wa miradi hiyo ilihali wakitambua kwamba, miradi hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa ilani ya CCM, chama ambacho amedai kipo madarakani kwa kipindi chochote tangu kuanzishwa kwa miradi hiyo.

''Hata miradi hii ilivyoanzishwa,ilianzishwa awamu ya tano mimi nikiwa makamu wa Rais. Kwa hiyo ni sehemu ya miradi hiyo kuanza kwake na kutekelezwa kwake. Sasa kwa kunitizama sura na kusema kwamba asingeweza kuendesha hii miradi nadhani hekima haikutumika.''

Samia azindua nyumba zaidi ya mia sita Magomeni

Rais Samia ambaye alikuwa akizungumza wakati wa uzinduzi wa nyumba za makazi 644 zilizojengwa kwa pamoja katika eneo la Magomeni amesisitiza kuwa hakuna mradi hata mmoja ulioasisiwa wakati wa utawala uliopita, utasimama.

Hii siyo mara ya kwanza kwa Rais Samia kutumia majukuwa ya wazi kuutetea utawala wake jinsi ulivyojipanga kuendelea kutekeleza miradi yote iliyoasisiwa na mtangulizi wake. Mara kadhaa amekuwa akiwakosoa wale wanaotilia shaka kuhusu kukamilika kwa miradi hiyo akisema kuwa, hata kwa njia ya mikopo ya nje miradi hiyo lazima itekelezwe kwa wakati.

Soma pia→

''Inawezekana anaupinzani mkubwa ndani ya chama''

Rais Samia amezindua nyumba 644 za Magomeni Kota,jijini Dar es Salaam
Rais Samia amezindua nyumba 644 za Magomeni Kota,jijini Dar es SalaamPicha: Getty Images/AFP/Daniel Hayduk

Kauli yake ya kuwa yeye na mtangulizi wake ni kitu kimoja, ndiyo inayowafanya wachambuzi wa mambo kujaribu kudadisi zaidi hasa kutokana na mwelekeo wa sera zake kutofautiana na sera za mtangulizi wake Rais Magufuli aliyekosolewa kwa kutokuwa na mahusiano mazuri na jumuiya za kimataifa.

Mbali na hayo, kuna wale wanaodadisi kuwa hatua ya Rais Samia kurejea mara kwa mara kwa kauli zake hizo, huenda kunaashiria kuwepo kwa hali ya sintofahamu ndani ya chama chake ambacho kinajiandaa kuwa na mkutano mkuu Aprili Mosi mwaka huu.

Mchambuzi Sammy Ruhuza amekuwa na maoni haya kuhusiana na hali hiyo: ''Inawezekana ana upinzani mkubwa ndani ya chama chake,inawezekana kuna wapambe ambao ni wa Magufuli ambao wameona uwepo wa huyu Rais inawazidia wao.''

Miongoni mwa miradi mikubwa inayosubiriwa kukamilishwa ni pamoja na wa ujenzi wa bwawa la maji la Stigler Gorge ambao awali ulielezwa ungeanza kuzalisha umeme mwanzoni mwa mwaka huu. Hata hivyo, wizara ya nishati inasema huenda ukachelewa kuanza uzalishaji wake kutokana na sababu kadhaa.