1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Saleh aitisha uchaguzi wa mapema

26 Septemba 2011

Rais Saleh ametaka ufanyike uchaguzi wa mapema katika hatua ambayo huenda isiwaridhishe waandamanaji wanaomtaka aondoke madarakani.

https://p.dw.com/p/12gNl
Rais wa Yemen, Ali Abdullah SalehPicha: dapd

Akizungumza baada ya siku sita za wimbi la machafuko yaliyosababisha vifo vya watu zaidi ya 100, rais Saleh alisema amejitolea kwa dhati kukabidhi madaraka kupitia uchaguzi. Lakini tangu mzozo wa kisiasa nchini Yemen ulipoanza mwezi Januari mwaka huu wakati waandamanaji walipojitokeza mabarabarani kumshinikiza ajiuzulu, kiongozi huyo ametoa mapendekezo kadhaa kumaliza machafuko nchini humo, lakini hakutekeleza lolote linalomtaka aachie madaraka.

Rais Saleh, aliyerejea Yemen Ijumaa iliyopita kutoka Saudi Arabia, ambako alikuwa akitibiwa baada ya majeraha aliyoyapata wakati wa jaribio la kumuua, alisisitiza kukubali kwake mpango uliopendekezwa na baraza la nchi za Ghuba linalomtaka akabidhi madaraka. Alisema makamu wa rais ndiye mwenye mamlaka ya kuzungumza na upinzani.

Katika hotuba ya kuadhimisha miaka 49 ya mapinduzi ya Septemba 26 mwaka 1962 yaliyoshushudia Yemen ikitangazwa kuwa jamuhuri, rais Saleh pia alisema na hapa namnukulu, "Tuelekee sote kwenye mazungumzo, maelewano na kukabidhi madaraka kwa amani kupitia chaguzi na uchaguzi wa mapema wa urais," mwisho wa kumnukulu rais huyo wa Yemen.

Mfalme Abdullah wa Saudi Arabia amewataka viongozi wa Yemen kuutekeleza mpango wa Baraza la nchi za Ghuba utakaomuwezesha rais Saleh kukabidhi madaraka kwa makamu wake.

König und Premierminister von Saudi-Arabien Abdullah ibn Abd al-Aziz Al Saʿud im Juni 2010
Mfalme Abdullah wa Saudi ArabiaPicha: picture alliance/dpa

Rais Saleh alijifunika kitambaa kichwani na shingoni na mpangilio wa maua ukafunika mikono yake, pengine kwa lengo la kuyaficha makovu ya moto aliyoyapata wakati wa shambulio la bomu dhidi ya ikulu yake.

Waandamanaji wagadhabishwa na hotuba

Waandamanaji walikusanyika katika mahema kwenye kambi yao kubwa katikati ya mji mkuu Sanaa, wakipiga kelele za kumtaka rais Saleh aondoke, wakiwa wamevunjwa moyo na matamamshi yake ambayo hayakuwa na tofauti yoyote na kauli zake za awali. Waandamanaji wamechoshwa na malengo ya rais huyo tangu kuuliwa watu 17 Jumamosi iliyopita, wakati vikosi vya serikali vilipoishambulia kambi yao mjini Sanaa.

Jemen Sanaa Protest Demonstration Saleh
Waandamanajni mjini SanaaPicha: dapd

Wanajeshi wawili waliuwawa kwenye mapigano katika kitongoji cha kibiashara cha Taiz na mwingine wa tatu akauliwa katika mkoa wa Abyan kabla rais Saleh kutoa hotuba yake. Wanajeshi wawili waliwaua wapiganaji wawili wa kikabila na kuwajeruhi waandamanaji 18 wanaoipinga serikali ndani na nje ya mji mkuu Sanaa, hivyo kuongeza hofu ya kuzuka vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Yemen.

Mjini Sanaa wanajeshi walitumia risasi za moto dhidi ya maelfu ya waandamanaji waliokuwa wakiandamana mabarabarani.

Mwandishi: Josephat Charo/RTRE/AFPE

Mhariri: Hamidou Oummilkheir